Habari za Punde

*YANGA YAWAFANYIA 'KITU MBAYA' COASTAL UNION YAWABANJUA MABAO 8-0 UWANJA WA TAIFA DAR

KATIKA kile kisichotarajiwa na wengi Yanga leo imewashangaza mashabiki wa Soka nchini na kuwaachia Coastal Union kumbukumbu isiyofutika kwa kuwabanjua jumla ya mabao 8-0, huku Amis Tambwe akitupia mabao manne peke yake, na Simon Msuva akiendelea kung'ara na kuongoza katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akitupia bao moja na kufikisha idadi ya mabao 13 akiwa juu ya kavumbagu.

Alikuwa ni Amis Tambwe aliyeanza kufungua pazia la mabao kwa bao zuri la kichwa, katika dakika ya tisa akiunganisha mpira wa Sherman baada ya Oscar Joshua kupiga mpira wa adhabu na Simon Msuva akifunga bao la pili katika dakika ya 23 kwa shuti la mbali akiunganisha pasi nzuri ya Amis Tambwe.

Bao la tatu lilifungwa na beki wa kulia, Juma Abdul, katika dakika ya 48. Bao la nne lilifungwa na Amis Tambwe tena katika dakika ta 49 huku bao la tano likifungwa na Mliberia Kpah Sherman katika dakika ya 50,  akiosha nyota kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga na timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.
Alikuwa ni Simun Msuva tena katika dakika ya 87, aliyeifungia timu yake bao la Sita akiunganisha pasi nzuri ya kichwa ya Amis Tambwe, huku Salum Telela, akiiandikia Yanga bao la Saba katika dakika ya 88, kwa shuti kali aliunganisha pasi ya Simon Msuva na bao la nane likifungwa tena na Amis Tambwe katika dakia ya 90.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Kocha wa Coastal Union, Jamhuri Khweru 'Julio', alisema kuwa alitegemea timu yake itafungwa na Yanga ingawasi kwa idadi kama hiyo ya magoli 8-0.

''Nilitegemea timu yangu kupoteza mchezo wa leo ingawa si kwa idadi kubwa kama hii ya magoli nane, mimi ratiba yangu ilikuwa ikionyesha kuwa tunatakiwa kucheza na Yanga Machi 18, na juzi nikiwa katika michezo ya Bonanza la Pasaka ndiyo nikaambiwa nijiandae kwa mchezo wa leo, huku nikiwa tayari nimeshawapa mapumziko  wachezaji wangu baada ya Sikukuu,

Hivyo kukutana na timu kama Yanga ambao wametoka kwenye mchezo wa kimataifa hivi juzi tu ni kama miujiza, wachezaji wangu walipoteza stamina na umakini na ndiyo maana tukafungwa idadi hiyo ya magoli na kama tungekuwa tumecheza na timu ya Simba leo tungefungwa mabao hata 10''. alisema Julio

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara kati ya Mabingwa Azam Fc na Mbeya City, timu hizo zimetoka suluhu kwa kufungana bao 1-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Na kwa matokeo hayo Yanga wameendelea kujichimbia kileleni wakiwa na jumla ya Pointi 43, baada ya kuchezaa michezo 20 wakifuatiwa na Azam Fc wenye Pointi 37  wakiwa wamecheza michezo 19 na kuzidi kuuweka rehani ubingwa wa Ligi Kuu.
KWA MATUKIO YA PICHA ZA MTANANGE HUO, KAA NASI BAADAYE.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.