Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wakazi wa kijiji
cha Kisorya, wilaya ya Bunda alipokutana nao baada ya kukagua ujenzi wa
barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 inayojengwa kwa kiwango cha
lami, wilayani humo, mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, katika ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Bunda, mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mwibara, akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati wa ukaguzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Bunda, mkoani Mara.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Bunda, mkoani Mara.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Makutano-Sanzate yenye urefu wa KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 54. Barabara hiyo inajengwa na wakandarasi wazawa M/S Mbutu JV.
*****************************************
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi Nyanza Road
Works kukamilisha ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51
kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Prof. Mbarawa ametoa
kauli hiyo wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo na kuzungumza na wananchi wa
kijiji cha Kisorya na kusema kuwa usanifu wa barabara na madaraja katika
barabara hiyo umewasilishwa sasa ni jukumu la mkandarasi kuendelea na ujenzi
kwa kasi na kwa viwango vya ubora.
"Serikali ina nia
njema kwa wananchi wa wilaya ya Bunda na mkoa wa Mara sasa tunaijenga barabara
hii na mwishon mwa mwaka mtaanza kunufaika nayo", amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Ameongeza kuwa kukamilika
kwa barabara hiyo utarahisisha mawasiliano na kupunguza gharama za shughuli za
usafirishaji wa samaki, mazao na abiria, uboreshaji makazi na kukuza uchumi kwa
maeneo yaliyo kando ya barabara.
Kuhusu suala la fidia,
Prof. Mbarawa amefafanua kuwa Serikali italipa fidia kwa mwananchi ambaye
barabara imemfuata kama anavyostahili.
"Serikali haina nia
ya kumuonea mtu yeyote bali inachofanya inalipa kulingana na sheria
inavyoelekeza", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine
Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Makutano-Sanzale KM 50 na
kumwagiza mkandarasi wa M/S Mbutu JV Contractor (T) kuhakikisha wanakamilisha
mradi huo kabla ya mwezi Julai mwaka huu.
"Mradi huu ni wa
muda mrefu sana na wananchi wameusubiri kwa muda kama hamtamaliza mradi huu
mpaka mwezi juni, hii itakuwa kazi yenu ya mwisho, maana ninategemea nyinyi
kama wazawa mngekuwa wa mfano" amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema kwa sasa mkoa umeamua
kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa miradi ya barabara kila baada ya miezi
mitatu ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Naye Meneja wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mara, Mhandisi Mlima Ngaile amesema Wakala
utasimamia mradi wa ujenzi wa barabara hizo na kuhakikisha mradi unazingatia
viwango kulingana na mkataba.
Waziri Prof. Mbarawa
yuko mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili akiwa na lengo la kukagua utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya sekta ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment