Wahitimu
wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari WAMA- Nakayama wakionyesha maonyesho ya
masomo kwa Mgeni Rasmi, Mhe. Ummy Mwalimu, Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma
Kikwete pamoja na wageni waalikwa.
Wahitimu
wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya WAMA -Nakayama katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa WAMA
mara baada ya kumkabidhi Cheti cha Shukrani
kwa mchango wake katika maendeleo ya elimu yao.
******************************
Mhe. Ummy Mwalimu aelezea Mikakati
ya Serikali katika kuhakikisha Usawa wa Kijinsia Katika Elimu - Mahafali ya
Kwanza ya Kidato cha Sita Shule ya Sekondari WAMA Nakayama
Na Philomena Marijani, WAMA Foundation
Serikali imechukua
hatua maalum za kisera na kimipango
kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia katika elimu, mafunzo,
sayansi na teknolojia. Maelezo hayo yametolewa na Mhe.Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati
wa sherehe za Mahafali ya kwanza ya Kidato cha Sita ya Shule ya Sekondari ya
WAMA- Nakayama yaliyofanyika mwishoni wa wiki katika ofisi za WAMA zilizopo Kawe,
Dar es Salaam.
Mhe.Ummy Mwalimu ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo amesema moja ya hatua hizo ni pamoja na
kuongeza idadi ya wasichana wanaopata
elimu ya msingi ili kuwepo na idadi sawa ya wavulana na wasichana.
Aliongeza kuwa
kwa mwaka 2008 serikali ilifanyia
marekebisho Sheria ya Elimu na mafunzo ili kukidhi matakwa ya usawa wa
kijinsia. “Baadhi ya maswala ambayo yamerekebishwa ili kuboresha mazingira
ya shule yaweze kuwa rafiki kwa wasichana ni pamoja na kuhamasisha jamii
kutoa chakula shuleni, kujenga mabweni na vyoo kwa ajili ya wasichana na pia kuongeza
idadi ya walimu. Wizara yangu pia
imeandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na Sheria ya Mtoto No.21 ya
mwaka 2009 ambayo inasisitiza jamii kuzingatia utoaji wa haki za msingi kwa watoto,
moja ya haki hizo ni haki ya kuendelezwa.” Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Mhe. Mwalimu
aliwashauri wahitimu wa WAMA-Nakayama wasiridhike
na elimu ya kidato cha sita bali
wajiendeleze kwa kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini na hatimaye serikali ipate viongozi wengi
wanawake.
Akiongea katika sherehe
za mahafali hayo Mke wa Rais Mstaafu na
Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete
alisema Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama ilianzishwa ili kutoa mchango katika Juhudi za Taifa za kumkomboa mwanamke kwa kuwapatia fursa za elimu bora ya sekondari watoto wa kike wanaotoka
katika mazingira magumu wakiwemo yatima.
“Taasisi inatambua kwamba ili
mtoto wa kike aweze kupata mafanikio katika masomo yake ni muhimu kumjengea
mazingira wezeshi ya kusomea na kuishi. Ndiyo maana tuliamua kuwajengea shule
yenye mahitaji yote ya kupata elimu bora na pia kuepuka vishawishi mbalimbali
vinavyoweza kupelekea kukatisha masomo. Alisema Mama Kikwete.
Mama Kikwete
aliwashukuru wadau wote ambao wamekuwa
wakitoa misaada mbalimbali tangu kuanzishwa kwa shule ya WAMA- Nakayama na
kusema ushirikiano huo umesaidia kufanikisha ndoto ya kuwasaidia watoto wa
kike na matunda yake yanaonekana kwa
wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita.
Akisoma hotuba yake Kaimu
wa Balozi wa Japan hapa nchini,Bw. Hiroyuki KUBOTA alisema shule hii iliweza
kuanzishwa kwa msaada kutoka kwa Bw.
Nakayama wa Japan ambaye alichangia hela za ujenzi wa shule. Aliongeza kuwa Ubalozi wa Japan hapa nchini umekuwa
ukisaidia shule katika masuala mbalimbali ikiwemo maboresho ya sick- bay,
maabara, na kwa sasa ubalozi unasaidia upanuzi wa jengo la utawala ambao
utamalizika baada ya muda mfupi.
Shule ya Sekondari ya
WAMA- Nakayama iliyopo Nyamisati, Rufiji
katika Mkoa wa Pwani ilianza rasmi mwaka 2010. Shule inasaidia wasichana yatima
na waliotoka katika mazingira hatarishi kutoka mikoa yote Tanzania bara na
visiwani. Jumla ya wanafunzi wa kike 27 watamaliza kidato cha sita mwezi mei
mwaka huu katika michepuo ya ECA na PCB.
No comments:
Post a Comment