***************************************
Na Mwandishi Wetu
KIJANA Julius Dawson ambaye kwa jina la kisanii anajulikana kama 'Elinaja' (23), mkazi wa Tabata Segerea, ambaye mwaka jana alikuwa gumzo baada ya kuandika mashahiri ya muziki wa Bongo Flava "mistari ya Bongofleva" katika karatasi yake ya kujibia mtihani wa kidato cha nne, amefunguka na kuweka wazi kile kilichomfanya kufanya tukio hilo la kihistoria katika tukio hilo lililoonekana kituko cha mwaka.
Dawson, ambaye asili yake ni mzaliwa wa Moshi Marangu, ambaye kwa sasa anaishi peke yake Tabata baada ya baba yake kufariki huku mama yake akiwa anaishi Wilaya ya Kisarawe, alisema lengo la kufanya vile ilikuwa ni kufikisha ujumbe kwa jamii ili kuokoa maisha ya vijana wengi ambao hupotezwa muda kwa kulazimishwa kusoma bila kujali kile anachohitaji kujana kutokana na mfumo uliopo sasa ambao unamlazimisha kila kijana kuufuata bila ya kuwepo na mfumo mbadala.
Akizungumza kwa kujiamini wakati akiwa katika mahojiano na mtangazaji wa kipindi cha "Power Breakfast" cha Radio Clouds FM, Gerald Hando, Dawson, alisema kuwa mfumo mmoja wa maisha unawaharibia maisha vijana wengi ambao hawawezi kufiti katika mfumo huo, ambao pengine wangeweza kufanikiwa kama kungekuwa na mifumo mbadala kwa kuchagua wakipendacho kusomea.
"Waulize watu hawa wanaotamba katika muziki au umiss, utakuta wazazi wao walikuwa wanawakimbiza sana "huyu hataki shule", lakini akishafanikiwa utamsikia mzazi huyo huyo akisema "Mungu kamjaalia mwanangu kafanikiwa katika muziki". Sasa kama mzazi angemsapoti kwa kutambua kipaji chake tangu mapema si angefanikiwa zaidi kuliko kumpotezea muda wake?" Alisema na kuhoji Dawson.
"Tatizo la nchi yetu ni kwamba kuna 'system' moja iliyowekwa, kwamba usipoifuata huna 'option' nyingine. Wakati naandika vile nilikuwa na lengo la kutuma na kufikkisha ujumbe kwa wahusika wanaosimamia elimu kwamba kuna umuhimu wa kuwekwa 'system' tofauti za maisha kwa sababu mtu anaweza akawa si mzuri katika 'system' yao lakini akawa mzuri katika 'system' nyingine. Hivyo ziwepo ili wazazi waokoe pesa na muda wa kulazimisha kumpeleka mtu katika kitu asichokipenda na ambacho anakimudu.
"Ujumbe wangu ni kwamba wazazi na jamii itambue vipaji vya vijana wao. Inapotokea mtoto tangu akiwa mdogo na akaonekana kuwa na kipaji cha kuimba ama kuigiza ama fani yeyote basi ni vyema akasomea kitu ambacho kipo ndani yake ya damu yake kuliko kupoteza muda na pesa bure.
Mimi ni mmoja kati ya watu walioathirika na maisha magumu nikiwa mitaani kwa sababu tu tumeshindwa kwenda na 'system' niliyokuwa nikiihitaji. Unakuta vijana wana vipaji vingine ambavyo vingeweza kuwafanya wakaishi maisha bora kabisa, lakini mzazi analazimisha kufuata anachokihitaji yeye.
"Nilipoandika jambo sikuamini kama lingekuwa kama lilivyokuwa na kuteka hisia za kila mtu ila nilikuwa na maana yangu kubwa ya kufikisha ujumbe. Lakini lilivyopokewa ilikuwa tofauti. Watu walikuwa wakiangalia upande mmoja tu. Na ilikuwa inaniumiza sana. Kuna wakati nilikuwa nikipanda katika daladala, na kukuta watu wakiongelea jambo lile bila kujua mlengwa wanayemzungumzia wapo naye katika gari hilo, huku wengine wakiponda sana. Bila wao kujua na mimi nilikuwa nikijumuika nao katika kuchangia mawazo huku mimi nikishikilia na kusimamia msimamo wangu kwa kuwaeleza kama ambavyo nimeeleza hapa leo, nilikuwa nawaeleza kama haya ninayosasema hapa."
