Habari za Punde

*PELE AWATAKA SERENGETI BOYS KUJITUMA ILI KUFUZU KUCHEZA FAINALI ZA AFRIKA MWAKANI

Nyota wa zamani wa Ghana, na klabu ya Olympique Marseille, Abedi Pele, amewaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kuwa "hakuna njia ya mkato katika kutafuta mafanikio" na kuwataka kufanya jitihada ili watimize ndoto zao, ikiwa ni pamoja na Serengeti Boys kuhakikisha inafuzu kucheza fainali za Afrika mwakani.
 
Pele, ambaye aliiongoza Marseille, kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao dhidi ya AC Millan ya Italia, alisema hayo Jana asubuhi wakati alipotembelea Kiti cha ufundi cha Karume kushuhudia programu ya mazoezi ya vijana wadogo inayofanyika kila mwisho wa wiki kwenye Uwanja wa Karume ambako watoto kuanzia umri wa miaka sita hadi 17 hufundishwa mbinu za kusakata soka.
 
"Katika kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye ameletwa nchini na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) kuangalia shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
 
"Tunaona wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze kucheza kwa kiwango cha juu. 
 
Bila ya kufanya juhudi binafsi, kujituma na kudhamiria huwezi kufanikiwa.
 
"Wale wenye vipaji vikubwa, lakini hawafanyi jitihada watabakia, wale wasiojaliwa kuwa na vipaji, lakini wanafanya jitihada, watakwenda mbele na kupata mafanikio," alisema nyota huyo wa Ghana ambaye alijijengea jina kwa kufunga mabao safi na muhimu kwa nchi yake na klabu ya Olympique Marseille wakati ikitamba katika soka barani Ulaya.
 
"Soka barani Afrika Linamazingira yanayofanana, hakuna mtoto wa waziri anayecheza soka, wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi wa benki ambaye anacheza soka. 
 
Soka inachezwa na watu wanaotoka kwenye familia ambazo hazina maisha mazuri na hivyo nafasi sawa na wengine wote. 
 
Mnachotakiwa kufanya ni kujituma, kudhamiria na kufanya jitihada ili mfungue mlango wa mafanikio.
 
Pele, ambaye jina lake halisi ni Abedi Ayew na ambaye watoto wake wainaichezea Marseille, pia aliwataka wacheaji wa timu ya Taifa ya Vijana walio na umri china ya miaka 17 kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Algeria mapema mwakani.
 
"Mkifuzu mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu," alisema gwiji huyo ambaye anaiwakilisha FIFA katika kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo''. 
 
"nikiwaangalia naona mna uwezo wa kuwaondoa wapinzani wenu na nitafuatilia mechi yenu. Mkifuzu tutakuwa wote na nitawaunga mkono.
 
Pele, ambaye kwa sasa anamiliki shule ya mpira wa miguu ambayo imefanikiwa kutwaa Kombe la FA mara moja, ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo wa FIFA kwa nchini za Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na mmoja wa viongozi wa Idara ya Mawasiano ya FIFA, Emmanuel, atakuwa nchini kwa siku tatu ambazo atazitumia kupata taarifa za shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo za soka la watoto (grassroots), soka la vijana, soka la wanawake na miradi mingine ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.