Habari za Punde

*UPATIKANAJI WA HARAKA WA HUDUMA ZA AFYA UTAPUNGUZA VIFO VYA KINAMAMA WAJAWAZITO NA WATOTO


Mama Salma Kikwete.
Na Anna Nkinda – aliyekuwa Paris
Kuwepo kwa upatikanaji wa haraka wa huduma za afya na wataalamu wa kutosha wa kutoa huduma hiyo  kutasaidia kwa kiasi kikubwa kina mama wajawazito kujifungua salama na hivyo kupunguza vifo vyao na  watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati alipozitembelea ofizi za shirika la AMREF Ufaransa zilizopo mjini Paris ili kuona jinsi linavyofanya kazi mbalimbali ikiwa ni  kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto zinapungua barani Afrika.
Mama Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa ujenzi  zaidi wa vituo vya Afya, Zahanati,  Hospitali, upatikanaji wa vifaa tiba na kuwepo kwa wingi wa wataalamu wa masuala ya  afya kutasaidia kina mama wajawazito kupata huduma nzuri na hivyo kujifungua salama.
“Kina mama wengi wajawazito  wanakufa kutokana na kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Maralia na upungufu wa damu hivyo basi jitihada za pamoja baina ya Serikali na wadau wa afya zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa kina mama hawa wanajifungua salama na kutokufa na  magonjwa haya”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliishukuru Taasisi ya AMREF International kwa kuanzisha kampeni Barani Afrika kwa ajili ya  kuchangisha fedha za kuwasomesha manesi wengi ili kina mama wajawazito waweze kupata huduma ya kutosha wakati wa kujifungua na hivyo  kujifungua salama.
Akisoma taarifa ya AMREF International Mkurugenzi wa Shirika hilo nchini Ufaransa Muriel Gavila alisema kuwa  mpango mkakati waliokuwa nao nchini Tanzania katika kampeni ya kuwasaidia wanawake Barani Afrika kwa mwaka 2012 – 2015 ni kuchangisha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa manesi wakunga 3800 ili kina mama wajawazito waweze kupata bora zaidi.
Gavila alisema kuwa shirika hilo limekuwa likifanya kazi mbalimbali za kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua, kutoa elimu kwa wahudumu wa afya na  kutoa elimu ya uzazi kwa jamii.
AMREF Ufaransa imeahidi kufanya kazi kwa pamoja  na Taasisi ya WAMA katika upande wa afya ya mama na mtoto  ili kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano vinapungua nchini Tanzania.
Mama Kikwete alikuwa nchini Ufaransa  na  Mumewe Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa ajili ya mwaliko wa  ziara ya kiserikali ya siku tatu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.