Habari za Punde

*SERIKALI KUTATUA WIZI WA FEDHA ZA BENKI KWA NJIA YA MTANDAO


Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.

Immaculate Makilika- Maelezo.
SERIKALI  imesema kwamba Benki ya NMB inatarajia kuanzisha utaratibu wa kutuma ujumbe wa simu  kwa wateja  kupitia simu zao (Bank massage) pindi mteja atakapofanya muamala  ili yule mwenye akaunti aweze kukubali  au kukataa au kufahamu kuwa kipindi  hicho akaunti yake  inatoa au inatumika kutoa fedha.

 Aidha, Serikali imefafanua kuwa  imezitaka benki zote kutumia  teknolojia  ya kisasa ya (Euro Mastercard Visa-EMV Compliant) ambayo hutumia mfumo wa “chip based” na kuachana  na mfumo wa kizamani  unaotumia “magnetic stripe”. Ambao kwa sasa umepitwa na wakati na ni rahisi kwa wahalifu kuuchezea na kuiba  fedha za wateja.

Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma wakati Naibu Waziri wa  Fedha, Saada Mkuya,  alipokuwa akijibu swali la Kidawa Hamid Saleh(Viti Maalum - CCM) alipouliza je,Serikali ina mkakati gani wa kupambana na matatizo ya wizi wa Mabenki kwa njia ya mtandao.

 Alisema   kupitia Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali katika juhudi za kupambana na  tatizo la wizi kwa njia ya mtandao.

Aidha Naibu waziri alisema hatua zingine za kukabiliana na tatizo hili la mabenki ni kuweka mfumo  wa “Anti- Skimming  Devices ambapo mfumo  huu unazuia mwizi kugundua namba ya siri ya mteja(PIN), na kwa upande wa Benki ya NMB imeamua kusimamisha utaratibu wa “swapping” uliokuwa unatekelezwa na kampuni ya simu ya Airtel.

Katika swali la nyongeza Kidawa aliuliza pia kama Serikali imewapa  adhabu yeyote wafanyakazi wa NMB na Airtel waliobainika kuhusika na upotevu wa fedha za wateja na je kama Benki ya NMB  itarejesha fedha hizo kwa wateja?

Mkuya alijibu maswali hayo kwa kusema kuwa bado hajajua namna gani NMB na Airtel imewaadhibu wafanyakazi wak, isipokuwa kuhusu kurejesha fedha kwa wateja  ndio NMB inafanya hivyo.

Aidha Naibu waziri huyo aliendelea kwa  kusema  Serikali inakamilisha sheria ya wizi kwa njia ya mtandao (Cyber Crime Act) ambayo itasaidia  kupunguza tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.