WIZARA YA FEDHA NA
MIPANGO
UFAFANUZI
WA HOJA ZA WAHESHIMIWA
WABUNGE
AKICHANGIA HOTUBA ZA WAZIRI WA
FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA
BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI 2015 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2016/17
PAMOJA NA BAJETI KUU YA SERIKALI KWA MWAKA 2016/17
JUNI 20, 2016
DODOMA
A.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa
hii kukushukuru wewe binafsi, Naibu
Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri majadiliano kuhusu Taarifa ya Hali
ya Uchumi wa Taifa 2015 na Mpango wa Maendeleo wa 2016/17 pamoja na Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2016/17, niliyowasilisha tarehe 8
Juni, 2016.
2.
Mheshimiwa
Spika, Kipekee, ninampongeza sana Mhe. Naibu Spika kwa
umahiri na weledi wa hali ya juu alioonesha katika kusimamia Kanuni za Bunge
wakati wote wa kikao hiki cha Bunge la bajeti. Hakika viwango vyake ni vya
kimataifa. Japokuwa Mhe. Joseph Kakunda, mwanafunzi wangu Idara ya Uchumi Chuo
Kikuu cha Dar-es-Salaam alichomekea sehemu fulani akidai kwamba mimi ni bahiri,
(nadhani alimaanisha bahiri wa kutoa maksi za upendeleo!), nataka niliambie Bunge lako tukufu kwamba kwa
viwango ambavyo Mhe. Naibu Spika alivyoonesha humu ndani, hakika ningempa maksi
za haki asilimia 100 kama walivyofanya maprofesa wake wa sheria UD na UCT.
Hongera sana.
KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
3.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutambua
michango iliyotolewa na: Kamati ya Bajeti, chini ya M/kiti wake Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; Mheshimiwa David Ernest Silinde,
Mbunge wa Momba, Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu
Wizara ya Fedha na Mipango, na waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa
kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni. Ninawashukuru wote.
4.
Mheshimiwa
Spika, jumla ya Wabunge 158
wamechangia hoja niliyowasilisha. Kati ya hao, 133 wamechangia kwa kuzungumza
na 25 kwa maandishi.
B: HATUA ZILIZOPONGEZWA NA WABUNGE WENGI
5.
Mheshimiwa
Spika, Hatua zilizopongezwa na Wabunge wengi wakati wa mjadala juu ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali 2016/17 ni pamoja na zifuatazo:
·
Kuthubutu
kutenga asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo,
ikiwa pamoja na kuanza ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard
gauge, barabara, umeme, ununuzi wa meli mpya ziwa Victoria na ndege tatu za
abiria;
·
Kuongeza
ukusanyaji wa kodi na mapato yasiyo ya kodi hadi kufikia wastani wa shilingi
1.2 trilioni kwa mwezi kwa kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuimarisha
matumizi ya vifaa vya kielektroniki (EFDs) katika ukusanyaji wa mapato, na
Hazina kutoa fedha hizo kama ilivyopangwa;
·
Kusimamia
nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ikiwa pamoja na
safari za nje, posho, sherehe, kuondoa watumishi hewa katika utumishi wa umma;
·
Kuhimiza
azma ya kufanya kazi na kurejesha nidhamu ya watumishi kazini kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa;
·
Kuwapunguzia
wafanyakazi mzigo wa PAYE na SDL kwa waajiri;
·
Kuanzisha
mahakama ya kushughulikia mafisadi;
·
Kuweka
kipaumbele katika kufufua na kujenga viwanda ili kupanua fursa za ajira na wigo
wa kodi; na
·
Kujielekeza
kutekeleza Ilani ya CCM 2015, ahadi za viongozi wakuu na Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 ili kutatua kero za wananchi, hasa masikini.
C: USHAURI
ULIOTOLEWA NA WABUNGE WENGI
6.
