Mhandisi Mkuu kutoka
Shirika la Reli (TRL), Mhandisi Nelson Ntejo akitoa maelezo kwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia) kuhusu maendeleo
ya kazi ya ukarabati wa eneo lililoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha mwanzoni
mwa mwaka, katika eneo la Kilosa mkoani Morogoro, wakati Waziri huyo alipokagua
reli hiyo Mkoani humo, hivi karibuni.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mhandisi
Mkuu kutoka Shirika la Reli (TRL), Mhandisi Nelson Ntejo, alipokagua ukarabati
wa njia ya reli ya kati ya eneo la Kilosa mkoani Morogoro iliyoharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha
mwanzoni mwa mwaka huu. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua kazi zinazoendelea
katika eneo la Kilosa, ambapo ukarabati umekamilika na treni za mizigo zimeanza
kupita.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akishiriki katika kazi za kujaza mchanga kwenye viroba vinavyotumika kama kingo za kudhibiti maji ya mto Mkondoa yasifike kwenye miundombinu ya reli katika eneo la kilosa, mkoani Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Dkt. Stephen Kebwe, akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika
la Reli (TRL), na wakazi wa Kilosa, wakati alipokagua ukarabati wa njia ya reli
ya kati eneo la Kilosa karibu na mto Mkondoa, mkoani humo.
Muonekano wa treni ya mizigo ikianza safari zake katika stesheni ya Kilosa, mkoani Morogoro kuelekea mkoani Mwanza mara baada ya njia hiyo kukarabatiwa.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro Dkt. Stephen Kebwe na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adamu Mgoyi,
alipokutana nao katika ukaguzi wa ukarabati wa njia ya reli ya kati kutoka eneo
la Kilosa.
Muonekano wa sehemu ya njia ya reli ya kati eneo la Kilosa iliyokarabatiwa baada ya kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha, mkoani Morogoro mwanzoni mwa mwaka huu.
*********************************************
Shirika
la Reli Tanzania (TRL) limepata hasara ya takribani shilingi bilioni tano
katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya njia ya reli ya kati kusombwa na
mafuriko katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya reli hiyo
na kusema kuwa Serikali imejipanga kupata suluhisho la kudumu la uharibifu
katika maeneo hayo ambapo mara kadhaa yamekuwa yakiathiriwa na mvua kutokana na
mabwawa yaliyopo kujaa mchanga na hivyo kusababisha uharibifu huo.
“Serikali
kwa sasa inayafanyia kazi mapendekezo matatu yaliyowasilishwa na RAHCO
ikiwemo kuihamisha reli kwenye milima jirani, kuihamishia eneo
ambapo inajengwa reli ya kisasa ya SGR ama kujenga tuta kubwa, huku
tukizingatia gharama halisi za kazi hiyo kabla ya kufanya maamuzi",
amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza
kuwa mbali na Serikali kuja na suluhu ya muda mfupi ya kurejesha safari za
treni pia amewatoa hofu wafanya biashara kwa kuwahakikishia kuwa mizigo yao iko
salama na itasafirishwa kwa wakati.
Kwa
Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe, amemuhakikishia Waziri
Prof. Mbarawa kuwa Mkoa umejipanga kuhakikisha unatoa elimu kwa wananchi kwenye
utunzaji wa mazingira ili kunusuru uharibifu unaotokea kutokana na shughuli za
kibinadamu.
“Kama
Mkoa tumejipanga kuwa kuanzia sasa Sheria zilizopo zinazokataza kulima
kandokando ya mito na kando ya reli sasa zitafuatwa na tutaendelea kutoa
elimu kwa wananchi ili miudombinu hiyo isiathirike kwa sababu ya shughuli za
kibinadamu zinazofanywa kupitia kilimo", amesisitiza Dkt. Steven
Kebwe.
Ameongeza
kuwa kuanzia mwakani mkoa umejipanga kutenga fedha kwa ajili ya kutumia njia za
asili kulinda miundombinu hiyo kwa kupanda miti na kuotesha matete ili kulinda
miundombinu.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Massanja
Kadogosa, amesema kazi ya ukarabati imekamilika kwa sehemu kubwa kwani
tayari treni tano za mizigo zimepita salama na kuongeza kuwa kazi
zinazomaliziwa kwa sasa ni kujaza mchanga kwenye matuta ya reli hiyo na
kumalizia kingo ili kuilinda reli.
No comments:
Post a Comment