Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiwasili kwenye Hoteli ya Rainbow, jijini Harare, Zimbabwe kwa ajili ya
kuhudhuria Mkutano wa dharura wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa SDC, uliofunguliwa
leo Aprili 29, 2015 na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Jijini unaojadili kuhusu
Uendelezaji wa Viwanda.
Rais Mugabe, akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal (kkulia), akiwa na baadhi ya Viongozi wenzake katika Mkutano wa dharura
wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa SDC, uliofunguliwa leo Aprili 29, 2015 na Rais
wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Jijini Harare, Zimbabwe, kuhusu Uendelezaji wa
Viwanda.
Baadhi ya Mawaziri wa Tanzania, waliohudhuria mkutano huo
wakimsikiliza kwa makini Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, wakati akisoma hotuba
ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa dharura wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa SDC,
uliofunguliwa leo Aprili 29, 2015, kuhusu Uendelezaji wa Viwanda.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbali mbali za Afrika.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akifuatilia hotuba ya Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, wakati akifungua
rasmi Mkutano wa dharura wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa SDC, uliofunguliwa
leo Aprili 29, 2015, kuhusu Uendelezaji wa Viwanda.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal (katikati), akiwa na baadhi ya Viongozi wenzake wakisimama kuomboleza kifo cha Hashim Mbita, aliyefariki hivi majuzi, nchini Tanzania.
**************************************************************************
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA DHARURA WA VIONGOZI WA NCHI
NA SERIKALI WANACHAMA WA SADC KUHUSU UENDELEZAJI VIWANDA
HARARE, ZIMBABWE
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Jumatano Aprili 29, 2015, ameiwakilisha
Tanzania katika mkutano wa dharura wa Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
uliofanyika jijini Harare, chini ya Uenyekiti wa Rais Robert Mugabe, Rais wa
Zimbabwe, Mwenyekiti wa sasa wa SADC pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika
(AU). Mkutano huo wa siku moja pia umehudhuriwa na Rais Seretse Ian Khama, Rais
wa Botswana na Makamu Mwenyekiti wa SADC, Mfalme Muswati III wa Swaziland, Rais
wa Msumbiji Filipe Nyusi, Rais wa Namibia Hage Geingob, Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Watu wa Lesotho Pakalitha Mosisili, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na Rais
wa Zambia Edgar Lungu.
Awali akifungua mkutano huo Rais Mugabe
alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kuwa na mpango madhubuti wa Viwanda kwa
kuwa uwepo wa viwanda utasaidia kupunguza tatizo kubwa linalozikabili nchi hizi
hasa ajira, pamoja na uchumi duni unaotokana na ukosefu wa viwanda vya
kuboresha bidhaa zinazozalishwa katika nchi za ukanda huu. Mkakati huu
uliopitishwa na Wakuu wa nchi na Serikali wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
unaanza mwaka huu 2015 hadi mwaka 2063.
Katika mkakati huu nchi za SADC
zinalenga kutanua uhuru wa soko katika utatu wa kanda za Kibiashara yaani SADC,
EAC na COMESA ikiwa ni pamoja na kutenga eneo huru la ukanda wa kiuchumi wa
nchi za kanda hizi, huku lengo likiwa kufanikiwa upatikanaji wa eneo huru la
ukanda wa biashara kwa nchi za Afrika. Masuala mengine ni pamoja na kukuza
bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizi katika masoko ya Asia ambao ni walaji na
watumaji wakubwa wa malighafi zinazozalishwa katika nchi hizi.
Rais Mugabe alifafanua pia kuwa, nchi hizi kwa
umoja wake zikiunganishwa utakuta ndizo zina rasimali kubwa ya madini ya
Dhahabu, Almasi na hata Gesi na kwamba kama mtengamano huu utakamilika nguvu ya
pamoja inaweza kugeuza hali ya maisha ya wananchi wa nchi hizi sambamba na
maendeleo ya kiuchumi katika nchi hizo.
Awali akizungumza kabla ya hotuba ya ufunguzi ya
Rais Mugabe, Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stargomena Lawrence Tax aliishukuru
serikali ya Zimbabwe kwa maandalizi mazuri ya mkutano huu ambao ulikuwa ni
mwendelezo wa ule uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe Agosti 17, 2014 mkutano
uliotaka nchi wanachama wa SADC pamoja na kupitisha mkakati wake wa Kimaendeleo,
upange dira ya utanuaji na uendedlezaji viwanda katika ukanda huu.
Matukio mengine katika mkutano huu ni pamoja na
makabidhiano ya Kituo cha Mafunzo ya Utunzaji Amani katika nchi za SADC,
makabidhiano yaliyofanywa na nchi ya Zimbabwe chini ya Rais wake Robert Mugabe
kwa Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt Stargomena Tax. Kufuatia makabidhiano haya,
Chuo hiki sasa kitakuwa kinamilikiwa na SADC na matumizi yake yatahusisha
vyombo na wataalamu mbalimbali wanaohusika na masuala ya utunzaji amani ndani
ya nchi hizi, ili kupata mafunzo ya kuboresha kazi zao kufuatia migogoro kuwa
mingi katika nchi mbalimbali Afrika.
Pia Rais Mugabe alitumia muda huo kuutaka
Mkutano huu wa Dharura kutoa heshima zao kufuatia kifo cha Brigedia Jenerali
Hashim Mbita aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Ukombozi kwa kutambua
mchango wake katika uhuru wa nchi zilizomo SADC na pia mchango wake kwa ajili
ya maendeleo ya nchi hizi. Raia Mugabe alimtaja Hayati Brigedia Mbita kama
mpiganaji mahiri na kiongozi aliyefanya kazi kwa maslahi ya watu wengi bila
kuchoka na kwamba Afrika na SADC vitamkumbuka daima kwa mchango wake huo.
Imetolewa na: Ofisi ya
Makamu wa Rais
Harare,
Zimbabwe
Aprili
29, 2015





No comments:
Post a Comment