Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea vizuri na kambi ya mazoezi mkoani Mbeya ambapo tayari imecheza mechi moja ya kujipima nguvu.
Ilicheza mechi hiyo jana (Septemba 8 mwaka huu) dhidi ya Tanzania Prisons iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom kwenye mji wa Nakonde ulioko mpakani mwa Tanzania na Zambia. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku bao la Serengeti Boys likifungwa na Miraji Selemani.
Serengeti Boys leo jioni (Septemba 9 mwaka huu) inatarajia kucheza mechi nyingine wilayani Mbozi dhidi ya Mbozi United. Itacheza mechi ya tatu Jumanne (Septemba 11 mwaka huu) jijini Mbeya dhidi ya timu ya daraja la kwanza ya Mbeya City.
Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Jakob Michelsen kambi hiyo inaendelea vizuri, na anatarajia kupata mechi moja ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kucheza mechi ya mashindano na Misri, Oktoba 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment