*GABRIEL MOLLEL ANYAKUA TUZO MBILI
*KUIWAKILISHA SWAHILI FASHION WEEK KATIKA MAONYESHO
YA MITINDO MSUMBIJI 2012
Baada ya miezi mingi ya maandalizi, waandaji wa Swahili
Fashion Week wamefanikia kuhitimisha onyesho kubwa la mitindo na mavazi katika
nchi za Afrika mashariki na kati, tukio lilinaloendelea kuiweka tasnia ya
mitindo katika ramani ya mitindo Afrika na Duniani kiujumla.
Ikiwa na viwango vipya na vyenye ubora, waandaji
wamefanikiwa kuwa na tukio bora la mwaka na kuwaacha wahudhuriaji wakihitaji
maelezo zaidi kuhusu onyesho la 2013. Kama ilivyo ada vitu vizuri lazima viwe na
mwisho, Swahili Fashion Week 2012 ilimalizika kwa kutolewa tuzo siku ya Jumamosi
ya tarehe 8, Desemba 2012.
Tuzo
za Swahili Fashion Week 2012 zimelenga kutambua mchango wa wabunifu mbalimbali
ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya mitindo Afrika
Mashariki. Tuzo hizo zinaongeza chachu ya uvumbuzi na ubunifu katika tasnia ya
mitindo. Hii inaendana na kuifanya mitindo ya Kiswahili kujulikana duniani.
Alisema Mustafa Hassanali, Mmiliki na Muandaaji wa Swahili Fashion Week.
Swahili Fashion Week 2012, imefanyika katika Hoteli ya
Golden Tulip iliyopo jijini Dar es salaam, kuanzia tarehe 6-8 Desemba, ikiwa
tukio kubwa la Mitindo ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lililokutanisha
wabunifu zaidi ya 50 kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Mshindi wa Tuzo mbili mwaka huu, Mbunifu Mvumbuzi wa
mwaka na Mbunifu Bora wa Mwaka, Gabriel Mollel ataiwakilisha Swahili Fashion
Week katika week ya mitindo Msumbiji inayoanza Desemba 7-15. Kwa mwaka wa tano
sasa Swahili Fashion Week imefanikiwa kuendeleza uhusiano na Mozambique Fashion
Week.
“Ni faraja kuiwakilisha Tanzana na Swahili Fashion Week
katika maonyesho ya Msumbiji, kushinda tuzo mbili mwaka huu, kwangu ni matokeo
ya kujituma na ubunifu mzuri, ninatumia muda mwingi kutengeneza kazi zangu. Hii
tuzo inanipa nguvu kubwa lakini ni changamoto kwani kazi ngumu katika maisha ni
kubaki katika hadhi ile ile ambayo watu walikuamini na kukupa katika shughuli
unayoifanya” Alisema Gabriel
“Kama Swahili Fashion Week ni jambo la fahari na
kujivunia kuwa sehemu ya Mozambique Fashion Week, Gabriel Mollel hataiwakilisha
tu Swahili Fashion Week nchini Msumbiji, ila pia anaiwakilisha nchi yetu kwa
kuonyesha ubunifu na mitindo iliyotengenezwa Tanzania” Alisema Mustafa
Hassanali.
Huu
ni mwaka wa Tano sasa tangu Swahili Fashion Week ianze kushirikiana na
Mozambique Fashion Week ambapo Mustafa Hassanali alishiriki mwaka 2007 na 2008
huku Jamila Vera Swai akiwakilisha 2009, Manju Msita 2010, Robbi Morro na
Ailinda Sawe wote walienda 2011.
“Swahili Fashion Week inalengo la kutangaza, kuinua na
kutafuta masoko ya bidhaa za wabunifu wa Afrika Mashariki katika soko la Afrika
na duniani kote. Tasnia ya Mitindo afrika inaitaji kutambiliwa na kuwekwa katika
ramani ya dunia” Aliongeza Mustafa Hassanali.
