Habari za Punde

*MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR, Balozi Seif Ali Iddi AZINDUA DAHALIA YA CHUO CHA KILIMO MIZIMBANI UNGUJA

 Jengo la Dakhalia ya Chuo cha Kilimo Kizimbani likionekana katika mandhari nzuri na ya kupendeza.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipanda mti kama kumbukumbu mara baada ya kuizinduai dakhalia ya Chuo cha Kilimo Kizimbani Wilaya ya Magharibi.
 Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua Dahalia ya chuo cha Kilimo kizimbani ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mkurugenzi wa Chuo cha Kilimo Kizimbani Nd. Mohd Khamis Rashid akimpatia Balozi Seif zawadi ya ndizi bora aina ya Mkono Mmoja  iliyolimwa kitaalamu chuoni hapo.
***********************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vijana pamoja na wanafunzi wa Zanzibar wana fursa nzuri ya  kupata elimu ya juu hapa hapa nchini  kutokana na kuongezeka kwa vyuo vikuu ili kupunguza gharama zisizo za lazima.
Alisema utafiti wa Kitaalamu umebainisha kwamba mwanafunzi anayepata digirii ya kwanza mfano Nchini Uingereza analazimika kulipiwa zaidi ya shilingi milionio 57,000,000/- fedha ambazo zinaweza kugharamia wanafunzi kadhaa hapa nchini wakati kiwango na ubora wa elimu kinafanana.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akiizindua Dakhalia mpya ya chuo cha Kilimo Kizimbani ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“ Tumefikia wakati Zanzibar hakuna  sababu kwa elimu ya diploma na digirii ya kwanza kufuatwa tena nchi za nje hasa tabia iliyojengeka kwa vijana kwenda Ulaya kwani tayari tumeshakuwa na vyuo vikuu vinavyotosheleza mahitaji”. Alifafanua Balozi Seif.
Aliutaka uongozi wa Chuo cha Kilimo Kizimbani kuongeza juhudi za kutoa Taaluma ili Taifa likidhi mahitaji ya Wataalamu wa Kilimo ambao hivi msasa wapo 141 wakati mahitaji ni Wataalamu 287 kukiwa na upungufu wa Wataalamu 146.
Balozi Seif alifahamisha kwamba ujenzi wa dakhalia uliofanywa na chuo cha kilimo ni mabadiliko makubwa yatakayoiwezesha Zanzibar kuwa na wataalamu wake na kuacha mfumo wa kutegemea watalaamu wa kigeni ambao wanaibebesha mzigo Serikali.
“ Nafurahi kuona chuo cha Kilimo Kizimbani kimezaa dakhalia ikiwa ni ishara ya mabadiliko na mapinduzi katika sekta ya kilimo ambayo ni tegemezi kwa Uchumi wa Taifa”. Alifafanua Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe Zanzibar.
“ Mapinduzi ya Kilimo  ni vyema yakaenda sambamba na mabadiliko ya chuo cha Kizimbani”. Aliendelea kusisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
 Amewaomba wanafunzi wa chuo hicho kujizatiti katika mafunzo yao kwa vile Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeshawaandalia mazingira bora ya kujipatia Elimu wanafunzi hao.
Alikumbusha kwamba taratibu za chuo lazima zifuatwe na wanafunzi hao katika dhana ya kudumisha nidhamu ya hali ya juu  itakayokijengea sifa nzuri chuo hicho kitaifa na Kimataifa.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd. Afan Othman Maalim alisema katika kukijengea uwezo zaidi wa kitaaluma chuo cha Kilimo  Kizimbani Wizara ya Kilimo tayari inawaandaa Walimu kumi kupata mafunzo ya ajuu kwa ajili ya kukiwezesha chuo hicho kutoa elimu ya Digirii ya kwanza.
Nd. Afan alisema hatua hiyo imelenga kuondosha tatizo la uhaba wa mabwana na mabibi shamba uliopo ambao unachangia kudumaza juhudi za wakulima katika uzalishaji wa Kilimo.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo alifahamisha kwamba mpango huo utakwenda sambamba na juhudi za serikali kupitia wizara hiyo na kwa msaada  wa  Serikali ya Norway kwa kujenga dakhalia nyengine kubwa na ya kisasa muda ufupi ujao.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa dakhalia hiyo pamoja na mikakati ya baadaye ya Chuo Mkurugenzi wa chuo cha Kilimo Kizimbani Nd. Mohd Khamis Rashid alisema ujenzi wa dakhalia hiyo yenye vyumba saba na kuhudumia wanafunzi 42 umekuja kutokana na changamoto iliyojitokeza ya ongezeko kubwa la idadi ya Vijana wanaotaka kujiunga na chuo hicho.
Alisema mbali ya wanafunzi wa chuo hicho lakini pia dakhalia hiyo itatumiwa na  wakulima wa mafunzo na muda mfupi kipindi ambacho wanafunzi wa chuo hicho watakuwa likizoni.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kuangalia maonyesho ya kazi mbali mbali zinazofanywa na wanafunzi hao likiwemo zaidi suala la utafiti wa ardhi, mazao ya kilimo na mifugo.
Walimu wa chuo cha Kilimo Kizimbani wakiongozwa na mwalimu wa mazao katika chuo hicho Bwana Foum Ali Garu alimueleza Balozi Seif juhudi zinazochukuliwa na chuo hicho katika kuwajengea uwezo wa kitaalamu wanafunzi hao katika kufanya utafiti kwa vitendo.
Dakhalia hiyo ya chuo cha Kilimo Kizimbani  imegharimu jumla ya shilingi Milioni 399,000,000/- na kugharamiwa na Mfuko wa Kimataifa wa kuendeleza Kilimo { IFAD }.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/1/2013.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.