Habari za Punde

*WAKATI YONDAN AKIMWAGA WINO YANGA, RAGE AIBUKA NA KUDAI 'ETI' SAINI YA YONDANI YANGA NI SAWA NA 'KUSAINI KATIKA TOILET PAPER'

BEKI wa Simba Kelvin Patrick Yondan, akionekana pichani wakati akisaini mkataba na Klabu ya Yanga, ambapo beki huyo amewaomba mashabiki wa Soka na viongozi wa Yanga kumtambua kuwa kwa sasa yeye ni mchezaji halali wa Klabu ya Yanga na kudai kuwa hajawahi kusaini mkataba mpya wowote na Simba na amesema yeye amesaini Yanga tu mkataba wa miaka miwili.

Yondan amesema Simba wanampakazia kusaini mkataba mpya''Nawataka  wapenzi wote wa soka Tanzania watambue kwamba kuanzia sasa mimi ni mchezaji halali wa Yanga''.alisema Yondan


Yondani alisema kuwa awali aliikana Yanga kwa sababu walimsainisha fomu bila kumkabidhi kitita cha fedha, lakini leo ameamua kuweka wazi maamuzi yake na kuweka wazi uwazi baada ya kukabidhiwa kitita chake cha Sh. Milioni 30 taslimu na kumalizana katika mambo yote ya mkataba.
***********************************
TAARIFA  KWA VYOMBO VYA HABARI 
Uongozi wa Klabu ya Simba Sports club, umeibuka na kusema umesikitishwa na kitendo cha Klabu ya Young Africans, kuvunja taratibu za usajili kwa kumrubuni mchezaji wake Kelvin Patric Yondani, kwa kuzungumza naye na baadaye kwa ushahidi wa picha kuonekana wakimsainisha mkataba ambao baadaye imeripotiwa na vyombo vya Habari kwamba alikuwa akisaini mkataba wa kuichezea timu hiyo ya Young Africans. 

Kwamba katika picha hiyo ameonekana mjumbe wa Young aliyejiuzuru bwana Seif Ahmed na hilo lilitoa shaka kama utaratibu huo umefanywa na klabu ya Young, lakini shaka hiyo imeondolewa pale ambapo tovuti ya Young imetangaza kumsajili mchezaji huyo wa Simba SC, lakini zaidi ya hilo picha inaonyesha fedha zikiwa zimewekwa mbele ya mchezaji jambo linaloonyesha mazingira ya kurubuniwa kwani kwa utaratibu wa kifedha, pesa nyingi kiasi hicho malipo yake yanashauriwa/yanapashwa kupitia benki. 

Mbali ya hayo picha hiyo inamuonyesha Kelvin akiwa katika jezi ya mazoezi ya timu ya Taifa na yenye logo ya Kilimanjaro na kumbukumbu zinaonyesha mkataba kati ya TBL na TFF tarehe 9/5/2012, kwa haraka haraka tukio hilo limefanyika katika kipindi chini ya mwezi mmoja ingawa taarifa za ushahidi zinaonyesha tukio hilo limetokea jana tarehe 6/6/2012.

Simba Sports Club ilipenda kuamini kwamba tukio hilo haliihusu klabu ya Young kwani bwana Seif Ahmed alishajiuzuru kutoka kwenye kamati ya Young Africans, kwani Young ni klabu kongwe na inayojua taratibu zote za usajili.

Kwamba Simba Sports Club imeshawasiliana na jopo lake la mawakili na inajiandaa kuishtaki klabu ya Young katika chombo husika cha mpira na kudai adhabu ya kutopitisha majina yote ya usajili ya Young kwa mwaka 2012/2013 na miaka mingine miwili ijayo na Simba SC ipo tiyari kufuatilia suala hili hadi katika mahakama ya mpira ya FIFA.

Kelvin Yondani ni mchezaji halali wa Simba Sc aliye na mkataba hadi 31 mei 2014 mkataba ulioongezwa tarehe 23/12/2011 kuundeleza mkataba wa awali uliokuwa unaisha tarehe 31/5/2012. Sheria za FIFA za hadhi na uhamisho wa wachezaji ziko wazi  katika kipengele cha 5 kifungu kidogo cha 2 kinasema kwamba mchezaji atasajiliwa kuichezea timu moja tu kwa wakati mmoja.

Imetolewa leo tarehe 7/6/2012.
 MH. ISMAIL ADEN RAGE (MB)
MWENYEKITI
SIMBA SPORTS CLUB

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.