WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Camillus Membe, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 117 tangu kuzaliwa kwa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana ofisi za Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), sherehe hizo zitafanyika Jumapili Juni 26, 2011 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mbio za kujifurahisha yaani Fun Run.
Taarifa hizo zilizotokana na barua ya mwaliko kutoka TOC kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Amir Mhando, zinasema kwamba Membe atashiriki mbio za wazee za urefu wa kilometa tano (km 5) na pia kutakuwa na mbio kwa ajili ya watoto za umbali wa km 2.5.
Barua hiyo ya Juni 13, 2011 yenye kumbukumbu Na. TOC/ODR/VOL. IV/66 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi, inasema kwamba mbio hizo zitafanyika kuanzia saa 12.00 alfajili ambako usajili utafanyika dakika chache kabla ya kuanza.
“Baada ya maadhimisho haya kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini ikiwa pamoja na Pwani, Tabora, Zanzibar , Kagera, Dodoma nakadhalika...Kamati ya Olimpiki Tanzania kwa kushirikiana na Mkoa wa Dar es Salaam itaadhimisha siku hiyo katika Uwanja wa Taifa,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
IOC ilizaliwa rasmi Juni 23, 1894 jijini Paris , Ufaransa na kila mwaka ifikapo tarehe hiyo nchi zaidi ya 200 wanachama wa kamati hiyo ya kimataifa, Tanzania ikiwamo huadhimisha siku hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za michezo.
Huadhimishwa kwa washiriki wakiwa watu wa rika na jinsia zote.
“Kwa kuwa tarehe 23.06.2011 imengukia siku ya Alhamisi ambayo ni siku ya kazi, Kamati ya Olimpiki Tanzania imeamua kitaifa kuadhimisha siku hiyo Jumapili tarehe 26.06.2011 mjini Dar es Salaam katika Uwanja wa Taifa,” ilisema barua hiyo.
No comments:
Post a Comment