Meneja wa Wakala
wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, akimuonesha Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, sehemu ya ujenzi wa barabara ya mchepuo kutoka Chimwaga-Ihumwa yenye urefu wa KM 10
inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa
ajili ya kupunguza msongamano wa magari
yanayoingia mkoani humo.
Mhandisi Mkazi anayesimamia ujenzi wa barabara ya Chimwaga-Ihumwa KM 10 kwa kiwango cha lami, Mhandisi Nicholaus Mzeru, akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi kwa waandishi wa habari ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92.4 na KM 8 zimeshakamilika kujengwa, mkoani Dodoma
***************************************
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Elias Kwandikwa, amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Mbande - Kongwa (Km 11.7)
na Chimwaga - Ihumwa (Km 10) utasaidia kupunguza msongamano kwa magari
yanayoingia Dodoma mjini.
Naibu Waziri huyo
ameyasema hayo wakati akikagua barabara hizo na kuridhishwa na kasi ya ujenzi
wake ambapo amesisitiza kwa makandarasi wanaojenga barabara hizo kuhakikisha
wanamaliza kazi hizo kwa muda uliopangwa na kwa viwango vilivyo kwenye mkataba.
"Tutaendelea
kujenga na kuboresha barabara hizi za mchepuo lengo ni kupunguza foleni
katikati ya mji kwani Dodoma sasa inakua kutokana na uwepo wa watumishi wengi
wa Serikali na ongezeko la magari, kwa hiyo sisi kama Serikali hatuna budi
kuangalia namna ya kuboresha miundombinu yetu ili ikidhi haja ya ongezeko
hili", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, amefafanua kuwa
barabara hizo zikikamilika zitakuwa ni njia mbadala kwa watumiaji kwani sio
lazima kwa magari yote kupita mjini na badala yake yatatumia njia nyingine za
mchepuo kuendelea na safari zake.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua athari za mvua katika barabara
za mji wa Dodoma na kuwataka wananchi na madereva kuchukua tahadhari ili
kuepusha hatari zinazoweza kuwakabili wakati wakivuka ama kupitisha
magari yao katika kipindi hiki ambacho baadhi ya sehemu za barabara
zinajaa maji kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Amewaomba viongozi
mbalimbali wa Serikali kushirikiana katika kutoa ushauri kwa wananchi
kuhusu utafutaji wa maeneo yanayowafaa kuishi ili kunusuru maisha yao na
mafuriko ambayo yanaweza kuwakabili kutokana na kuchagua maeneo yasiyo sahihi
kwa makazi ya binadamu.
Kwa upande wake, Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard
Chimagu, amefafanua kuwa barabara ya Mbande- Kongwa yenye urefu wa
KM 11.7, kwa sasa imejengwa kilometa Tano ikiwa ni awamu ya kwanza na kufikia
mwezi ujao watajenga tena kilometa nyingine Tano.
Naye, Msimamizi wa ujenzi
wa barabara ya Chimwaga - Ihumwa yenye urefu wa KM 10 kwa kiwango cha lami,
Mhandisi Nicholaus Mzeru, amesema mradi ulianza mwaka 2013, ambapo kwa
sasa umefika asilimia 92.4 na kilometa 8 tayari zimeshajengwa.
Ujenzi wa Barabara ya
Chimwaga- Ihumwa (Km 10), inajengwa na mkandarasi Nyanza Road Works kwa
gharama ya takriban shilingi bilioni 15 ambapo ujenzi wake unaendelea na
unategemewa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, athari za mvua eneo la katondo katika barabara za mji huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akiongozana na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, wakikagua athari za mvua eneo la Kibaigwa, katika barabara ya Dodoma-Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana nae wakati akikagua athari za mvua eneo la Kibaigwa, katika barabara ya Dodoma-Dar es Salaam.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Mbande-Kongwa yenye urefu wa KM 11.7 inayojengwa kwa kiwango cha lami, ambapo mpaka sasa KM 5 tayari zimekamilika, mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment