Habari za Punde

*TUMEYA KATIBA YATOA UFAFANUZI


Na Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari yakiwemo baadhi ya magazeti ya jana (Alhamisi, Januari 17, 2013) ambazo zinaashiriakuwa Tume inakataa kupokea baadhi ya maoni yanayowasilishwa kwake na makundi mbalimbali.

Taarifa hizo za vyombo vya habari zimetokana na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Dkt. Ramadhan Mlinga aliyoitoa mara baada ya taasisi yake kuwasilisha kwa Tume maoni kuhusu Katiba Mpya siku ya Jumatano, tarehe 16 Januari, 2013 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mara baada ya PPRA kuwasilisha maoni kwa Tume, Wajumbe wa Tume walisita kupokea maoni ya taasisi hiyo na badala yake kuagiza PPRA kuandaa maoni tena na kuyawasilisha katika Tume ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe 16 Januari, 2013.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Alhamisi, Januari 17, 2013) kwa vyombo vya habari na Katibu wa Tume hiyo Ndg. Assaa Rashid, taarifa hizo siyo za kweli na kuwa Tume yake haina mamlaka ya kisheria ya kukataa kupokea maoni.

“Tume inapenda kuwataarifu wananchi, makundi, taasisi na wadau wengine wote kuwa Tume haijakataa na haina mamlaka ya kisheria ya kukataa kupokea maoni ya mtu, jumuiya, taasisi au kundi lolote,” alisema Ndg. Assaa katika taarifa yake na kuongeza:

“Katika mikutano inayoendelea (na makundi mbalimbali), kabla ya kuhitimisha mkutano husika, Tumehuomba chama cha siasa, jumuiya, taasisi au mtu aliyewasilisha maoni kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizojitokeza katika kikao” alisema na kufafanua kuwa ufafanuzi huu hutolewa kwa hiari palepale katika mkutano au kwa maandishi baada ya siku kadhaa ambazo Tume hukubaliana na mtu au kikundi kilichowasilisha maoni.

Akifafanua zaidi Ndg. Assaa ameseama kuwa mikutano inayoendelea kati ya Tume na Makundimbalimbali inafuatia kukamilika kwa mikutano ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi tarehe 19 Disemba mwaka jana (2012).

“Kwa msingi huu, katika mkutano kati ya Tume na PPRA uliofanyika juzi, tarehe 15 Januari, 2013, Tume iliiomba PPRA kuangalia uwezekano wa kutoa ufafanuzi wa masuala ya ziada ambayo Tume ilitaka kupata maoni ya kitaalamu kutoka katika taasisi hiyo,” alisema kiongozi huyo wa Tume na kuongeza kuwa ombi kama hilo pia limetolewa kwa makundi mengine ambayo yameshakutana na Tume kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi tarehe 1 Mei mwaka jana (2012) na wiki iliyopita ilianza kazi ya kukusanya maoni ya makundi na watu mbalimbali kuhusu Katiba Mpya. Mikutano hii inatarajiwa kukamilika tarehe 25 mwezi huu (Januari, 2013).

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.