Habari za Punde

*KIFO CHA KAPTENI JOHN KOMBA CHAISHITUA CCM, AACHA AMEREKODI WIMBO MMOJA TU WA KAMPENI 2015

Kapteni John Komba, (pichani chini) enzi za uhai wake akiwa nyumbani kwake katika moja ya harakati za kuandaa nyimbo za Kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015.

Marehemu Kapteni John Komba, alikuwa tayari ameanza kufanya mazoezi ya kurekodi albam ya  nyimbo za uchaguzi mkuu wa 2015 za Chama cha Mapinduzi CCM, ambapo alikuwa akishirikiana na baadhi ya wanamuziki wake wa zamani aliokuwa nao katika bendi ya TOT kuandaa nyimbo hizo kabla ya kupeleka kwa kundi zima ili kufanyia mazoezi na kurekodi baada ya kupitishwa.

Wanamuziki hao ni pamoja na Thabit Abdul, aliyekuwa akipiga gitaa la besi na Kinanda, Jerry Juma almaarufu kama JJ, ambaye pia alikuwa akipiga Kinanda, Korobiniani Mkinga, na Gaspar Tumaini.

Akizungumza na mtandao huu mmoja wa wanamuziki hao, Jerry Juma almaarufu kama 'JJ Mzee wa Mbezi', alisema kuwa Marehemu alikuwa amewaalika kushiriki katika kuandaa nyimbo hizo na tayari walikuwa wakifanya mazoezi nyumbani kwake pale Tangibovu Mbezi Beach.

Aidha Jj, alisema kuwa hivi majuzi siku ya Ijumaa kabla ya kifo chake walikuwa pamoja usiku wakifanya mazoezi, ndipo alipowaambia kuwa alikuwa hajisikii vizuri hivyo akaomba apumzike na wamuachie kazi ya kuandika na akawaahidi kuwa akipata nafuu ataamka usiku ili aanze kuandika mashahiri ya nyimbo hizo walizokuwa wakifanyia mazoezi na kuwataka wakutane Jumapili kwa ajili ya kupitia alipofikia ili kufanya marekebisho.

''Tulikuwa tukifanya mazoezi pale nyumbani kwake ghafla, akaanza kusema kuwa hajisikii vizuri, akaomba feni ikaanza kumpepea huku akiendelea nasi kufanya mazoezi, lakini baada ya muda akasema kuwa hajisikii vizuri anahisi kuzidiwa na ndipo alipotuomba kusitisha ili akapumzike na akatuahidi kuwa akipata nafuu ataamka usiku ili aanze kuandika ili kesho yake amalizie kurekebisha ili tukutane siku ya Jumapili tuendelee na mazoezi, lakini kwa bahati mbaya siku iliyofuata Jumamosi akafariki dunia ni kazi ya Mungu''. alisema Jj

Katika Albam hiyo iliyotakiwa kuwa na jumla ya nyimbo tano walishafanikiwa kurekodi wimbo mmoja uitwao CCM Mbele kwa Mbele, ambao waliutumia katika sherehe za miaka 38 ya CCM zilizofanyika kitaifa Mkoani Ruvuma Songea mwezi uliopita.

Wimbo wa pili waliokuwa wakifanyia mazoezi kabla ya kifo cha Kiongozi wao Kapten Komba, unaitwa, Kimewaka kwa CCM Kimenuka kwa Wapinzani, ambao kwa asilimia kubwa ulikuwa ukielekea kukamilika iwapo wangefanikiwa kukutana siku ya Jumapili kama si kofo hicho ili kuongezea maneno na kufanya marekebisho machache kabla ya kufikisha kwa kundi kufanyia mazoezi na kisha kurekodiwa.

Aidha JJ, alisema kuwa katika ablam hiyo alikuwa tayari ametunga wimbo wake mmoja uitwao Wapinzani wamekula za Chembe Lazima wakae, ambao tayari ulikwisha pitishwa na Kiongozi wao marehemu Komba, ambaye alishasema kuwa katika Wimbo huo haongezi wala hapunguzi neno bali ni kufanyia mazoezi tu.

''Ni kweli CCM imepata pengo kubwa sana kwa kuondokewa na Kiongozi wetu Kaapteni John Komba, lakini tunawaahidi Viongozi wetu wasihofu kwani Msiba huu ni wetu sote na Komba ameacha Hazina kubwa ya Vipaji ambayo itafanya yote yaliyoachwa na Kapteni Komba na kwa uhakika ili kumuenzi kiongozi wetu huyu''. alisema JJ

Wimbo huo uliorekodiwa ulifanyiwa kazi katika Studio za Hiland zilizopo Kigogo jijini dar es Salaam, chini ya mwandaaji, Rich, ambapo pia na hizo zilizobaki zinatarajia kuandaliwa katika studio hiyo.

ambapo walitakiwa kuingia studio kurekodi wimbo wa pili wiki hii, lakini kwa mapenzi ya mungu Kiongozi huyo ameacha kazi hiyo bila kuimalizia na kuacha majonzi makubwa kwa wana CCM na Watanzania kwa ujumla.

Marehemu Komba (katikati) akiwa na kundi lake la TOT katika moja ya shughuli za CCM.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.