Habari za Punde

*KOZI YA WAKUFUNZI WA WAAMUZI YA FIFA KUANZA KESHO

Kozi ya wakufunzi wa waamuzi (Futuro III Refereeing Course) ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inaanza kesho (Septemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
 
Jumla ya washiriki katika kozi hiyo itakayoanza saa 3 asubuhi kwenye hoteli ya Holiday Inn ambao wanatoka katika nchi 21 za Afrika ni 69.
 
 Kozi hiyo inayotarajiwa kumalizika Septemba 22 mwaka huu inafanyika katika maeneo mawili ya ufundi (technical) na utimamu wa mwili (fitness).
 
Nchi washiriki ni Afrika Kusini, Botswana, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Mauritius, Namibia, Nigeria, Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Swaziland, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
 
Washiriki kutoka Tanzania kwenye kozi hiyo ni Joan Minja, Leslie Liunda na Soud Abdi (technical) na Riziki Majalla (fitness).
 
Baadhi ya wakufunzi wa kozi hiyo wanaotoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Carlos Henriques anatoka Afrika Kusini, Fernando Gracia (Hispania), Steve Bennett (Uingereza), Tarek Bouchamaoui (Tunisia), James Sekajugo (Uganda), Bester Kalombo (Malawi), Felix Tangawarima (Zimbabwe) na An-Yan Lim Kee Chong (Mauritius).
 
Kozi hiyo itafunguliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na mjumbe wa Kamati ya Vyama (Associations Committee) ya FIFA.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.