Kocha mwenye kila aina ya mbwembwe,vituko na makeke, Jose Mourinho, amefikia makubaliano ya kuchukua mikoba ya Louis Van Gaal na hivyo kuwa kocha mpya wa timu ya Manchester United aka Mashetani Wekundu.
Kwa mujibu wa mtandao wa BBC Sport, makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo ya siku takribani tatu. Wakala wa Jose Mourinho na uongozi wa juu waManchester United wamefikia makubaliano na kwamba uamuzi huo wa kumuajiri raia huyu wa Ureno utatangazwa rasmi hapo kesho (Ijumaa).
Kwa mujibu wa SkySport tayari mkataba rasmi wa kuinoa Manchester kwa miaka mitatu umeshatiwa sahihi na Jose Mourinho alionekana akirudi nyumbani akiwa ameshikilia mkataba huo na chupa ya mvinyo mwekundu. Atalipwa kiasi cha Paundi Milioni 45 kwa miaka hiyo mitatu. Inasemekana amepewa zaidi ya paundi Milioni 200 kwa ajili ya kusajili vipaji mbalimbali wakati huu wa msimu wa majira ya joto.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea amekuwa bila kazi tangu December mwaka jana alipofungashiwa virago. Atachukua mikoba ya Van Gaal ambaye pamoja na kushinda kikombe cha chama cha mpira wa miguu nchini Uingereza (FA) kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace, muda wake wa kuendelea kuinoa Manchester ulikuwa umeshafikia mwisho.
Kibarua cha kwanza kwa Mourinho kitakuwa tarehe 7 August wakati Manchester United watakapoumana na mabingwa wapya wa EPL timu ya Leicester City katika kuwania Ngao Ya Hisani katika Uwanja wa Wembley jijini London.

No comments:
Post a Comment