Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akimsikiliza kwa makini Mkuu
wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri (kushoto), alipomtembelea ofisini kwake katika
ziara yake ya kikazi mkoani humo kwa lengo la kukagua miradi ya ujenzi ya
barabara iliyokamilika na inayoendelea. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora,
Queen Mlozi.
Mbunge wa jimbo
la Urambo, Mhe. Magreth Sitta, akimshukuru Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa (kulia), kwa kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa barabara
ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 inayojengwa kwa kiwago cha lami, mkoani
Tabora. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani), kuhusu hatua za mradi wa ujenzi wa barabara ya
Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 na kusisitiza nia ya Serikali ya kuwajengea
uwezo wakandarasi wazawa ili waweze kutekeleza miradi ya ujenzi hapa nchini.
Mbunge wa jimbo
la Urambo, Mhe. Magreth Sitta, akiagana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara
ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.
Muonekano wa
Daraja la Kasisi lenye urefu wa mita 54 lililopo katika barabara ya
Tabora-Pangale yenye urefu wa KM 30. Ujenzi wa barabara hiyo umefikiwa asilimia
80 na inajengwa na mkandarasi CICO kwa gharama ya shilingi bilioni 28.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na uongozi wa Wilaya ya Urambo, alipokutana nao katika ziara yake ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, na uongozi wa
wilaya ya Tabora wakipita juu ya daraja la Wala lenye urefu wa mita 34 katika
barabara ya Tabora-Pangale yenye urefu wa KM 30, katika ukaguzi wa ujenzi wa
barabara hiyo, mkoani humo
***************************************
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka
makandarasi wazawa wa kampuni ya Samota, Anam na Jossam JV wanaojenga barabara
ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 kwa kiwango cha lami wahakikishe wanakamilisha
ujenzi wa barabara hiyo kwa muda uliowekwa.
Prof.
Mbarawa ametoa agizo hilo katika kijiji cha Motomoto, Wilaya ya Urambo mkoani
Tabora alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua mtandao wa barabara
mkoani humo na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Nataka
nione kazi za ujenzi zinafanyika kwa haraka, kwani uzoefu unaonesha baadhi ya makandarasi
wazawa wamekuwa na kasi ndogo, hivyo mjipange vizuri ili barabara ikamilike kwa
wakati”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesema
kuwa nia ya Serikali ni kuwajengea makandarasi wazawa uwezo ili waweze
kutekeleza miradi mikubwa mingine ya ujenzi hapa nchini lakini haitasita
kuwanyima kazi hizo kama miradi hiyo itacheleweshwa, haitakidhi viwango
vinavyohitajika na kama hawataonekana eneo la kazi kwa kipindi kirefu.
“Mkandarasi
mzawa atakayechelewesha mradi wowote wa ujenzi hatapewa kazi nyingine kwa
sababu atakuwa amechelewesha maendeleo ya wananchi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Ameongeza
kuwa Serikali imejipanga kuwalipa makandarasi wazawa kwa wakati ili waweze
kutekeleza miradi yao kwa ufanisi.
Naye
Mbunge wa jimbo la Urambo, Magreth Sitta, amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa
ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi wa wilaya yake na Kaliua na hata
mikoa jirani kwani usafirishaji wa mazao na abiria utarahisishwa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa amesema wamejipanga
vyema kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wazawa hao, na kuahidi kumsimamia ili
amalize kazi hiyo kwa wakati, lakini kwa kiwango.
Awali
akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), mkoani humo Mhandisi Damian Ndibalinze, amesema mkandarasi
ameshapewa fedha za mradi hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huo na
kuahidi kuwasimamia ili wakamilishe kabla ya mwaka 2020.
Ameongeza
kuwa ujenzi wa barabara hiyo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 37.6 na zote
zikiwa zinafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
asilimia 100.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya
Tabora-Pangale yenye urefu wa KM 30 inayojegwa na mkandarasi CICO kwa gharama
ya shilingi bilioni 28.6 na kumtaka mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi wa
barabara hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi wa sita.
Waziri Prof. Mbarawa
yuko mkoani Tabora kwa ziara ya siku mbili akiwa na lengo la kukagua
utekelezaji wa miundombinu ya barabara, mkoani humo
No comments:
Post a Comment