Licha ya kutambua mchango wa wadau mbalimbali wa tasnia
ya mitindo Afrika Mashariki, SFW pia ilitoa nafasi kwa wabunifu vijana
wanaochipukia kuonyesha kazi zao na mitindo yao kwa mashabiki wa mitindo
waliohudhuria katika Swahili Fashion Week mwaka huu ambapo wabunifu mbalimbali
walionyesha ubunifu wao.
Wabunifu wa Swahili Fashion Week pia walipata nafasi ya
kushiriki katika semina iliyoandaliwa na USAID COMPETE kwa kushirikiana na
ORIGIN AFRIKA juu ya kutafuta masoko kwa bidhaa wanazozitengeza.
Swahili Fashion Week 2012 imedhaminiwa na Vodacom, USAID
Compete, Origin Africa, EATV, East Africa Radio, Golden Tulip Hotel. Amarula,
Precision Air, 2M Media, Global Outdoor Ltd, Vayle Springs Ltd, Eventlites,
Ultimate Security, BASATA (Baraza La Sanaa Taifa),Strut It Afrika, Ndibstyles,
PKF Tanzania, DARLING, PUSH Mobile, DarLife, Century Cinemax, Natol na 361
Degrees.
KUHUSU
SWAHILI FASHION WEEK
Swahili Fashion Week ni jukwaa kubwa la
mitindo ya mavazi la kila mwaka katika ukanda wa Afrika mashariki na kati kwa
sasa. Huu ni mwaka wa Tano sasa, ambapo Swahili Fashion Week imekuwa ni
Jukwaa la wanamitindo na watengeneza vito vya urembo kutoka katika nchi
zinazoongea Kiswahili na bara zima la Afrika kwa ujumla kuweza kuonesha vipaji,
kutangaza ubunifu wao na kukuza mtandao wa mawasiliano ya kibiashara ndani na
nje ya nchi kwa wadau wa mitindo. Hili limelenga kuhamasisha ukanda huu wa
Afrika Mashariki na Kati kwamba ubunifu wa mavazi ni njia moja wapo ya kujipatia
kipato na wakati huo huo kukuza bidhaa zinazotengenezwa Afrika ( Made in
Africa concept)
Ikiwa imeanzisha uhai na jukwaa la matumaini kwa kilinge cha mitindo
katika ukanda huu, Swahili Fashion Week Swahili Fashion week imelenga kuwa
maonyesho ya ubunifu wa mavazi linaloonekana sana Afrika na hasa kwa ajili ya
soko la kimataifa, lililoundwa, kutengenezwa na kujengwa mwaka 2008 na Mustafa
Hassanali.
Ifikapo mwaka 2013, Swahili Fashion Week ina lengo la kuwa ni tukio
litakalotokea mara mbili kwa mwaka, ambapo kwa kuanza tukio la kwanza
litafanyika nchini Kenya kama sehemu ya kwanza kisha tukio lenyewe kabisa
kufanyika baadae nchini Tanzania kama sehemu ya pili.
KUHUSU GABRIEL
MOLLEL
Gabriel Mollel ni muasisi
wa Sairiamu Community Action Foundation, ambayo ndio nembo yake ya
ubunifu, Sairiamu inamaana “Mtu anaetoa kwa mikono miwili” katika lugha ya
kimasai. Gabriel amekua akifanya kazi zake kwa mikono yake mwenyewe kwa ajili ya
jamii yake kwa da mrefu kabla hajawa na jina kubwa katika uwanda wa sanaa ya
ubunifu hapa Tanzania, ameweza kushiriki katika maonyesho mbalimbali ikiwemo
Harusi Trade Fair, Swahili Fashion Week na mengine mengi ambapo pia amekua
mshindi wa Swahili Fashion Week katika kipengele cha Mbunifu Bora
2011.
No comments:
Post a Comment