Habari za Punde

BANZA STONE AIBUKIA JUKWAA LA TWANGA*Awapagawisha mashabiki*Wamzonga baada ya kushuka jukwaani

Banza (kushoto) akisindikizwa na mpambe wake mara baada ya kushuka jukwaani, huku akizongwa na mashabiki wake......
Banza Stone akiwapagawisha mashabiki jukwaani....
Ukianza kuimba wapagawishe na Mtu Pesa.....utaona....Banza Stone (kushoto) akiteta jambo na mwanamuziki wa Twanga Kalala Junior.

Na SPM
MWANAMUZIKI mahiri wa miondoko ya Dansi nchini, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’, juzi aliwachengua mashabiki wa muziki wa dansi baada ya kutinga katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni, wakati wa michezo ya Bonanza na kupanda katika Jukwaa la Bendi ya African Stars, ‘Twanga Pepeta’ na kuimba vibao vyake alivyotunga wakati akiwa na bendi hiyo.

Banza alizua gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wake waliokuwepo kwenye viwanja hivyo ambao wengi wao hawakuthubutu kuvumilia kukaa kwenye viti wakati mwanamuziki huyo akighani baadhi ya vipande vya rapu zake na nyimbo zake zilizopata kutamba siku za nyuma.

Ama kwa hakika sauti yake ilikuwa ni kivutio kwa kila aliyekuwepo viwanjani hapo na hasa wengi wao wakiwa hawaamini kile walichokuwa wakikisikia kutoka kwa Banza kutokana kuugua kwa kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu na wakiwa hawaamini kama angeliweza kupanda jukwaani na kuimba kwa sauti ile ile waliyoizoea kutokana na kutokuwa na nguvu za kutosha.

Banza aliimba vibao vya bendi yake mpya na Bambino Sound na kibao cha Mtu Pesa alichoimba wakati akiwa na bendi hiyo, ambacho ndicho hasa kilichowainuma mashabiki wote katika viti, na kunogesha zaidi alipofikia katika rapu iliyoimbwa na swahiba wake Msafiri Diouf.

Kilipofikia kipande hicho alianza kuimba mwanamuziki Kalala Junior, kisemacho “Uliniacha na mutoto wangu mudogo Vanesa eeh”, na kabla hajaingia sentensi ya pili ya rapu hiyo ghafla aliibuka Diouf na kudaka maiki na kuendeleza rapu hiyo iliyofanya mashabiki kushangilia bila kikomo huku maswahiba hao wakikumbatiana jukwaani wakati wakiimba na kucheza pamoja.

Mara baada ya kumalizika kwa wimbo huo Banza alishuka jukwaani huku akiwa na msimamizi wake na huku akizongwa na mashabiki ambao kila mmoja alitamani kumgusa na kumtunza pesa japo tayari alishashuka jukwaani.

Aidha Banza aliseama kuwa bado anaendelea na mazoezi madogomadogo ili kujiweka sawa kiafya na kurejesha nguvu na ndiyo maana anathubutu kutoka nyumbani na kutembea katika kumbi za starehe na kujaribu kupanda jukwaani ikiwa ni moja ya mazoezi yake kabla ya kurejea rasmi katika jukwaa la ushindani wa dansi.

Tukumbukie enzi za Mtu Pesa mwana wane...........Banza Stone (kushoto) akiimba na Swahiba wake Msafiri Diouf jukwaani.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.