Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla (kulia)
akihoji jambo kwenye chumba cha mapokezi katika Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa
Lindi, wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa wiki mkoani Lindi.
Kaimu Muuguzi Mkuu wa
Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Damasiana Msalla akimuongoza Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi
Kigwangalla kuelekea kwenye wodi za hospitaliwakati wa ziara ya kushtukiza
aliyofanya mkoa wa Lindi. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Muuguzi Kiongozi wa wodi ya wazazi katika
Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Getrude Mangosongo (wa kwanza kulia)
akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kushoto) alipotembelea wodi ya
akinamama wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa wiki mkoani
Mtwara. Kushoto ni Daktari wa zamu kitengo cha dharura hospitalini hapo,Dkt.
Ester Tumwanga na wa pili kulia ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa
wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa.
****************************************
Na Mwandishi Wetu, Lindi
Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Hamisi Kigwangalla amefanya ziara ya kushtukiza mwishoni mwa katika
hospitali za Rufaa za Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kujifunza namna
wanavyofanya kazi ili Serikali iweze kuboresha na kutoa wa huduma bora za afya
nchini.
Akifanya majumuisho ya
ziara hiyo Dkt. Kigwangalla amesema kuwa amefurahishwa na namna hospitali hizo
zinavyofanyakazi ya kuwahudumia wananchi ya kuhakikisha wanapata tiba ya
uhakika katika masuala ya afya.
“Nimefurahishwa na namna
Hospilali ya Rufaa ya Sokoine ya mkoa wa Lindi namna wanavyofanyakazi
wanavyotoa huduma, kila ofisi niliyofika madaktari walikuwepo na wanafanyakazi”
alisema Dkt. Kigwangalla.
Licha ya kufanya ziara
ya kushtukiza katika hospitali hiyo, Dkt. Kigwangalla alisema kuwa amefurahishwa
na kitendo cha kuwakuta madaktari wa zamu na watoa huduma wote wapo katika
maeneo yao ya kazi katika hospitali ya Sokoine Lindi mkoani na Ligula ya Mtwara
kitu ambacho kinawapa faraja wagonjwa pamoja na jamaa zao wanaohitaji kupata
huduma za afya ikiwemo huduma ya dharura anayohitaji kupewa mgonjwa kulingana
na tatizo lake.
“Ziara tunazozifanya
katika hospiltali za rufaa, mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati, lengo
letu ni kujifunza namna zinavyotoa huduma za afya kwa wananchi wetu ili baadaye
kuona ni maboresho gani yafanyike na hatimaye kutoa huduma bora zenye tija na
kwa wakati kwa wananchi” alisema Dkt. Kigwangalla.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kigwangalla ameziagiza
hospitali zote za mikoa nchini kote waige kutoka mkoa wa Lindi namna hospitali
hiyo inavyotoa huduma kwa haraka na kwa wakati kwa kutumia mfumo wa
kielekroniki kuanzia mgonjwa anapopokelewa chumba cha mapokezi hadi anapomaliza
kupata huduma na kuruhusiwa.
Faida
ya kutumia mfumo huo wa kielekroniki ni pamoja na kuongeza makusanyo kupitia
kwa wagonjwa wanaotumia huduma ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wale
wanajilipia wenyewe, makusanyo yanayopatikana yanatumika kuboresha utoaji wa
huduma ikiwemo kununua dawa na vifaa tiba kwa wakati, kutoa motisha kwa
wafanyakazi pamoja na kupunguza urasimu usiowa lazima kwa wagonjwa.
Licha
ya mafanikio hayo katika hospitali za rufaa za mikoa ya Lindi na Mtwara, hospitali
hizo zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madaktari bingwa ambapo hadi sasa Hospitali
ya Sokoine ina Daktari Bingwa mmoja na Hospitali ya Ligula mkoani Mtwara ina
madaktari Bingwa wawili licha ya ukubwa wa mikoa hiyo pamoja na kuhudumia wagonjwa
kutoka nchi jirani ya Msumbiji.
Katika
kutatua changamoto hiyo, Dkt. Kigwangalla amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa (RAS)
yote kuandaa vyumba vya kufanyia upasuaji pamoja na vifaa tiba na kuandaa
nyumba watakapokaa madaktari bingwa ambapo ameahidi Serikali itaanza kuwapangia
vituo madaktari hao kwa kuanzia na mikoa ambayo imejipanga ili waanze kutoa
huduma mara moja.
Akizungumzia namna
walivyofanikiwa kutoa huduma bora, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya
Sokoine ya mkoa wa Lindi Dkt. Evaristo Kasanga alisema kuwa wameboresha namna
ya kukusanya mapato hospitalini hapo kwa kufunga mashine za kielekroniki
zinazopelekea wakusanye sh.milioni 24 kwa mwezi tofauti na hali livyokuwa hapo
awali ambapo zilikuwa zinakusanywa chini ya sh.milioni 10 kwa wateja wanaotumia
mfuko wa bima ya afya.
