Na Mwandishi Wetu, Dar
KLABU ya Yanga imechukua maamuzi magumu baada ya kuwakata mshahara wachezaji wake wawili, Simon Msuva na David Luhende, kiasi cha Sh. 200,000 kila mmoja.
Msuva na Luhende, wamelimwa kiasi hicho cha fedha kutoka katika mishahara yao baada ya kukutwa na hatia na kukiuka mikataba yao kwa kucheza mechi za mchangani maarufu kama ndondo.
Chanzo cha habari hizi za uhakika kutoka ndani ya klabu ya Yanga zinaeleza kuwa, Msuva na Luhende waliamua kujiachanganga katika moja ya mechi za uswahilini katika moja ya timu za mtaani kwao katika michuano ya mchangani jambo ambalo lilishazuiliwa na uongozi wa Yanga.
“Ukiachana na uongozi kukataza, lakini suala hilo liko katika mikataba yao. Unaweza kusema wamekiunga mikataba yao, ndiyo maana utaona adhabu imekuwa kubwa ili iwe fundisho kwa wengine.
“Luhende alikuwa akimlalamikia kocha kwamba fedha alizokatwa ni nyingi sana, lakini uongozi na hata kocha mwenyewe tumesisitiza adhabu iendelee kubaki hivi,” kilieleza chanzo.
Ingawa wachezaji hao hawakutaka kulizungumzia suala hilo, lakini Yanga imeahidi kupambana na tatizo hilo la wachezaji wake kucheza mechi za mchangani.
Uamuzi huo unatokana na baadhi ya wachezaji wa ligi kuu, kugundulika huumia wakati wakiwa katika mechi zao hizo za ndondo na kuzifanya klabu zao kuingia gharama kuwatibia.
Tatizo la wachezaji kucheza mechi za mchangani kwa ajili ya kujipatia malipo ya ziada limeendelea kuwa kubwa katika timu mbalimbali za ligi kuu hapa nchini.
Miongoni mwa wachezaji wa Ligi Kuu waliowahi kukutwa na kashfa hii, tena wakati timu yake ikielekea kucheza mechi ya Ligi Kuu ni Haruna Moshi 'Boban'. Wengine ni Ramadhan Ledondo, Shaban Kisiga, Shamte Ally, Said Morad, Juma Nyosso na Juma Kijiko.

No comments:
Post a Comment