JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon
Sirro anawashukuru Wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Jeshi la Polisi
jambo ambalo limesaidia kupunguza
uhalifu kwa kiasi kikubwa hapa nchini. Kiujumla hali ya usalama hapa nchini ni
shwari na matukio makubwa ya uhalifu wa
kutumia Silaha yamepungua kwa kiasi kikubwa na jitihada za kukabiliana na
makosa ya usalama barabarani zinaendelea ili kupunguza ajali zinazosababisha vifo na
majeruhi kwa raia.
Tunapoelekea kipindi hiki cha Sikukuu
ya Pasaka, Jeshi la Polisi katika mikoa yote linawahakikishia wananchi kuwa limejipanga
kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha
kuwa sikukuu hii inasherekewa kwa amani na utulivu na hakuna vitendo vyovyote
vya uhalifu vitakavyofanyika na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi utaimarishwa kwenye
maeneo yote yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe, sehemu za starehe na maeneo
mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuhakikisha wananchi
wote wanasherekea sikukuu hiyo katika hali ya utulivu.
Wazazi wanatakiwa kuwaangalia
watoto wao na kutowaacha kutembea peke yao bila ya kuwa na uangalizi wa karibu,
pia wamiliki wa kumbi za starehe wanatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za
uendeshaji wa kumbi hizo ikiwemo kutoruhusu disko toto na kujaza watu kupita
kiasi.
Vilevile Jeshi la Polisi
linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na
kuzingatia Sheria za Usalama barabarani hasa kwa madereva wa magari na pikipiki
kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia
vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.
Nawatakia Pasaka njema.
Imetolewa na:
Simon Sirro
Inspekta Jenerali wa Polisi
Makao Makuu ya Jeshi la Polisi

No comments:
Post a Comment