CHAMA cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinaendelea na maandalizi kwa
ajili ya Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika Desemba 21 na 22
mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani
Pwani.
Kama
tulivyosema wiki iliyopita kuwa mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wanachama
zaidi ya 100, ambao kushiriki kwao itabidi wathibitishe kwa njia ya maandishi
kwa maana ya email ili uwepo wao uweze kuthaminika.
Lakini bado
kuna mwitikio mdogo wa wanachama wanaothibitisha ushiriki wao, ambapo hadi
kufikia leo saa tano asubuhi waliothibitisha ni 22 tu, hivyo tunasisitiza
wengine wafanye hivyo haraka na tusikubali kufanya mambo kwa mazoea na mwisho wa
kuthibitisha ni Jumamosi Desemba 15, saa kumi alasiri na watakaokwama kufanya
hivyo watahesabika wamekosa sifa ya kushiriki mkutano.
Tunaomba
wanachama wote ambao wanatarajia kuhudhuria mkutano huo wathibitishe ushiriki
wao kwa Katibu Mkuu wa TASWA kwa njia ya email: mgosius@yahoo.com au taswatz@yahoo.com.
Kamati ya
Utendaji ya TASWA inaendelea na juhudi za kutafuta wadhamini kwa ajili ya
Mkutano Mkuu, ambapo kiasi cha Sh. Milioni 20 kinahitajika kufanikisha mkutano
ikiwa ni gharama mbalimbali ikiwemo chakula, malazi, usafiri kwa wanachama wa
Dar es Salaam, pamoja na usafiri na malazi kwa wanachama wanaotoka nje ya Dar es
Salaam.
Tayari wadau
watatu wamejitokeza kupiga jeki mkutano huo, ambapo Alhamisi Desemba 13 saa tano
asubuhi mgahawa wa City Sports Lounge Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto atatangaza
mdhamini mmoja ambaye tutakuwa tumemalizana naye.
Kiasi cha
fedha kinachohitajika ni kikubwa sana, hivyo bado jitihada zinaendelea kutafuta
wadhamini wengine kuhakikisha mkutano unakuwa wa mafanikio makubwa na tunaomba
wenye nia ya kushirikiana nasi wafanye hivyo.
Licha ya
wanachama pia tunatarajia katika mkutano huo pia watakuwepo wadau mbalimbali wa
TASWA wakiwemo waandishi wakongwe wa habari za michezo ambao watapewa nafasi ya
kuzungumza.
Wanachama wa
TASWA watapata fursa ya kupokea na kujadili Ripoti ya Utendaji ya chama, Mapato
na Matumizi, maendeleo ya chama na masuala mbalimbali yanayohusu waandishi wa
habari za michezo kwa ujumla.
Pia kutakuwa
na semina maalum itakayoendeshwa kwa washiriki wa mkutano huo ili wawe na uelewa
kuhusiana na ajenda ya kuinua kipato kwa wanachama ambayo itajadiliwa kwenye
mkutano huo.
Kamati ya
Utendaji ya TASWA imekubaliana iwasaidie wanachama wake waweze kujitegemea kwa
kuanzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCO’S), lakini imeamua kwanza iwaite
wataalamu wa vyama vya ushirika watoe elimu juu ya jambo hilo na kukishakuwa na
uelewa wa kutosha suala hilo lipelekwe kama ajenda kamili ya kuanzisha chama
hicho kwenye Mkutano Mkuu.
Amir
Mhando
Katibu Mkuu
TASWA
10/12/2012
No comments:
Post a Comment