SHIRIKISHO la Soka Barani Afrika (CAF) limeweka ngumu kwa beki mpya wa Yanga Hassan Kessy kuanza kuitumikia timu hiyo katika mchezo wa kesho dhidi ya Bajaia baada ya kuomba barua ya Kessy kuruhusiwa na klabu yake ya zamani, Simba SC kuhamia Yanga,jambo linaloonekana kukwamishwa na Klabu ya Simba walioonekana kuchelewa kutoa barua hiyo.
''Hatutamtumia Kessy katika mchezo wa kesho, ukweli ni kwamba simba wameamua kuweka mtimanyongo tu wa kutoa release letter, kwani mkataba wa Kessy, kwa mujibu wa kumalizika kwake ni mpaka ile tarehe ya kwenye contract inapoishia ndio mkataba unaisha rasmi.'' alisema Msemaji wa Yanga Jerry Muro
Mkataba wa Kessy unamalizika mwezi huu na ili aanze kuichezea Yanga anatakiwa kuwa na barua ya kuruhusiwa na Klabu yake ya zamani Simba.
Baada ya Simba kupata taarifa hizo mmoja wa Viongozi alisema kuwa TFF iliwaomba kuandika barua hiyo ili Kessy aweze kuruhusiwa kucheza kesho lakini ugumu ukawa ni taarifa zenyewe kuwafikia kwa ghafla na siku ambayo si ya kazi.
“TFF wanatuomba tuwe waungwana tuandike hiyo barua ili huyo kijana acheze kesho, sasa bahati mbaya wanatuambia Jumamosi jioni na kila mtu amepumzika nyumbani kwake, ofisi zimefungwa,”amesema kiongozi mmoja wa Simba, ambaye hakutaka kutajwa jina.
“Wavute subira, Jumatatu siyo mbali, tutalifanyia kazi hilo suala, ila kwa leo au kesho kulifanyia kazi hilo suala ni vigumu,” aliongeza.
Yanga itamenyana na Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine katika mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika mjini Bejaia kesho.
Na kocha Pluijm alimtegemea Kessy kuziba pengo la majeruhi Juma Abdul, ambaye amebaki Dar es Salaam na sasa atakuwa hana namna nyingine zaidi ya kumpanga Mbuyu Twite beki ya kulia.
WAKATI HUO HUO:
KIUNGO Mshambuliaji Obrey Cholla Chirwa aliyemwaga wino jana ameondoka alfajiri ya leo kuelekea Algeria kuungana na timu yake mpya Yanga SC iliyopo nchini Algeria.
Baada ya kukamilisha usajili wake tayari klabu ya Yanga imetuma CAF jina la mchezaji huyo ili kupata leseni yake, ni mategemeo kuwa leseni ya Chirwa itafika jioni ya leo, ili na yeye kama atahitajika katika mchezo huo aweze kuruhusiwa kucheza,
Mzambia huyo anayechezea timu ya taifa ya Zambia chini ya miaka 23 kwa mara nyingine ataonana na pacha wake wa zamani katika safu ya ushambuliaji ya FC Platinum Donald Dombo Ngoma.
No comments:
Post a Comment