Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Vijana wa wilaya ya Lindi
mjini wametahadharishwa kutokubali kudanganywa na kutumiwa kufanya
vurugu ambazo zinaharibu vitu vichache walivyonavyo na kwa kufanya
hivyo wanarudisha nyuma maendeleo yao.
Tahadhari hiyo imetolewa
jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kupitia wilaya hiyo Mama Salma Kikwete wakati akiwanadi wagombea
wa chama hicho kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa
Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata ya
Makonde.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete alisema ni vyema vijana wakaelewa historia ya nchi yao na kujua
lipi jema na baya kwani kuna baadhi ya wanasiasa wanawashawishi ili
wafanye vurugu kwa madai kuwa hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana
jambo ambalo siyo kweli.
“Hao wanaowadanganya nyinyi mfanye
vurugu na kuharibu vile vichache mlivyonavyo eti kwa kuwa maisha yenu
hayajaimarika kwao hawafanyi hivyo, kwao kuna maendeleo na ninyi mnazidi
kujirudisha nyuma kimaendeleo. Msikubali mkoa wetu uwe sehemu ya
majaribio na kutumika kwa manufaa yao”.
Kama wangekuwa
wanawapenda na kutaka kuwasaidia ili muendelee wangewajengea hata shule
ambazo zingewafanya vijana na watoto wetu wasome, hapo hakuna
kipingamizi kwani Elimu ni mkombozi wa maisha na elimu inaleta
maendeleo”, alisema Mama Kikwete.
MNEC huyo alisema Serikali
makini ni lazima ijali maisha ya watu wake, kwa kutambua hilo Serikali
ya CCM imeimarisha miundo mbinu kwa kujenga barabara za lami, shule ili
watoto wasome na kuimarisha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kujenga
Hospitali na vituo vya afya na kuhakikisha wahudumu wa afya
wanaongezeka.
Alisema, “Maisha bora kwa kila mtanzania siyo Chama
kinapita nyumba kwa nyumba kugawa pesa bali ni kwa kuboresha
miundombinu, kukiwa na shule watoto watasoma, kukiwa na barabara nzuri
wananchi wasafirisha mazao yao, kukiwa na huduma bora za afya wananchi
watatibiwa haya yakifanikiwa maisha ya mtu mmoja mmoja yataimarika”.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Lindi Mjini Muksini Rafii
alisema katika uchaguzi huo ndani ya wilaya hiyo wagombea za nafasi za
wajumbe 147 na wenyeviti saba wamepita bila kupingwa.
Kwenye
mkutano huo mwanachama mmoja aliyejulikana kwa jina la Raphael Mahuna
kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye alikuwa ni
mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing kwa tiketi
ya chama hicho na mwanachama mmoja kutoka Chama cha Wananchi (CUF)
walijiunga na Chama Cha Mapinduzi.
Mahuna alisema ameamua kwa
hiari yake mwenyewe bila ya kulazimishwa kujiunga na CCM kwani alipokuwa
anagombea nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing alishindwa
kufanya kampeni kwa kuwa alikosa wajumbe wa kumuunga mkono.
Katika
uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mkoani Lindi
wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika vitongoji 600, vijiji 87 na mitaa
nane wamepita bila kupingwa.
No comments:
Post a Comment