Habari za Punde

*CCM ANZNIBAR WALAANI PROPAGANDA CHAFU ZINAZOTOLEWA NA MAALIM SEIF DHIDI YA SERIKALI YA MAPINDUZI

TAARIFA YA CCM ZANZIBAR KWA VYOMBO VYA HABARI ILIYOTOLEWA NA AFISI KUU YA CCM ZANZIBAR KUHUSIANA NA PROPAGANDA CHAFU ZINAZOTOLEWA NA KATIBU MKUU WA CUF MAALIM SEIF SHARIF HAMAD DHIDI YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR NA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kinatoa indhari kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusiana na Propaganda chafu, za uongo na upotoshaji zinazoendelea kusambazwa na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ndani na nje ya nchi dhidi ya Serikali mbili zilizoko madarakani chini ya Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake.
CCM Zanzibar tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa marejeo imekuwa ikishuhudia matukio mbali mbali ya hujuma ambazo chanzo chake ni kauli za uchochezi, uongo na upotoshaji zilizotolewa hadharani na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad katika ziara zake kwenye maeneo tofauti Unguja, Pemba na nje ya Zanzibar.
Wana-CCM, viongozi na wananchi wa Zanzibar wameshuhudia kuchomwa kwa mashamba ya mikarafuu, kuharibiwa mazao ya wakulima, watu hasa wanachama na wafuasi wa CCM kuchomewa nyumba zao, kuitishwa migomo, wananchi kushawishiwa kutoitambua serikali halali iliyoko madarakani pamoja na matukio kadhaa yenye kuashiria uvunjifu wa amani na uhujumu wa uchumi wa nchi.
Jumatano ya tarehe 15 Juni, 2016, Katibu Mkuu wa CUF kupitia televisheni ya “Voice of America” (VOA), alionekana hadharani akishutumu Serikali za Tanzania na viongozi wake waliopo na walioondoka madarakani kwa madai tofauti ya uongo ikiwemo kile alichodai kukosa uwajibikaji na ukiukwaji wa makusudi wa misingi ya utawala wa sheria.
Kwa maoni ya CCM Zanzibar, jitihada za Maalim Seif hazina lengo la kutaka kurejewa uchaguzi wa Zanzibar ambao umefanywa kwa mujibu wa sheria za nchi, bali zinalenga kujitafutia umaarufu alioupoteza kutokana na ubinafsi wake wa kuwakataza wafuasi wake kushiriki uchaguzi wa marudio, jambo ambalo limewanyima fursa muhimu kisiasa ya kutoa hoja za kisheria kupitia chombo rasmi cha kutunga sheria – Baraza la Wawakilishi.
Chama cha Mapinduzi Zanzibar kwa mara nyengine tena kinatoa wito kwa Serikali zote mbili na vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kuvifumbia macho vitendo vinavyoendelea kufanywa na kiongozi huyo wa upinzani, kwani athari za baadae za matukio hayo zinaweza kuwa kubwa kiuchumi, kisiasa, kijamii na bila ya shaka kwa mustakbali wa maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Aidha, vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya watu wanaopatikana na hatia kuhusiana na matukio hayo, vyenginevyo waliowengi wataamini kwamba hakuna kinachofanyika licha ya hujuma na matukio mengi yanayoendelea kufanywa na hivyo kuamini kwamba wapo baadhi ya raia ambao wao wapo juu ya sheria.
Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinajivunia hali ya amani na utulivu ambayo imetawala nchini tokea kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, hadi kumalizika kwa uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 ambao ulikamilisha ushindi wa CCM kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunapongeza uteuzi wa viongozi waliounda Serikali pamoja na juhudi za Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi kero mbali mbali zinazowakabili wananchi kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015 – 2020. Kadhalika tunapongeza hoja mbali mbali zinazotolewa na wajumbe wa CCM kwenye kikao kinachoendelea cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi.
CCM inawaomba wananchi kutobabaishwa na kauli za uchochezi na uasi zinazotolewa na Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kuna kila dalili zinazoonesha kuwa yeye na Chama chake wameshapoteza mwelekeo wa kisiasa na badala yake wanatafuta mwelekeo mwengine ambao kamwe haukubaliki nchini Tanzania ambako hakuna historia ya vita wala matukio ya uasi.
Chama Cha Mapinduzi kinawasisitiza wananchi kwamba hakuna uchaguzi mwengine utakaofanyika kabla ya mwaka 2020 na hakuna Serikali nyengine itakayekwa madarakani kwa kile kinachodaiwa kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.