Mheshimiwa
Spika, Wabunge wengi pia
walitoa ushauri katika maeneo mbalimbali, ili yazingatiwe katika bajeti hii au
bajeti zijazo. Naomba kurejea ushauri muhimu uliotolewa na Wabunge kama
ifuatavyo:
·
Kuongeza
tozo kwenye mafuta ili mapato hayo yatumike kupanua huduma za maji na na
kukamilisha vituo vya afya na zahanati vijijini;
·
Kuboresha
mfumo wa kodi ikiwa pamoja na kufuta kodi, ushuru na tozo za kero kwa wakulima,
wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa/ wawekezaji, lakini
pia kutoa ahueni ya kodi kwenye taulo za akinamama na vifaa vya watu wenye
ulemavu, vifaa vya michezo, zana za uvuvi, na kulinda viwanda vya ndani;
·
Kuchukua
hatua za ziada kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuongeza kilimo
cha umwagiliaji, pembejeo, ugani, utafiti, mnyororo wa thamani, masoko, ruzuku,
mikopo na bajeti ya kilimo;
·
Kuimarisha
utalii kwa kuzingatia fursa za kipekee za Tanzania katika sekta hii;
·
Kuchukua
hatua madhubuti kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi;
·
Shilingi
milioni 50 zilizoahidiwa kwa kila kijiji ziwekewe utaratibu mzuri na endelevu;
·
Kuongeza
kasi ya kulipa madeni ya ndani (watumishi, wastaafu, wakulima, watoa huduma
& makandarasi);
·
Kuimarisha
elimu na kuhakikisha inaendana na mahitaji ya wataalam wa Tanzania ya leo na
kesho;
·
Kupanua
wigo wa kodi hususan katika sekta zenye mapato makubwa kama mawasiliano,
madini, maliasili na ardhi, na sekta nyingine zenye fursa kama uvuvi na
biashara kwenda nchi jirani, e-commerce, gawio kutoka katika mashirika ya umma,
sambamba na kuhakikisha kila mwananchi analipa kodi stahiki ili kuchangia
maendeleo ya Taifa na kupunguza utegemezi;
Kupambana
na uvujaji wa mapato hususan katika biashara ya mafuta, miamala ya
kielektroniki, transfer pricing na misinvoicing, misamaha ya kodi, wizi na
udanganyifu katika ukadiriaji wa kodi, maduka ya jumla, n.k.
·
Kuimarisha
ushirikishwaji wa wadau ikiwa ni pamoja na Bunge, katika maandalizi ya mipango
na bajeti ya Serikali;
·
Kuendeleza
utulivu wa uchumi ikiwa pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei, kuongezeka kwa kasi
deni la Taifa, kushuka kwa thamani ya shilingi, matumizi ya dola sambamba na
shilingi (dollarisation), kupanua huduma za kibenki hadi vijijini na kupunguza
riba;
·
Kuboresha
sheria mbalimbali ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara
nchini;
·
Kuchukua
tahadhari katika kufanya mageuzi katika mfumo wa kodi na tozo nchini ili
kuepuka kudhoofisha halmashauri na utekelezaji wa dhana ya (ugatuaji madaraka D
by D);
·
Kutoa
msukumo zaidi kwa ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya
kipaumbele, ikiwa pamoja na PPP;
·
Kuanzisha
duka la kununua madini kutoka kwa wafanya biashara wadogo kutoka nchi jirani na
kutoza kodi ya asilimia moja
·
Kuandaa
mikakati mahsusi kwa ajili ya kukabiliana na umasikini katika mikoa masikini
zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia upya uwiano katika mgawanyo wa fedha na
rasilimali nyingine za umma; na
·
Kuongeza
bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili kuiwezesha kufanya kazi zake kwa
ufanisi;
D: UFAFANUZI WA BAADHI YA HOJA
7.
