Baadhi ya wananchi
wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda
akitoa hotuba ya ufunguzi wa Maonesho ya 22 ya Nane Nane leo katika viwanja vya
Ngongo Mkoani Lindi.
*********************************************
Na Eleuteri Mangi-Lindi
Maonesho ya Nane Nane
nchini yamekuwa shamba darasa ambalo wananchi wanakutanishwa kujifunza masuala
mbalimbali ambapo wakulima na wafugaji na wananchi kwa ujumla wanaweza kutoka
na mambo kadhaa kwa manufaa ya kuongeza kipato cha kaya na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda leo wakati akifungua
rasmi Maonesho ya 22 ya Nane Nane kitaifa mwaka huu katika viwanja vya Ngongo
Mkoani Lindi.
“Nimetembelea mabanda
mengi nimefarijika sana na nimevutiwa na mambo mengi ya kilimo na maandalizi
mazuri yanayopamba maadhimisho haya, katika mabanda hayo nimevutiwa zaidi na
banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Wamelima mboga mboga, mchicha,
vitunguu, biringanya, mahindi, matango na nyanya. Wote mliokuja kwenye maonesho
haya mkajifunze uzalishaji huo ni wa muhimu kwa kila mtu”alisema Waziri Mkuu Pinda.
Aidha, Waziri Mkuu
ameiongezea kanda ya kusini miaka miwili zaidi na kuandaa maonesho hayo kitaifa
na hivyo yatafanyika miaka mitano mfululizo ambapo yanatarajiwa kujumuisha
mwaka 2014 yalipoandaliwa kwa mara ya kwanza hadi 2018.
Muda huo umeongezwa ili
kuendelea kufungua na kuboresha miundo mbinu ya viwanja vya Ngongo mkoani Lindi
na mikoa ya kusini kwa ujumla ikiwemo huduma za jamii ndani ya mikoa hiyo na
kuongeza hamasa ya ushiriki kutoka taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma
pamoja na asasi mbalimbali nchini.
Kwa upande wake mkazi
wa eneo la Ngongo kijiji cha Tulieni kata ya Mnazi Moja Mkoani Lindi mzee
Shaibu Said Chibebedenge amesema kuwa maonesho ya mwaka huu yamaendelea kuwa
bora zaidi kuliko mwaka uliopita kwa kuongezeka ubora wa miundo mbinu ikiwemo
barabara ndani ya viwanja vya Maonesho.
Maonesho ya Nane Nane
nchini yameanzishwa rasmi mnano mwaka 1993 ambapo hadi sasa yanaendelea kote
nchini kupitia kanda saba ambazo ni Arusha, Dodoma, Morogoro, Mbeya, Mwanza,
Tabora na Lindi ambapo maonesho hayo yanafanyika kitaifa kwa mara ya pili
mfululizo.

No comments:
Post a Comment