Habari za Punde

*MWENYEKITI WA CCM RAIS DKT JAKAYA KIKWETE AWASILI DODOMA KUANZA VIKAO VYA CHAMA, AZUNGUMZA NA KUSHIRIKI CHAKULA CHA USIKU NA WABUNGE WA CCM DODOMA

 Rais Jakaya Kikwete, akisalimiana na Shibuda, mmoja wa Wabunge wa CHADEMA wakati alipowasili kwenye Ukumbi wa St Gasper jana usiku kwa ajili ya kukutana na wabuge wa CCM kupatana nao chakula cha usiku na kufanya nao mazungumzo.
*************************************
Na Mwandishi Maalum, Dodoma,
MWENYEKITI wa CCM Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete jana Jumamosi jioni amewasili mjini Dodoma tayari kwa vikao muhimu vya chama hicho tawala vitavyofanyika kwa siku nne katika ukumbi wa Makao Makuu ya CCM maarufu kama White House.

Katika Uwanja wa ndege wa Dodoma Dkt Kikwete amepokewa na viongozi pamoja na wana CCM  wakiongozwa na Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilal na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM.
Baada ya mapumziko mafupi katika Ikulu ndogo ya Dodoma Dkt Kikwete alielekea ukumbi wa St. Gaspers ambako aliongea na wabunge wa CCM na kupata nao chakula cha usiku.

Katika hotuba yake, Dkt Kikwete aliwapa changamoto wabunge wa CCM waende kwa wapiga kura wao na kuwaelemisha kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya uliopitishwa Jumamosi Bungeni Dodoma.

Dkt Kikwete aliwasisistizia wabunge hao umuhimu wa kupeleka elimu hiyo ya mchakato wa kupata katiba mpya baadaya ya hivi karibuni kuibuka kwa  upotoshaji mkubwa wa nini kinachoendelea, na kusema kuwa wakiwa wabunge wa chama tawala ni wajibu wao kuelimisha umma kwamba kanuni na sheria zote zimefuatwa katika kupitisha muswada huo ambao umesomwa kwa mara ya pili, baada ya kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa sheria.

Rais Kikwete aliwakumbusha wabunge hao kwamba mchakato huo si jambo geni na kwamba ndio uliofuatwa na Marais wote toka wa awamu ya Kwanza hadi ya tatu, akisisitiza kwamba ni muhimu wanancho wote wakaelewa hilo, ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya watu wachache wanaotaka kupotosha umma kwamba hatua hiyo ni batili wakati sio kweli, ikizingatiwa kwamba kila lililo katika katiba ya sasa limezingatiwa.

Pia aliwasihi Watanzania kujitokeza kutoa maoni yao ya ni katiba gani wanayoitaka pindi muda wa kufanya hivyo utapowadia, na wasikubali kughiribiwa na wachache waliopania kupindisha ukweli.

Kwa mujibu wa ratiba leo Jumapili kutakuwa na Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ukumbi wa White House kitachofanyika kutwa nzima, kitachofuatiwa na kikao cha Kamati kuu ya CCM Jumatatu na Jumanne. Halmashauri kuu ya CCM itakutana kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.
 Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiwasili na kupokelewa Uwanja wa Ndege wa mjini Dodoma jana jioni.
 Wabunge wa CCM, wakishangilia na kuimba wakati wakimpokea Mwenyekiti wao Rais Kikwete katika Ukumbi wa St, Gasper mjini Dodoma jana jioni.
 Wabunge wa CCM wakimpokea Mwenyekiti wao ukumbini.
 Mapokezi kwa shangwe na nderemo...
 Mapokezi yanaendelea....
 Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa, akisalimiana na wabunge wenzake alipowasili ukumbini humo.
 Wabunge wa CCM wakiwa ukumbini humo wakimsikiliza Mwenyekiti wao Rais Jakaya kikwete kwa makini.
Baada ya mazungumzo na kupata chakula cha usiku pamoja na wabunge hao Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete, aliagana na wabunge hao.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.