Alipoulizwa na Gerald Hando, kuwa anajisikiaje kupata fursa ya kutoa ufafanuzi wa jambo hilo hewani, Dawson alisema: "Katika siku ninayojisikia furaha maishani mwangu, ni leo. Najiona kama mtu ambaye nimeutua mzigo mzito uliokuwa ukimuelemea. Baada ya hapa hata nikiambiwa kufa, ni sawa tu kwa sababu nimeshautua mzigo."
Dawson pia alitumia fursa hiyo kuomba radhi kwa Jamii kama kuna aliyekwazika ama kumkatisha tamaa yeyote kutokana na kitendo chake kile hicho.
"Maoni yangu ni kwamba jamii iwasapoti watu kufanya kitu wanachokiweza. Mwisho kama kuna mtu ama mzazi nilimkwaza ama nilimkatisha tamaa, namuomba radhi. Mimi si 'bad boy', mimi ni kijana mwema kabisa. kwani hata ningejaza majibu ambayo nahisi nisingeyapatia kwa usahihi bado kwangu yasingekuwa na faida" alisema
Akielezea historia yake na kilichosababisha kuchelewa kumaliza kidato cha nne akiwa na umri mkubwa, Dawson alisema masomo yalikuwa yakimuwia magumu na hivyo kumfanya arudie kidato cha pili kila alipofeli kwa miaka miwili mfululizo na hatimaye kukaa benchi kwa miaka minne.
"Nilianza shule ya msingi Umoja Mabibo mwaka 1996, lakini maisha yalikuwa magumu hapa mjini hivyo tukiwa na wazazi tukahamia Kisarawe.
"Mwaka 2002 nikachaguliwa kujiunga na Sekondari Manerumango. Wakati nikiwa kidato cha pili nikafeli mara mbili. Mara ya kwanza nilirudia, lakini mara ya pili nikaacha shule.
"Baadaye mama yangu mdogo akanichukua nikaja huku Dar kusoma. Nikarudia tena shule baada ya kukaa nje ya masomo kwa miaka minne.
"Shule nilikuwa naipenda, lakini yenyewe haikuwa ikinipenda kwani aina ya elimu niliyokuwa naipata naona ilikuwa ngumu kwangu. Nilikuwa nachukua masomo ya biashara. Nadhani ugumu niliuona kutokana na jinsi nilivyoumbwa tu. Nilikuwa nasukumwa pia na mama yangu mkubwa. Maksi zangu zilikuwa za chini sana. Mwisho ndio nikamaliza kidato cha nne mwaka jana nikiwa na umri mkubwa kama hivi."
Alisema baada ya kufikisha ujumbe, sasa anajisikia huru licha ya kwamba hana kazi ya kufanya ya kumuingizia kipato, zaidi ya kujishughulisha na usanii wa kutunga na kuimba muziki wa Bongo Flava.
"Nimefanikiwa kurekodi wimbo wangu mmoja unaitwa "Mr President" ambao unaongelea upande wa rais anayetolea majibu maswali ya wananchi na huku pia akielezea ugumu wa kazi yake.
"Nimeurekodi katika studio ya prodyuza mzungu Fundi Samweli wa Kibaha na kisanii natumia jina la "Elinaja". Katika sehemu ya mistari yake, Dawson anaimba: "Mnasema Mr President kila mahala kajaza rafiki zake, ni nani kati yetu anashirikiana na maadui zake."
Na kiitikio kinasema: "Wanagomba wanasumbua kila tatizo nasemwa mimi, mara "Mjomba" mara "Mshua" oooh Mr President." Jina la Mjomba lilitumika katika nyimbo za Mrisho Mpoto wakati neno "Mshua" lilitajwa katika wimbo 'Rizi-One' wa rapa Izzo Bizness.
Dawson a.k.a Elinaja, alisema amerekodi wimbo huo kwa fedha za kuunga-unga kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki."Nina nyimbo za kutosha albam nzima. Tatizo ni pesa. Naomba jamii inisaidie kufanikisha ndoto yangu," alisema kijana huyo ambaye aliwafanya waandishi wa habari waangue vicheko mwaka jana wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Joyce Ndalichako, alipoisoma "mistari" yake ya Bongofleva, wakati akitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.
Baada ya mahojiano ya Dawson na Hando, watu mbalimbali walituma ujumbe radioni Clouds FM kuonyesha sapoti yao kwa kijana huyo akiwamo Salum Mwalimu wa Vodacom na Jackson Mbado wa Airtel, huku Salum Mwalimu akimuita kuwa ni shujaa wake.
No comments:
Post a Comment