Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodgar Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Ismail Aden Rage.
Rage ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Simba alimuandikia Rais Tenga barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema ‘kamati hiyo kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mpira Tanzania zinavyoeleza.’

“Kutokana na uzoefu na uwezo ambao Rage anao katika uongozi wa mpira wa miguu, ni vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu za maendeleo ya mpira wa miguu,” amesema Rais Tenga.
Pia Rais Tenga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mpira wa miguu kuongozwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai ambayo imetoa kwa kamati zote za TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala kupendelea upande wowote.
Rais Tenga amesisitiza kuwa kamati hazina budi kuchukua hatua zinazostahili bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa. Amezitaka kamati zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa vile kwa kufanya hivyo, uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua, hivyo mpira wa miguu kuongozwa kwa sheria na haki.
No comments:
Post a Comment