Mafanikio ya Hospitali
ya Rufaa ya Sokoine ya mkoa wa Lindi yamejengwa juu ya falsafa yao inayosema
“Sisi watumishi wa Sokoine tunaamini kwamba monjwa ndiye tajiri yetu, tunaahidi
kuwa tutatoa huduma bora kwa wagonjwa wetu bila ubaguzi, hatupokei wala kutoa
rushwa”.
Kwa upande wa makusanyo
ya kawaida, Dkt. Kasanga alisema kuwa yamefikia sh.milioni 40 pesa tasilimu
ikilinganishwa na hali livyokuwa hapo awali ambapo zilikusanywa chini ya
sh.milioni 8 kwa mwezi.
“Hatua hiyo imesaidia
kuboresha utoaji wetu wa huduma kwa kuanzia na usafi wa mazingira, mifumo ya
kisasa ya mawasiliano ndani ya hospitali ili kurahisisha mawasiliano kati ya
wagonjwa na wafanyakazi, wagonjwa kwa wagonjwa, wafanyakazi kwa wafanyakazi
pamoja na masuala yote ya dharura kama daktari anahitajika kutoa msaada” Dkt.
Kasanga.
Aidha, Dkt. Kasanga alisema kuwa hospitali
hiyo imefanikiwa kuwa mshindi wa pili kwa utoaji wa huduma bora Tanzania kwa
mwaka 2015 ambapo wamezawadiwa kikombe cha ushindi wa nafasi hiyo na
wamejipanga kuanzia Januari 2016 kuachana na mfumo wa watumishi kusaini kwenye vitabu
wanapofika kazini badala yake wataanza kutumia mfumo wa kusaini kwa kuweka
alama za vidole kwenye mashine maalum (Biometric) ambayo imefungwa na Shirika
la Miradi la Ujerumani la GIZ hatua itakayorahisisha usimamizi wa mahudhurio
kazini, kutoa huduma sahihi kwa wagonjwa na kwa wakati.
Naye Kaimu Mganga Mkuu
wa Mkoa ambaye pia ni Daktari wa Kinywa na Meno Hospilali ya Rufaa ya Sokoine
ya mkoa wa Lindi Dkt. Hussein Athuman akitoa taarifa ya ugonjwa wa kipindupindu
alisema kuwa hali inaendelea vizuri na idadi ya wagojwa imepungua kwa hatua
inayoridhisha.
“Hali ya ugonjwa wa
kipindupindu hadi mwishoni mwa wiki ilikuwa ni nzuri na tunaendelea kuisimamia
ipasavyo, wilaya ya Kilwa ilikuwa na kesi za wagojwa wapya watatu ambapo mmoja
tayari amesharuhusiwa kurudi nyumbani, manispaa ya Lindi kulikuwa na mgonjwa
mmoja ambaye naye amesharuhusiwa” alisema Dkt. Hussein.
Ugonjwa wa kipindupindu
mkoani Lindi umeathiri wilaya tatu za Manispaa ya Lindi, Kilwa na Lindi
Vijijini ambapo wilaya ya Kilwa ndiyo imeathiriwa zaidi kuliko wilaya nyingie
kutokana na ukaribu wa wilaya hiyo na mkoa wa Dar es salaam ambapo ugonjwa huo
uligundulika mapema mwezi Augosti mwaka huu.
Aidha, Dkt. Hussein alisema
kuwa mkoa huo umefanikiwa kusimamia ipasavyo na kuzuia maambukizi ya mapya ya ugonjwa
huo yasitokee na kusambaa kwa kufanya usafi mahali pote katika makazi ya watu,
hospitali, vituo vya afya na zahanati kama desturi ya mkoa huo wakichagiwa na
agizo la kufanya usafi Desemba 9, 2015 la Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Zaidi ya hayo, Dkt.
Hussein alisema kuwa waliweka dawa katika visima vyote vya maji hatua ambayo
imesaidia kupunguza kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindi mkoani humo.
Kwa niaba ya uongozi,
wafanyakazi na wananchi wa mkoa wa Lindi, Dkt. Hussein amewashukuru wadau wa
maendeleo kwa kuendelea kuwaunga mkono kwa kuboresha mazingira ya hospitali ya
Sokoine wakiwemo wabunge, washirika wa maendeleo wakiongozwa na Shirika la Miradi la Ujerumani la Giz kuendelea
kuwaunga mkono katika kuwahudumia wananchi.



No comments:
Post a Comment