Habari za Punde

*MAHAKAMA YA ARDHI YAWEKA ZUIO LA BOMOA BOMOA WILAYA YA KINONDONI DAR

Na Raymond Mushumbusi  MAELEZO
Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi imeweka zuio la kubomoa nyumba zilizopo katika wilaya ya Kinondoni hasa zile ambazo wamiliki wake wameleta ombi lao mahakamani kuzuia kubomolea. 
Akitoa hukumu hiyo mbele ya walalamikaji, wakili wa Serikali, mawakili wa walalamikaji na wananchi, Jaji wa Mahakama hiyo kuu ya Ardhi Mhe.Panterine Kente amesema kuwa mahakama imezingatia maelezo toka pande zote mbili kwa kuangalia madhara watakayopata wananchi kwa kutekelezwa kwa zoezi hilo.
Jaji Panterine Kente ameongeza kuwa mahakama ya Ardhi haijaweka zuio la bomoa bomoa kwa Tanzania nzima bali kwa wale tu walioleta maombi ya shauri la zuio la kubomolewa nyumba zao na kusisitiza kuwa Serikali  itaendelea na uwekaji wa alama za x na ubomoaji wa nyumba zilizopo sehemu hatarishi na sehemu zisizostahili.
“ Nakuagiza Wakili Abubakari Salim uniletee majina yote leo hii na sio kesho ya waliofungua shauri la zuio la kutobomolewa nyumba zao ili tuweze kuendelea na zoezi la ubomoaji” Alisema Jaji Kente
 
Akizungumza baada ya kutolewa hukumu hiyo Wakili wa Serikali Manchare Henche amesema wamepokea hukumu hiyo na wao wataendelea na majukumu yao ya ubomoaji wa maeneo hatarishi kama Mahakama ilivyoeleza kuwa haijatoa zuio la bomo bomoa kwa Tanzania nzima ila kwa wale tu walioleta shauri la zuio.
“Tunaomba walio maeneo ya mabondeni wahame kwani zoezi hili linaendela na zoezi la uwekaji wa alama za x litaendelea kama kawaida kwa maeneo mengine nje ya haya yaliyowekewa zuio” Alisema Henche.
Aidha akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa hukumu hiyo Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Maulid Mtulia amesema kuwa uamuzi umeridhisha na pia mahakama imetenda haki kwa wananchi wa kinondoni na wanashukuru kwa kupata nafasi ya kusikilizwa kwa hoja zao.
 
Kesi hiyo namba 822ilifunguliwa na wawakilishi nane wanaowawakilisha  wanachi 674 ambao nyumba zao zilikuwa katika mpango wa kubomolewa  chini ya sheria za mipango miji.
Baada ya Mahakama kuu ya Tanzania kitengo cha Ardhi kutoa zuio la bomoa bomoa kwa wakzi hao kesi ya msingi itatajwa tena januari 11.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.