Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon Tullo Chambo kulia, akishiriki mbio za Tabora Marathon zilizofanyika hivi karibuni, Tullo ambaye pia ni mhariri wa habari za michezo wa Gazeti la Tanzania Daima, amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Riadha Tanzania (RT).
*****************************************
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatoa pongezi kwa Mhariri wa Habari za Michezo wa gazeti la Tanzania Daima, Tullo Chambo kwa kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Riadha Tanzania (RT).
Chambo alitwaa nafasi hiyo kwenye Uchaguzi Mkuu wa RT uliofanyika Jumapili mjini Morogoro, ambapo ni miongoni mwa wajumbe wapya walioingia kwenye chama hicho.
Wengine walioshinda ni Anthony Mtaka ambaye anakuwa Rais mpya wa RT, wakati Makamu wa Rais Utawala ni William Kallaghe, Makamu wa Rais Ufundi, Dk. Ahmed Ndee, Katibu Mkuu, Suleiman Nyambui, Katibu Msaidizi, Ombeni Zavalla, Mhazini, Is-Haq Suleiman.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Mwinga Mwanjala, Meta Petro, Peter Mwita, Rehema Killo, Lwiza John, Zakaria Barrie, Zakaria Gwanda, Robert Kalyahe na Christian Matembo.
TASWA inatambua Chambo ni mwanahabari mzoefu, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mhariri wa habari za michezo na ni mtu mwenye kujua mambo mengi yanayohusu riadha, hivyo atakuwa kiungo muhimu kwa watu wa riadha, pia atakuwa kiongo kizuri kwa waandishi wa habari za michezo kuhusiana na mambo ya riadha.
TASWA inaahidi kumpa ushirikiano wa kutosha kadri itakavyoweza na inamtakia kila la heri, huku ikiamini hatawaangusha Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa RT waliomuamini wakamchagua kushika wadhifa huo.
Pia Taswa inawapongeza viongozi wote wa RT walioingia madarakani Jumapili, ikiamini watakuwa chachu ya mafanikio ya riadha hapa nchini.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
25/05/2012
No comments:
Post a Comment