Habari za Punde

*MIYEYUSHO APOZA MACHINGU YA MPHILIPINO KWA KUENDELEZA UBABE KWA UKOO WA MATUMLA

Na Mwandishi Wetu, Dar
BAADA ya kupoteza mechi yake ya kimataifa ya kirafiki wiki tatu zilizopita Bondia Francis Miyeyusho, usiku wa kuamkia leo ameendeleza ubabe kwa wabongo wenzake na mabondia wa ukoo wa Matumla, kwa kumchapa Mohamed Matumla kwa pointi katika pambano lisilo la ubingwa lililokuwa la uzito wa Bantam, lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, jijini Dar es Salaam.

Mohamed Matumla, ambaye ni mtoto wa Bondia Rashid Matumla, alifanikiwa kumaliza raundi zote 10 za pambano hilo na majaji wote watatu wakampa ushindi wa pointi Francis Miyeyusho 'Chichi Mawe'.

Pamoja na ushinda, lakini Matumla aliweza kuonyesha upinzani wa hali ya juu kwa Miyeyusho ambapo pambano hilo lilikuwa ni la majibizano.

Chichi alianza vizuri pambano hilo akimkalisha chini mpinzani wake raundi ya kwanza tu, baada ya kumpa ngumi ya kidevu ya kushitukiza.

Hata hivyo, Matumla aliinuka na kumalizia vizuri raundi hiyo, kisha kuibuka upya katika raundi ya pili na kuendelea vizuri hadi mwisho.

Miyeyusho alipiga ngumi nyingi zaidi ya mtoto wa Matumla, aliyeongozwa na baba yake ulingoni lakini mabondia wote walichapana makonde ya nguvu na kila mmoja alionyesha kukubali kipondo cha mwenzake.

Pambano hilo lilitawaliwa na vurugu za mashabiki wa mabondia hao kutokana na upinzani wa asili- Matumla akikusanya watu wa Keko na Temeke kwa ujumla na Miyeyusho akikusanya watu wa Kinondoni na Manzese.

Miyeyusho alipanda ulingoni leo kiasi cha wiki tatu tangu apigwe vibaya na Sukkassem Kietyongyuth wa Thailand Aprili 19 kwenye ukumbi huo huo kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya kwanza sekunde ya 55.

Miaka miwili iliyopita, Miyeyusho alishawahi kumpiga baba yake mdogo Matumla, Mbwana Matumla Oktoba 30, mwaka 2011 na leo ameendeleza ubabe dhidi ya ukoo huo maarufu katika mchezo wa ngumi.

Hilo lilikuwa pambano la 51 kwa Miyeyusho tangu aanze kupigana kifua wazi Februari 1, mwaka 1998 akiwa ameshinda mapambano 38, kati ya hayo 23 kwa KO na kupigwa 11, kati ya hayo 9 kwa KO na sare mawili.  

Mtoto wa Rashid Matumla ambaye ngumi katika ukoo wao zinaanzia kwa babu yake Mzee Ally Matumla, leo amepigwa kwa mara ya kwanza katika pambano la 15 tangu ajitose kwenye ngumi za kulipwa Novemba 17, mwaka 2010 akiwa ameshinda mapambano 11, manne kwa KO na ametoka sare mara tatu

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.