Habari za Punde

*YANGA KUANZA KUTETEA UBINGWA WAO KOMBE LA KAGAME NA ATLETICO

Mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) Dar Young African, wataanza kutetea ubingwa wao Julai 14 mwaka huu dhidi ya Atletico ya Burundi mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye,  ametangaza ratiba ya michuano hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Musonye, alisema kuwa jumla ya timu 11 zimethibitisha kushiriki katika michuano hiyo itakayoanza Julai 14 hadi 28 mwaka huu, ambapo kwa siku zitachezwa mechi mbili (saa 8 mchana na saa 10 jioni) huku Tanzania Bara ikiwakilishwa na Yanga, Simba na Azam. 

Mechi ya kwanza siku ya ufunguzi kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan itaanza saa 8 mchana, wakati Mabingwa watetezi wa Kombe hilo, Yanga ya Dar es Salaam, watashuka dimbani saa 10, jioni kuvaana na Atletico ya Burundi.

Aidha Musonye aliyataja makundi kuwa ni Kundi A lina timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Ports ya Djibouti. 

Wakati timu za Azam, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya zipo katika kundi B.

Yanga inaunda kundi C lenye timu za APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi. 

Aidha Musonye, alisema kuwa katika michuano hiyo, jumla ya timu nane zitaingia hatua ya robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. 

Na kundi A na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati B litatoa timu mbili.El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu ambayo yanafanyika Tanzania Bara kwa mwaka wa tatu mfululizo kutokana na sababu mbalimbali.

Coffee haitashiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14 mwaka huu wakati El Merreikh wikiend ya Julai 13-15 mwaka huu itakuwa na mechi ya michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Musonye, alitaja zawadi ya Bingwa wa michuano hiyo ya mwaka huu kuwa atajinyakulia kitita cha dola za Marekani 30,000/= na msindi wa pili ataibuka na dola 20,000/= na mshindi wa tatu dola 10,000. 

Michuano hiyo itakuwa ikionyeshwa moja kwa moja (live) na Televisheni ya SuperSport.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.