Mkurugenzi wa Habari na Itifaki, Bw. Jossey Mwakasyuka
(kushoto) akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani)
kuhusiana na malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo katika
ukumbi wa mikutano ofisi ya Bunge mjini Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo
wakisikiliza kjwa makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Habari na Itifaki,
Bw. Jossey Mwakasyuka wakati alipofanya mkutano na waandishi hao kwa lengo la kutolea
ufafanuzi kuhusiana na malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo
katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Bunge mjini Dodoma. Picha
zote na Benedict Liwenga-Maelezo
*******************************
Na Benedict Liwenga,
Maelezo-Dodoma.
OFISI ya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, imetoa
ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa
kwa malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Ufafanuzi huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Habari na
Itifaki Bw. Jossey Mwakasiyuka wakati alopokutana na waandishi wa habari kwa
lengo la kutolea ufafanuzi kuhusiana na taarifa hizo zilizoikera ofisi hiyo ya
Bunge Maalum.
Mwakasyuka amevieleza vyombo vya habari kuwa, ofisi ya Bunge
Maalum imekerwa na kuchapishwa kwa taarifa hizo na baadhi ya vyombo vya habari
kwani taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha Waheshimiwa
Wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho
wanazolipwa.
“Ni vema ikaeleweka kwamba Wajumbe wa Bunge Maalum wote ni
watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi
zinazowaingizia kipato na kwamba Ujumbe wa Bunge Maalum ni nafasi ya muda tu ya
kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba Mpya”. Alisema Mwakasyuka.
Mwakasyuka ameongeza kuwa, si vema kwa vyombo vya habari
kuwadhalilisha Wajumbe hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo
kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi ya Bunge Maalum vizuri
kama ilivyotarajiwa na wananchi.
Akifafanua kuhusiana na malipo ya posho hizo, Mkurugenzi
Mwakasyuka ameviambia vyombo vya habari kuwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalum ambao
wanahudhuria vikao vinavyoendelea wamekwishalipwa posho zao zote kama
wanavyostahili.
“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata
taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye mchakato maalum unaojumuisha
kupata orodha za mahudhurio ya Wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka
Hazina, na upatikanaji wa fedha toka Benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku
kadhaa hadi kukamilika.” Alifafanua Mwakasyuka.
Aidha, Mwakasyuka amevitahadharisha vyombo vya habari vinavyondika habari za Bunge Maalum
kuzingatia maadili na kanuni za Uandishi wa habari zinazotolewa katika vikao
vya Bunge Maalum ili taarifa kama hizo za upotoshaji zisijirudie tena.
“Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio
kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio
makini”. Alionya Mwakasyuka.
Katika kanuni za Bunge Maalum, kanuni ya 77
inawataka waaandishi wa habari kuandika habari za Bunge Maalum kwa weledi
mkubwa kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari ili kuondoa uandishi wenye
kuleta chuki kati ya Serikali na Wananchi wake kwani kinyume na kanuni hiyo,
Katibu anaweza wakati wowote kuondoa ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa chombo
chochote cha habari iwapo chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu shughuli
za Bunge Maalum ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha ukweli au
vinginevyo inakiuka kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum.
No comments:
Post a Comment