Na Mwandishi Wetu
MWANAMICHEZO aliyewahi kuifadhili Simba na pia kumiliki timu ya Ligi
Kuu ya soka nchini, Azim Dewji ameingilia katika suala la mgogoro wa
Katiba ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), akisema ni bora Tanzania
ikafungiwa na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kuliko
kuyumbishwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Dewji aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, huku akimtaka Tenga
kuwa na msimamo katika maamuzi yake.
Alisema kuwa, Tenga akiwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la
Taifa (BMT) alikuwa tayari kuona Tanzania inafungiwa na FIFA, kuliko
kuacha soka la nchi hii liendeshwe kiholela.
“Sasa kama wakati ule alitaka tufungiwe, kwa sasa anaogopa nini na kuanza kubishana na Serikali?
“Kwa maoni yangu, ni bora tufungiwe lakini tusiendeshwe na
FIFA…Tanzania ina Serikali na ndiyo inayosimamia michezo, kwa hili
sioni sababu ya TFF kuitunishia msuli serikali.
Hii ni nchi, haiwezi kutishwa na taasisi tu ya soka ya kimataifa ambaye Tenga mwenyewe aliwahi kukaririwa miaka ya nyuma akisema ina genge la wahuni…,” alisema Dewji.
TFF imejikuta ikiingia katika mgogoro na Serikali baada ya Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuingilia
kati suala la mgogoro wa uchaguzi ndani ya TFF kwa kuagiza kufutwa kwa
matumizi ya Katiba ya shirikisho hilo ya mwaka 2012, kwa kuwa imekiuka
Kanuni na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Waziri huyo aliiagiza TFF kufuata utaratibu wa kurekebisha Katiba za
vyama vya michezo, kwa mujibu wa Sheria ya BMT iliyotungwa na Bunge
pamoja na Kanuni zake ambazo ziko wazi na rahisi kuzifuata.
Hata hivyo uamuzi huo wa Waziri, ulipingwa na Tenga pamoja na Kamati
ya Utendaji ya shirikisho hilo, ambapo Tenga ameomba kuonana na Waziri
akidai amepotoshwa na wasaidizi wake na uamuzi wake unaweza kulitia
soka la Tanzania katika matatizo.
Tenga alidai Serikali na BMT vimeachana na kuingilia masuala ya soka
tangu mwaka 2004 na ndani ya Katiba hiyo kuna utaratibu mzima ambao
unaonesha namna ambavyo TFF inapaswa kufanya uamuzi wake kama chombo
huru.
Hata hivyo, kisheria Katiba ya TFF lazima isajiliwe serikalini.
Awali TFF iliomba kukutana na Waziri na ikafanya hivyo, lakini
shirikisho hilo limeomba tena kukutana na Waziri Mukangara kwa madai
kuwa katika kikao cha awali Tenga hakuwepo badala yake walienda
watendaji, hivyo ni vyema kikafanyika kikao hicho ili kumpa ufafanuzi
wa baadhi ya mambo kwa nia ya kulimaliza jambo hilo.
Katika kikao hicho cha awali, Serikali iliitaka TFF kuitisha mkutano
wa katiba ndani ya siku 40 na baada ya hapo kuitisha uchaguzi ndani ya
siku kama hizo na pia imeitaka kutoa taraifa kwa wanachama wake kuhusu
mkutano huo ndani ya siku tano tangu siku walipokutana.
Uamuzi wa Dk Mukangara ulikuja siku chache kabla ya timu ya maofisa
wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuja nchini kufuatilia
mgogoro ulioikumba TFF na wadau wake kutokana na masuala mbalimbali ya
uchaguzi huo uliokuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu.
Ujumbe wa FIFA haukuja badala yake shirikisho hilo limetuma barua ya kutishia kuifungia Tanzania kama itathibitika serikali inaingilia masuala ya
soka.
No comments:
Post a Comment