Habari za Punde

*CCM MWANZA YAZIDI KUIBOMOA CHADEMA, YATEKA WANACHAMA WAKE 30

 Viongozi wapatao 30 wa Chadema ngazi ya wilaya katika wilaya ya Magu na Kwimba mkoani Mwanza, wakila kiapo cha utii, baada ya kurudisha kadi zao na kuhamia CCM leo wakati wa mkutano maalumu wa kuwapokea uliofanyika kwenye jengo la Nyanza jijini Mwanza.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mwanza, kimeendelea kukitesa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya viongozi wapatao 30 wa ngazi ya Wilaya katika Wilaya ya Magu na Kwimba kurudisha kadi zao kisha kujiunga na CCM.

Viongozi na wanachama hao wa Chadema, wamejiunga na CCM  jana baada ya kurudisha kadi zao na kukabidhiwa za CCM pamoja na fulana za chama hicho tawala, katika mkutano maalumu wa kuwapokea, uliofanyika katika ukumbi wa jengo la Nyanza jijini Mwanza.

Hafla hiyo ya kuwapokea wanachama hao iliongozwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sengerema, Mathew Lubongeja, ulikuwa na ajenda moja tu ya kupokea wanachama hao wapya.

Miongoni mwa viongozi waliokuwa wa Chadema, ambao wamerudisha kadi na kutangaza rasmi kujiunga na CCM ni pamoja na aliyekuwa Katibu wa Chadema wilaya ya Magu, Stansilaus Manyanza pamojaDominic Manembe ambaye alidai ni kiongozi wa Chadema wilaya ya Kwimba.

Hili ni tukio la pili kwa viongozi wa Chadema kuhamia CCM, baada ya Januari 3 mwaka huu viongozi wa ngazi zote za wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kutangaza kwenye mkutano wa hadhara kukihama chama hicho na kujiunga na chama tawala, mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Wakizungumza wakati wa mkutano huo maalumu wa kupokelewa ndani ya CCM, wanachama hao walikibeza waziwazi chama cha Chadema na sera zake, kwa kusema chama hicho kinaendeshwa Kifamilia zaidi, huku wakimtaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Peter Slaa kuwa ni 'mzinzi', na ndiyo maana alishindwa kwenye uchaguzi mkuu 2010 ngazi ya Urais.

Aidha walisema kuwa  wameamua kuondoka ndani ya Chadema na kujiunga na CCM baada ya kubaini pumba na mchele, na kwamba, sera, taratibu na kanuni za chama tawala ni nzuri na za uwazi zaidi kuliko zile za upinzani na kuahidi kushirikiana vyema na viongozi wa ngazi zote ndani ya CCM kwa ajili ya kujenga nchi.

Hata hivyo, aliyekuwa Katibu wa Chadema wilaya ya Magu, Manyanza alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi sababu hasa za kuondoka Chadema na kujinga na CCM alisema kwa kifupi kwamba: "Aisee, haya ni maisha tu...lakini Chadema Mwanza imeharibiwa na Katibu Wilson Mushumbusi".
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Ngeleja aliwapongeza wanachama hao wapya, na kusema kwamba moto uliowashwa Sengerema kwa viongozi wa Chadema kuhamia CCM utasambaa wilaya zote za mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla, na hiyo inatokana na sera za CCM kuwa nzuri na madhubuti.
 "Nawapongezeni sana wanachama wetu wapya tufanye kazi ndani ya CCM.  nasema moto niliouwasha Sengerema utasambaa wilaya zote za mkoa wa Mwanza na utawaka hadi taifa zima, maana CCM haina mpinzani kwa sera nzuri na mwelekeo thabiti wa maendeleo ya wananchi", alitamba Waziri Ngeleja.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.