Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi.
Zawadi Msalla (kulia) akisistiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)
wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu kusitishwa kwa wimbo wa Msanii Snura Mushi ujulikanao kwa jina
la Chura kwa kukiuka maadili.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimfuatilia kwa makini Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi.
Zawadi Msalla (hayupo pichani) wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu kusitishwa kwa wimbo wa Msanii Snura Mushi ujulikanao kwa jina
la Chura kwa kukiuka maadili.
*********************************************
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali imesitisha wimbo na Video ya
Muziki wa Chura wa Msanii Snura Mushi
kuchezwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuanzia leo mpaka pale
msanii huyo atakapoifanyia marekebisho
video ya wimbo huo.
Usitishwaji huo umetokana na maudhui
ya utengenezwaji wa Video hiyo ambayo haiendani na maadili ya Mtanzania.
Pia Serikali imesitisha maonyesho yote
ya hadhara ya mwanamziki huyo mpaka pale atakapo kamilisha taratibu za usajili
wa kazi zake za Sanaa katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Serikali inawataka wasanii kujiuliza
mara mbili kabla ya kubuni kazi zao za Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na
marafiki zao watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale wanaowadhalilisha, Waelewe
kwamba Sanaa si uwanja wa kudhalilisha
watu hata kidogo..
Aidha Serikali imechukizwa na kazi
hiyo ambayo si tu inadhalilisha tasnia ya Muziki bali inadhalilisha utu wa
mwanamke na inaifanya jamii kuanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya
Sanaa kwa ujumla.
Serikali inawakumbusha wananchi wote
kutokujiingiza katika makosa ya sheria ya mtandao kwa kusambaza wimbo huu kwa
njia yoyote ile ya kimtandao
Pia inavitaka Vyombo vya habari viwe
vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya Sanaa kabla ya kuwa mawakala wa
uharibifu wa jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa.
Serikali inatoa wito kwa wasanii wote
kuzingatia maadili ya Kitanzania kabla ya kutoa kazi zao kwani haitawavumilia
‘wasanii’ wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa kuwa sehemu ya
uvunjifu wa maadili.
Imetolewa na Zawadi Msalla
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini


No comments:
Post a Comment