Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Uchaguzi Kanda ya Pwani kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Stephen Elisante akizungumza na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wa ngazi ya Jimbo la Kinondoni na Kata za jimbo hilo kwenye mafunzo ya maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Februari 17, 2018.
Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kinondoni Boniface Lihamwike akiwaapisha wasiamamizi wasaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni na kata zake wakati wa mafunzo ya maandalizi ya Uchaguzi Mdogo.
Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni, Victoria Wihenge, akiwasilisha Mada ya Maelekezo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata kwa wasiamamizi wa Kinondoni. Picha na Hussein Makame-NEC
*****************************************
Hussein
Makame-NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewakumbusha
wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika
kusimamia uchaguzi ili kufanikisha Uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika
Februari 17, 2018.
Hayo yamsemwa na Kaimu Mkuu wa Sehemu
ya Uchaguzi Kanda ya Pwani kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Stephen Elisante
wakati akifungua mafunzo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la
Kinondoni na Kata za jimbo hilo la jiji la Dar es Salaam.
Alisema wasimamizi wa Uchaguzi
wanapaswa kutambua kuwa Uchaguzi ni mchakato unaohusisha taratibu mbalimbali
kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni, taratibu, maelekezo na miongozo
iliyotolewa kisheria.
“Hivyo mnapaswa kuzisoma sheria hizo
ili kuweze kutekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria...,tufanye maamuzi
yetu kwa kujitambua, kujiamini na kutoogopa na kuchukua hatua za haraka katika
kushughulikia changamoto zinazojitokeza” alisema Elisante.
Aliwakumbusha wasimamizi hao wa
Uchaguzi kuwa Tume imekuwa ikisisitiza kwamba Sheria za Uchaguzi hazikuacha
ombwe katika kueleza jinsi gani masuala ya Uchaguzi yanatakiwa yatatuliwe.
Kwa upande wake Afisa Uchaguzi wa
Jimbo la Kinondoni, Victoria Wihenge akiwasilisha mada ya Maelekezo kwa
wasimamizi hao, aliwataka kutoruhusu matumizi ya utambulisho mwingine mbadala
tofauti na ule ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeruhusu kutumika.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 61 (3) (a)
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya
Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, kimeipa mamlaka Tume kuidhinisha
matumizi ya utambulisho mwingine tofauti iwapo mpiga atakosa kadi ya kupigia
kura” alisema Victoria na kusisitiza kuwa:
“Vitambulisho vilivyoruhusiwa na Tume
ni vitatu, Kitambulisho cha Taifa, Hati ya Kusafiria kwa maana ya Passport na
Leseni ya Udereva, hivyo mtu akikosa kadi ya kupigia kura au vitambulisho hivyo
hakuna utambulisho wowote utakaoruhusiwa ili mtu aweze kupiga kura”
Mafunzo hayo kwa wasimamizi wasaidizi
wa Uchaguzi kwa ngazi ya Jimbo la Kinondoni na kata zilizoko kwenye jimbo hilo,
yalijumuisha viapo kwa wasiamamizi hao walioapa kutunza sira na kujivua au
kukiri kuwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo
la Kinondoni pamoja na Jimbo la Siha na Udiwani katika kata 10 za Tanzania,
unatarajiwa kufanyika tarehe 17 Februari mwaka 2018.



No comments:
Post a Comment