Habari za Punde

*MAMA ASHA BILAL AADHIMISHA SHEREHE ZA MIAKA 10 YA TAASISI YA MAZNAT NA KUZINDUA SHULE YA UREMBO YA TAASISI HIYO

 Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal, akiwasili kwenye Ukumbi wa VIP wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam jana jioni kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, kama Mgeni rasmi sambamba ya kuzindua Shule ya Taasisi hiyo inayofundisha masuala ya urembo.
 Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal, akishiriki kukata Keki na Maza Sinare, ambaye ni mmiliki wa Saluni ya Maznat, ikiwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam, jana Mei 5, 2013, sambamba na sherehe hizo pia Mama Asha, alizindua rasmi shule ya masuala ya Urembo inayosimamiwa na Taasisi hiyo. 
 Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam, jana, sambamba na sherehe hizo pia Mama Asha, alizindua rasmi shule ya masuala ya Urembo inayosimamiwa na Taasisi hiyo.
 Mama Asha, akipongezwa na wageni waalikwa baada ya kusoma hotuba yake ukumbini hapo.
 Sehemu ya wageni waalikwa waliohudhuria sherehe hizo.
 Mmiliki wa Saluni na Taasisi ya Maznat, Maza Sinare, akiwalisha keki baadhi ya wageni waalikwa wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam jana, sambamba na sherehe hizo pia Mgeni rasmi mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha, alizindua rasmi shule ya masuala ya Urembo inayosimamiwa na Taasisi hiyo.
 Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal (kulia) akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi shule ya masuala ya Urembo, wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam, jana. Shule hiyo inasimamiwa na Taasisi hiyo.luni na Taasisi hiyo ya Maznat, Maza Sinare. Kwa matukio ya picha zaidi bofya hapo chini.

 Msanii wa muziki wa Taarab, Mzee Yusuph, akiimba jukwaani kutoa burudani wakati wa sherehe hizo.
 Mama Asha Bilal, akiwaongoza wanawake waliohudhuria sherehe hizo katika kucheza muziki wa taarab, burudani iliyokuwa ikitolewa ukumbini hapo na Mzee Yusuph.
 Msanii wa muziki wa Injili, Bahati Bukuku, akiimba jukwaani kutoa burudani wakati wa maadhimisho hayo.
 Baadhi ya wadau wa Maznat, waliohudhuria sherehe hizo, wakisebeneka na miondoko ya taarab, ukumbini hapo.
 Baadhi ya wadau wa Maznat, waliohudhuria sherehe hizo, wakisebeneka na miondoko ya taarab, ukumbini hapo.
 Baadhi ya wadau wa Taasisi ya Maznat, wakihesabu fedha zilizopatikana baada ya kuchangwa na washirika wa karibu wa Taasisi hiyo ukumbini hapo jana wakati wa sherehe hizo kwa ajili ya kusaidia mfuko wa kusaidia Watoto Yatima ulio chini ya Taasisi hiyo, ambapo zilipatikana jumla ya sh. milioni 22.
 Mmiliki wa mtandao wa Mafoto Jr, Nasma Mafoto (kushoto) akiwa na wadau waliohudhuria sherehe hizo.
 Wasanii wa kundi la The Voice, wakitoa burudani ya kuimba 'Akapera' jukwaani wakati wa sherehe hizo.
 Mabaunsa wakifungua na kuripua Shampeni kwa pamoja ikiwa ni sehemu ya kusherehesha ukumbini hapo.
 Maznat, akipozi kwa picha na wafanyakazi wake...
 Mama Asha Bilal, akiwaongoza wageni waalikwa kugonganisha glasi wakati wa sherehe hizo.
 Kwa amani na furaha ya kutimiza miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, wageni waalikwa waligonganisha glasi zao.
Cheeeeeeeeaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaazzzzzzzzzzzzzzzzzzzzzzzzz!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

HOTUBA YA MHE. MAMA ASHA BILAL, KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA KUMI YA KAMPUNI YA MAZNAT.   TAREHE 05 MEI, 2013, UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE DAR ES SALAAM.
Waheshimiwa Mabalozi,
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Waheshimiwa Wabunge,
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke,
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania,
Viongozi wote wa Taasisi mbali mbali nchini,
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana.
Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uzima na afya tukaweza kujumuika pamoja katika hafla hii.  Pili, naomba kutoa shukrani zangu binafsi kwa heshima niliyopewa kuwa Mgeni Rasmi, katika hafla hii ya kuadhimisha miaka kumi ya kampuni ya Maznat Bridal Care.  
Nimefarijika sana kujumuika nanyi leo katika hafla inayotupa fursa nzuri sisi kama wanawake kujadili mambo mbalimbali yanayotugusa, kusherehekea mafanikio aliyopata Maznat na sisi sote, kufahamiana na kufurahi pamoja.  

Natoa pongezi zangu kwa wanawake wote mliohudhuria leo, kwani mmejitokeza kwa wingi kutoka katika sekta mbalimbali za biashara.

Mchango wa mwanamke katika familia na jamii yetu huchukuliwa kama jambo la kawaida, bila kuchanganua majukumu mazito aliyo nayo kila siku ya kulea watoto, kuzalisha mali, kukuza kipato, kuongeza nafasi za ajira, na shughuli nyengine nyingi.  

Licha ya kuwa mwanamke ndiye nguzo kubwa ya nguvu kazi kifamilia na katika ngazi nyengine, lakini bado wanawake ndiyo wanaongoza kwa umasikini.  Ni wazi kuwa ujira kwa wanawake haulingani na mchango wetu kiuchumi.  Hata hivyo, wakati umefika wa sisi wanawake kufanya shughuli zenye kipato ili kufidia, angalau kwa kiasi cha juhudi zetu.  

