Habari za Punde

*BUNGE LAPITISHA MUSWADA WA SHERIA YA KUANZISHWA KWA MAHAKAMA YA MAFISADI

Na: Lilian lundo – MAELEZO – Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2016 ikiwemo kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi.
Muswada huo umewasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju ambao ulikuwa na marekebisho ya sheria tano ambazo ni sheria ya mamlaka za Mahakama ya Rufaa, sheria ya Makosa ya Uhujumi Uchumi, sheria ya usimamiaji haki na matumizi ya sheria, sheria ya mahakama za mahakimu pamoja na sheria ya rufaa za kodi.
“Ili kutekeleza ahadi ya Serikali ya kuanzishwa Mahakama Maalum kwa ajili ya kushughulikia makosa ya rushwa (ufisadi) na uhujumu uchumi, imeonekana kuwa kuna umuhimu wa kurekebisha sheria hii kwa kuanzishwa  Divisheni Maalum ya Mahakama Kuu ambayo itakuwa na Majaji pamoja na watumishi wengine ambao wanahusika moja kwa moja na kesi za rushwa na uhujumu uchumi tu,” alifafanua Mhe. Masaju.
Mwanasheria Mkuu aliendelea kwa kusema kuwa, makosa yatakayofunguliwa katika mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ni yale ambayo thamani yake haipungui shilingi bilioni moja, lengo la kuweka ukomo huo kwa baadhi ya makosa ni kuiwezesha Divisheni hiyo kusikiliza makosa makubwa ya rushwa na uhujumu uchumi na kuacha makosa madogo yasiyofikia thamani hiyo kuendelea kusikilizwa mahakama za wilaya, hakimu mkazi au mahakama kuu.
Aidha, marekebisho mengine yanayopendekeza katika sheria hiyo ni pamoja na kuboresha masharti ya kutoa dhamana pale kosa linapohusisha fedha au mali ambayo thamani yake inazidi shilingi milioni kumi ambapo sheria ya sasa  inaeleza kuwa masharti ya dhamana kwa kosa kama hilo ni kutoa fedha tasilimu (cash deposit) inayolingana na nusu ya thamani ya mali ya kosa husika na thamani ya nusu inayobaki itolewe kwa njia ya bond.
Muswada unapendekeza kwamba masharti yaboreshwe ili pale mshtakiwa anapokuwa hana fedha inayotakiwa mahakamani basi aruhusiwe kutoa mali hiyo na kama mali hiyo haihamishiki basi hati au ushahidi unaothibitisha umiliki wa mali hiyo utolewe Mahakamani.
Marekebisho mengine ni pamoja na adhabu kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi iwe ni kifungo gerezani kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.