Habari za Punde

*MCHEZO WA ROBO FAINALI KOMBE LA UHAI KUPIGWA KESHO

Robo Fainali za michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zitachezwa kesho (Desemba 19 mwaka huu) kwenye viwanja vya Karume na Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mtibwa Sugar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume katika mechi itakayoanza saa 2 kamili asubuhi. Nazo Azam na JKT Ruvu zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Chamazi kuanzia saa 2 kamili asubuhi.
Mechi nyingine ya robo fainali itakuwa kati ya JKT Oljoro na Simba ambayo itachezwa kuanzia saa 9 kamili alasiri kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Coastal Union na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni.
Nusu fainali ya michuano hiyo itachezwa Ijumaa ya Desemba 21 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, wakati fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu zitapigwa Jumapili ya Desemba 23 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

WAKATI HUO HUO, TWFA KUCHAGUA VIONGOZI WAPYA MOROGORO
Uchaguzi wa viongozi wapya wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) unafanyika kesho (Desemba 19 mwaka huu) kwenye hoteli ya Midlands mjini Morogoro.
Kamati ya Uchaguzi ya TWFA ikiongozwa na Mama Ombeni Zavala ndiyo itakayoendesha uchaguzi huo chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wagombea katika uchaguzi huo ni Isabela Kapera, Joan Minja na Lina Kessy wanaowania uenyekiti, Rose Kissiwa (mgombea pekee wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti), Amina Karuma na Cecilia Mkafum (wanawania ukatibu mkuu).
Wengine ni Zena Chande (mgombea pekee wa nafasi ya Mjumbe Mkutano Mkuu wa TFF) na Sophia Charles na Triphonia Temba wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TWFA.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.