Naibu Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa (katikati) akizungumza na Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), mkoa wa Ruvuma, Eng. Lazeck Alinanuswe (kulia), wakati akikagua
barabara ya Mbinga-Mbamba Bay yenye urefu wa KM 67 inayotarajiwa kujengwa hivi
karibuni kwa kiwango cha lami na mkandarasi
CHICO.
Muonekano wa
barabara ya Mbinga-Mbamba Bay yenye urefu wa KM 67 inayotarajiwa kujengwa hivi
karibuni kwa kiwango cha lami na mkandarasi
CHICO. Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa tarehe 11 mwezi
Disemba mwaka jana.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa (mbele), akishuka ngazi wakati wa ukaguzi wa mradi wa
ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa unaojengwa na Wakala wa
Majengo (TBA), mkoa wa Ruvuma na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo.
Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA), mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Edwin Nunduma, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya
kukagua miradi ya ujenzi wa jengo la ofisi na nyumba ya makazi ya Mkuu wa
Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma. Miradi hiyo inajengwa na Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA).
Muonekano wa hatua ya awali ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma. Mradi huo unajengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
**************************************
Wananchi wa Mbamba Bay
wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara
ya Mbinga-Mbamba Bay (km 67), kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za
usafirishaji wa abiria na mizigo wanazozipata hususan katika kipindi cha
masika.
Wananchi hao wametoa
kero hiyo mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, alipofika wilayani
hapo kukagua barabara hiyo ambapo wamefafanua kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na
maliasili nyingi, wawekezaji na wafanyabiashara hushindwa kufika kutokana na
changamoto ya barabara, hivyo kupelekea uchelewaji wa maendeleo katika wilaya
yao.
"Uduni wa barabara
hii unapelekea kutopata maendeleo ya haraka, pia usafiri kutoka hapa kwenda
maeneo mengine ya jirani huwa mgumu hususan katika kipindi cha mvua kwani
madereva wengi hupandisha nauli", amesema mmoja wa wakazi wa Mbamba Bay, Bw.
Bahati Ndege.
Aidha, wananchi hao wameipongeza
Serikali kwa hatua zinazofanya katika utatuzi wa kero mbalimbali
zinazowakabili, hivyo wamefafanua kuwa Serikali kuamua kujenga barabara ya lami
kutaboresha uchumi katika wilaya yao na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri Elias Kwandikwa, amesema kuwa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo
umesainiwa tangu Mwezi Desemba mwaka jana na kufafanua kuwa kinachosubiriwa
sasa ni kwa mkandarasi kufika eneo la mradi na kuleta mitambo yake.
"Kila kitu kipo
tayari, Wananchi wasubiri kwa hamu ujenzi wa barabara hii ambao unatarajiwa
kujengwa kwa shilingi bilioni 129 na mkandarasi CHICO kwa ufadhili wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Amepongeza uongozi wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo kwa kuweka changarawe katika
barabara hiyo ambapo kwa namna moja inasaidia kurahisisha usafiri kwa kipindi hiki
ambacho mkandarasi anasubiriwa kufika eneo la kazi.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri huyo amekagua mradi wa ujenzi wa Ofisi na Nyumba ya Makazi ya Mkuu
wa Wilaya ya Nyasa zinazojengwa na Wakala wa Majengo (TBA), mkoani humo na kuridhishwa
na kasi ya ujenzi wake.
Naye, Meneja wa TBA
mkoani humo, Mhandisi Edwin Nunduma, amesema kuwa TBA katika wilaya hiyo ina
jumla ya miradi minne inayoendelea kwa sasa ikiwemo mradi wa ujenzi wa
zahanati, nyumba na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo amemhakikishia Waziri huyo
kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Naibu Waziri Kwandikwa
ameanza ziara ya kikazi mkoani Ruvuma ambapo leo amekagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Wizara yake ili kujionea maendeleo yake.

No comments:
Post a Comment