Habari za Punde

AFRIKA YAUNGANISHA NGUVU KUPAMBANA NA UGAIDI

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stegomena Tax (watatu kutoka kulia), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wanne kutoka kulia),wakiwa katika picha ya pamoja  na ujumbe uliowakilisha nchi ya Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi, Amani na Usalama wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika uliofanyika Makao Makuu ya umoja huo nchini Ethiopia. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 
**********************************************

Na Mwandishi Wetu, Ethiopia

Mawaziri wa Ulinzi, Amani na Usalama kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wameazimia kuanzisha jeshi la pamoja na kituo ili kupambana na changamoto ya ugaidi katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Kauli hiyo imetolewa nchini Ethiopia na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt.Stegomena Tax baada ya kumalizika kwa Mkutano wa mawaziri hao ambao hapo awali ulitanguliwa na mkutano wa wataalamu ukijumuisha Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka nchi wanachama wa umoja huo.

“Tuna tatizo la ugaidi kusini mwa nchi yetu lakini likiwa zaidi upande wa Msumbiji, lakini kama mnavyofahamu tatizo la ugaidi sio la nchi moja na nguvu ya nchi moja peke yake inakua vigumu kutokana na jinsi magaidi wanavyofanya kazi zao, tumejadili na kwa kutambua umuhimu wake  imepelekea kuwa na pendekezo la kuanzisha kituo na   jeshi la pamoja ambapo nchi wanachama watachangia askari ili kupambana na changamoto ya ugaidi lakini na changamoto nyingine za ulinzi na usalama kwa kubadilishana taarifa, uzoefu, kutoa mafunzo ambayo hiyo  itaongeza nguvu katika mapambano hayo.”alisema Dkt. Tax

Akizungumza juu ya ushirikiano wa nchi za Afrika kukabiliana na changamoto za uhalifu unaovuka mipaka, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema wameweka mikakati mbalimbali huku akiweka wazi jitihada za pamoja katika kupambana na ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya.

“Katika mambo ambayo tumeazimia kuyapa mkazo maalumu kupitia vikosi vyetu ni suala nzima la ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya kwa ujumla wake na imekua jambo la faraja kuona nchi zote wanachama wamekubaliana na wazo hilo huku tukisubiri idhini ya Wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya afrika kutoa maamuzi katika kikao kinachotarajiwa kufanyika muda si mrefu kutoka sasa.” alisema Waziri Masauni

Akielezea majukumu waliyopeana Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka nchi wanachama,Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema wao kama wakuu wa vyombo wameazimia kubadilishana taarifa hasa kwa uhalifu unaovuka mipaka.

“Tumezungumzia suala uhalifu Afrika na hasa yale makosa yanayovuka mipaka na moja kati ya makosa ambayo yamejitokeza kwa wingi sana ni ugaidi, ugaidi tumeuzungumza kwa mapana sana kwa sababu utaona nchi nyingi sana zimeathirika na ugaidi lakini unaweza kuangalia nchi kama wenzetu Msumbiji, Afrika Magharibi ugaidi umekua ni mkubwa sana, kwa hiyo suala ambalo limesisitizwa katika hili ni suala la kubadilishana taarifa ni suala la msingi sana na huwezi kupambana na ugaidi bila kubadilishana taarifa maana ni makosa ambayo leo wanafanya hapa kesho anaondoka anaenda kufanya nchi nyingine.”

Ujumbe wa Tanzania katika  Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stegomena Tax, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Meja Jenerali Jacob Mkunda akimuwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.