Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Godfrey Zambi, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandika, kuhusu hali ya miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko, pamoja na
viwanja vya ndege katika mkoa huo. Naibu Waziri huyo yupo katika ziara ya
kikazi ya siku 3 mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na uongozi wa mkoa wa Lindi katika kikao kazi, kuhusu umuhimu wa wataalamu wote kushirikiana katika masuala ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika mkoa huo. Kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Lindi, Mhandisi Isaack Mwanawima akisikiliza.
Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Lindi, Mhandisi Grayson Maleko, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu ujenzi wa maegesho ya kivuko kitakachotoa huduma kati ya Lindi Mjini na Kitunda, alipokuwa akikagua ujenzi wake mkoani humo.
Muonekano wa ujenzi wa maegesho ya kivuko kitakachotoa huduma kati ya Lindi Mjini na Kitunda, ambapo mkataba wa kukikokota Kivuko hiko kutoka Pangani mkoani Tanga kuja Lindi upo katika hatua za mwisho.
**************************************
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Elias Kwandikwa, ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)
makao makuu kusaini haraka mkataba kwa mkandarasi atakayebeba kivuko
kipya kutoka eneo kinapotengenezwa wilayani Pangani mkoani Tanga hadi
mkoani Lindi.
Akizungumza mara baada
ya kukagua maegesho ya kivuko hicho ambacho kinatarajiwa kutoa huduma za
usafiri kutoka Lindi Mjini - Kitunda mkoani humo, Naibu Waziri huyo
amewahakikishia wananchi kutegemea kupata huduma nzuri za usafiri kwani ujenzi
wa kivuko na maegesho yake kwa sasa umefika katika hatua
nzuri.
"Naagiza Mamlaka
husika kusaini haraka mkataba kwa mkandarasi atakayebeba kivuko hiki
kutoka Tanga hadi hapa ili wananchi waone kwamba kivuko kimefika na kipo tayari
kwa ajili ya kutoa huduma", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameridhishwa na ujenzi wa maegesho hayo ambayo kwa
sasa ujenzi wake umebakia asilimia 10 na hivyo kutarajiwa kukamilika muda
wowote.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa, ametembelea na kukagua uwanja wa
ndege wa Lindi ambapo amesema Serikali inaendelea na mpango wake wa kuboresha
viwanja vya ndege nchini ili kuimarisha huduma katika usafiri wa anga.
Amefafanua kuwa Serikali
kupitia mwaka wa fedha 2018/19 licha ya kuwa na mpango wa kuboresha uwanja huo
pia itaboresha Uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko lengo ni kuleta maendeleo kwa
wananchi.
Kwa upande wake Meneja
wa TEMESA mkoani Lindi, Mhandisi Greyson Maleko, amemhakikishia Naibu Waziri
huyo kujipanga katika kuhakikisha wananchi wa Lindi wanapata huduma bora za
kivuko.
Naye, Mbunge wa Viti
Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo Mheshimiwa Hamida
Abdallah, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusogeza
maendeleo kwa wananchi na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Naibu Waziri Kwandikwa
amemaliza ziara ya kikazi ya siku Tatu mkoani humo ambapo ametembelea na
kukagua Miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake ili kujionea maendeleo
na changamoto zake.
No comments:
Post a Comment