Kwa maana nyengine tuhakikishe sisi tunajilipa ujira kwa kazi zetu.
Kutokana na hilo, nichukue nafasi hii kumpongeza Bi. Mazna Sinare kwa ubunifu wake katika sekta ya urembo, na kuendeleza kasi ya maendeleo ya sekta hii muhimu katika uchumi wetu licha ya changamoto mbalimbali alizokuwanazo kama mama wa familia, na mwanamke katika jamii.  

Nimevutiwa sana na juhudi kubwa alizozifanya mpaka kufikisha miaka kumi ya huduma anazozitoa, na vile vile kufanikiwa kuanzisha mafunzo ambayo yataendeleza utaalamu wa sekta hii muhimu.  

Nakupongeza sana kwa kazi kubwa kwani wahenga wanasema “ukiona vyaelea ujue vimeundwa”. Aidha nakuombea kwa Mwenyezi Mungu muweza wa yote azidi kukubariki na akuzidishie mafanikio mema. 
Amin.
Hafla hii ya leo ni kiungo muhimu katika kutafsiri kwa vitendo Maazimio ya Beijing, pamoja na Malengo na Dira ya Maendeleo ya Taifa (Tanzania Development Vision 2025) na mikakati mbalimbali ya kitaifa ya kuondoa umasikini.  
Ustadi wa kupanga shughuli hii kwa kuweka nafasi kwenye ratiba, kusikia mafanikio ya wanawake wenzetu katika ujarisiamali, maonesho ya bidhaa mbalimbali na kupata elimu ya huduma za kifedha umenifurahisha sana, kwani sote tutapata elimu zaidi katika kujiendeleza kwenye shughuli zetu za kijasiriamali.

Katika kutekeleza malengo na majukumu yeke, na ili kufikia miaka kumi hii leo, Mazna amepitia changamoto mbalimbali ambazo zingeweza kumfanya akate tamaa katika biashara yake.  
Moja ya changamoto kubwa ni hali duni ya kiuchumi miongoni mwa wanawake wajasiriamali, changamoto ambayo wanawake wengi wajasiriamali mnayo hapa nchini.  
Hata hivyo, Maznat ametuonesha mfano mzuri kwa kuwa ameweza kumudu changamoto hii, kwa kutumia vizuri fursa zinazotolewa na taasisi za kifedha hapa nchini. 
Natoa wito kwa wanawake wenzangu kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wenzetu kumudu changamoto mnazozikabili.

Naomba nichukue fursa hii kuwaasa taasisi za kifedha hapa nchini kuongeza juhudi za kutoa mikopo kwa wanawake wajasiriamali, na pia kuhakikisha kuwa riba zinazotolewa zinaruhusu wajasiriamali hawa kukua kibiashara na si kuwakandamiza.  
Ni muhimu pia kwa wanawake wajasiriamali kuchangamkia fursa zinazotolewa na taasisi za kifedha, nawaomba mikopo mnayopata muitumie kwa umahiri ili kuweza kufikia malengo yenu katika ukuaji wa biashara.

Usawa wa kijinsia katika elimu na fursa za kiuchumi imeendelea kuwa changamoto kubwa, ambayo wanawake duniani kote wamekuwa wakipambana nayo.  Hatua kubwa mpaka sasa imefikiwa katika kuwakomboa wanawake kutoka kwenye umasikini.  
Hata hivyo, bado wanawake wengi zaidi wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za elimu na umasikini wa kipato.  Hivyo, juhudi kubwa zinahitajika kwa kila mmoja wetu kufanikisha majukumu yetu katika fursa tulizonazo.  

Tunatambua kabisa kwamba wanawake wanaposhiriki kikamilifu katika shughuli za jamii, uchumi wa nchi hukua zaidi.  Siku ya leo ni nyenzo muhimu sana katika kuwawezesha wanawake kujifunza kutoka kwa wengine walivyofanikiwa, kubadilishana uzoefu na kuelimishana.

Napenda kuwakumbusha juu ya nguvu kubwa ya wanawake katika kulisaidia Taifa letu kuimarika kiuchumi na kujitegemea.  Ushiriki wenu katika mapinduzi ya kiuchumi, uwe ni kipaumbele katika mipango yenu ya kila mwaka.  Bidhaa na huduma mnazotoa muongezee uthamani wake ili tuweze kumudu changamoto za ushindani katika soko la ndani na dunia.  

Tujitahidi biashara zetu tuziendeshe kwa kutumia teknolojia bora, na kufuata ushauri wa wataalamu wa ujasiriamali.  Tutumie vyuo vya mafunzo vilivyopo hapa nchini kujiendeleza, vyuo ambavyo tayari vinatoa ujuzi mbalimbali kwenye ujasiriamali. Pia tuwe makini katika kutunza mitaji yetu na kutumia huduma za kifedha vyema ili kuimarisha biashara zetu.  

Vile vile napenda kutumia fursa hii kuwaasa akinamama kwa ujumla, kutokatishwa tamaa na vikwazo mnavyokumbana navyo katika maisha.  Ni muhimu tuwe na mipango mizuri ya maendeleo, na kutumia muda wetu vyema ili kujiletea mabadiliko katika kila nyanja, tusibweteke na kupoteza wakati.

Baada ya kusema haya napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa kamati ya maandalizi, uongozi na wafanyakazi wa Maznat Bridal Care, kwa sherehe nzuri iliyofana sana.  Aidha, nawapongeza wanawake mliofika hapa leo kwa usikivu na uchangamfu wenu, pamoja na watoa huduma na burudani mbalimbali.  Nawaomba tuendelee kudumisha ushirikiano wetu katika kukuza uchumi wa taifa letu.  Natangaza sasa sherehe za miaka kumi ya Maznat zimefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.