Baadhi ya Warembo wakipozi kwa picha ya pamoja wakati wa Shoo ya kumtafuta Miss Talent.
Na Mwandishi wetu
MREMBO kutoka Kagera anayewakilisha Kanda ya Ziwa katika shindano la Redd’s Miss Tanzania, Babylove Kalala juzi usiku alifanikiwa kutwaa taji la Redd’s Miss Talet lililofanyika kwenye hoteli ya Giraffe, iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam.
Kutokana na ushindi huo, Babylove sasa anaunga na Miss Photogenic, Lucy Stephano na Redd's Miss Tanzania Sports Lady, Mary Chizi kuingia hatua ya 15 ya Redd’s Miss Tanzania litakalofanyika mwishoni mwa wiki.
Babylove alifanikiwa kuwashinda warembo wengine 30 aliokuwa anachuana nao, baada ya kuonesha kipaji cha hali ya juu wakati akicheza ngoma kwa kutumia nyoka, kiumbe ambaye warembo wengine walionekana kumuogopa mno.
Warembo wengine waliofanikiwa kuingia hatua ya tano bora walikuwa ni Joyce Baluhi na Irene Verda wa Kanda ya Mashariki, Catherine Masumbigana (Temeke) na Brigit Alfred (Kinondoni).
Mgeni rasmi katika shindano hilo alikuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Magige ambaye aliwataka warembo wanaoshiriki kutumia mashindano hayo kama chachu ya kufikia malengo waliyojiwekea.
Akizungumza mara baada ya kutwaa taji hilo, Babylove aliwashukuru washiriki wengine kwa kuwa chachu ya yeye kuhakikisha anakuwa mbunifu zaidi, huku akiahidi kufanya makubwa katika shindano la Redd’s Miss Tanzania.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
No comments:
Post a Comment