Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck (kulia) akizungumza na Naibu waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene nje ya ukumbi wa bunge wakati alipofika bungeni hivi karibuni, kwa ajili ya utambulisho wa mbio za Uhuru Marathon.
*******************************
Mwandishi Wetu
MASHINDANO yambio ndefu ambayo yatajulikana kama Uhuru Marathon, yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara katika hoteli ya JB Belmonte iliyopo Mtaa wa Azikiwe, Dar es Salaam.
Uhuru Marathon inazinduliwa huku tayari mashindano hayo yakiwa yametambulishwa rasmi kwa wabunge katika bunge lililopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, katika uzinduzi huo utakaofanyika kuanzia saa 12 jioni, viongozi wa kada mbalimbali watahudhuria.
“Kila kitu kwa ajili ya uzinduzi huo kimekamilika na watakuwepo viongozi wa kada mbalimbali wakiongozwa na Dk. Fenella, tunataka kufanya kitu kikubwa zaidi kwa nchi hii,” alisema.
Mratibu huyo alisema, lengo la mbio hizo ni kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kukumbuka, kuzingatia na kuuenzi urithi waliaochiwa na viongozi waliopigania uhuru wa nchi hii.
Alisema, urithi huo ambao utakuwa ukikumbukwa kila mwaka kupitia mbio hizo ni upendo, mshikamano, umoja na amani iliyopo. Melleck anasema mbio hizo zitakuwa zikifanyika kila mwaka na zitaanza rasmi hapo mwakani.
Katika mbio hizo, zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali, zitakuwepo pia mbio za kilomita 3, kilomita 5, Half Marathon kilomita 21 pamoja na Full Marathon yenyewe itakayokuwa kilomita 42.
Mratibu huyo anasema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji ya aina mbalimbali.
“Hapa tunachotaka kufanya katika mbio za kilomita 3 ni kuwaomba kama vile viongozi maarufu wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wetu serikali ili kushiriki, kwa kudumisha amani na upendo.
“Pia tutahakikisha kama mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia watu wenye mahitaji mbalimbali na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha maarufu zaidi duniani kushiriki,” anasema.
Mratibu huyo anafafanua kuwa wamejipanga mno katika hilo ili kuhakikisha wanafanya mambo makubwa zaidi na ambayo yataleta tija kwa taifa.
Waandaaji wa mbio hizo ambao ni Kampuni ya Intellectuals Communication Ltd kwa ushirikiano na waandaji wa mbio za Berlin Marathon zilizo maarufu zaidi duniani.
No comments:
Post a Comment