MCHEZAJI wa Azam Fc, aliyetangazwa kuuzwa kwa dau la dola za Kimarekani 50,000 ama za Madafu Sh. milion 80, Mrisho Ngassa huenda akatua Klabu ya Simba kwa dau la Sh. milioni 25, imeelezwa.
Habari zilizoufikia mtandao huu, zinasema kuwa tayari Simba wameonyesha kupanda dau kwa mchezaji huyo na kupiku dau lililotangazwa na watani wao la Sh. milioni 20,ambapo imeelezwa kuwa tayari Klabu hiyo imekwishalipa fedha hizo kwa Klabu ya Azam leo mchana.
Aidha imeelezwa kuwa tayari Klabu hiyo ya Azam imekwishasainiana fomu za uhamisho na Klabu ya Simba tayari kwa uhamisho wa mchezaji huyo.
Wakati Ngasa, akiuzwa kwa wekundu hao, kufuatia kitendo chake cha kubusu jezi ya Yanga, Kocha wake Muingereza, Stewart Hall, naye ametupiwa vilago na timu hiyo kwa kile kilichoelezwa kukaidi agizo la kutompanga Ngasa katika mchezo wa fainali za Kombe la Kagame zilizomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mtonyaji wa habari hizi ameeleza kuwa Kocha huyo alipewa maagizo kutoka kwa Uongozi wa juu wa Klabu hiyo kutompanga Ngasa katika mchezo wa fainali baina ya timu hiyo na Yanga, kitendo ambacho alikipuuza na kumpanga jambo ambalo limeonekana zilisema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa anafundisha timu ya vijana.
Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mbali na Ngassa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ pia yuko katika wakati mgumu na jana inadaiwa alionekana akilia wakati anazungumza na kiongozi mmoja wa Azam, akiuliza ni lipi kosa lake.
Sure Boy, ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya vijana ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ jana hajafanya mazoezi na leo pia, naye pia akituhumiwa kucheza kinazi katika mechi dhidi ya Yanga.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine. Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
No comments:
Post a Comment