Mheshimiwa
Spika, zipo hoja zilizotolewa
na Kamati ya Bajeti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kurudiwa na Waheshimiwa
Wabunge wengi, ambazo baadhi yake napenda kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo:
Hoja Na. 1: Pendekezo la
kuongeza Tozo ya shilingi 50 kwenye mafuta kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa maji
na kukamilisha
ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini
Ufafanuzi:
·
Mheshimiwa Spika,
hili ni pendekezo lenye lengo zuri na Serikali inalipokea. Hata hivyo, ni vema
kutambua kwamba kufuatia kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia,
gharama ya mafuta yote yaliyoagizwa kutoka nje imepungua (kwa takriban 20%) na
kuchangia kushuka kwa mfumuko wa bei (sasa umefikia 5.2%). Mwenendo huu hakika
umeleta ahueni kwa wananchi wetu wengi. Hivyo, kwa sasa Serikali imeamua
kutoongeza tozo kwenye mafuta ili wananchi waendelee kunufaika na unafuu huo wa
bei ya mafuta. Ni dhahiri kuwa ongezeko la tozo katika mafuta ya petroli na dizeli litasabisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini
jambo ambalo litaongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa
chakula na bidhaa kama vifaa vya ujenzi na huduma nyingine.
·
Aidha, wataalam wa uchumi wanashauri kuwa
kipindi kama hiki cha uwepo wa bei ndogo ya mafuta ni fursa nzuri kwa nchi
kuwekeza, hususan katika ujenzi wa miundombinu, viwanda (energy-intensive
sectors) na kuendeleza ujuzi na teknolojia. Ndiyo sababu Serikali inaona kuwa
ni busara Zaidi badala ya kuongeza tozo kwenye mafuta, tujielekeze kuongeza
bajeti ya kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji, nishati na
elimu sambamba na kutumia fedha zilizopangwa kwa ufanisi Zaidi.
·
Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa
kuboresha huduma ya maji nchini, ambayo ni ahadi ya muhimu katika Ilani ya CCM,
bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2016/17 fedha za
ndani zimeongezwa kwa asilimia 85 kutoka shilingi bilioni 373.01 mwaka 2015/16
hadi Shilingi bilioni 690.16 mwaka ujao wa fedha 2016/17. Kufuatia jitihada
kubwa zinazoendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato, Serikali itahakikisha fedha
hizi zinapatikana na kutolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji
vijijini kama ilivyokusudiwa. Aidha, kwa upande wa haja ya kukamilisha ujenzi
wa zahanati vijijini na vituo vya afya katika kata, Wizara ya afya inajipanga
kufanya kwanza tathmini ya majengo hayo katika mwaka 2016/17 kwa ajili ya
utekelezaji 2017/18.
Hoja Na. 2: Pendekezo la
kuondoa msamaha wa kodi ya Mapato kwenye kiinua mgongo cha Waheshimiwa Wabunge.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Kwa
mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kodi ya mapato hutozwa kwenye
vyanzo vyote vya mapato (global income);
Kiinua
mgongo ni chanzo kimojawapo cha mapato kinachotambuliwa na Sheria na hutozwa
kodi;
·
Kupitia
Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Mapato, kiinua mgongo kinacholipwa kwa
wabunge wakati wanamaliza muhula wa miaka mitano kimesamehewa kodi;
·
Msamaha
huu hauzingatii kanuni ya usawa ya utozwaji kodi, kwani watu wengine wote
wanaopata malipo ya kiinua mgongo, iwe katika sekta binafsi au utumishi wa
umma, hutozwa kodi katika mapato hayo. Kwa hiyo, hatua hii imechukuliwa ili
kujenga misingi ya usawa na haki katika ulipaji wa kodi; na
·
Lengo la kufanya marekebisho hayo sasa ni kwa ajili ya kuweka utaratibu wa
kisheria ambao utatumika kukokotoa stahili za Mbunge endapo ukomo wa Mbunge
yeyote utatokea katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 na kuendelea. Aidha, mabadiliko haya yanafanyika sasa ili kuzingatia
msingi wa utozaji kodi ambao inataka kodi iwe inatabirika (predictability
principle).
·
Mheshimiwa
Spika, Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba siku nilipowasilisha pendekezo
hili kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, aliridhia mara moja na kusisitiza kwamba kulipa kodi ni wajibu wa
Watanzania wote ili tujenge nchi yetu. Na kwa kuwa kiongozi lazima aongoze kwa
mfano alielekeza kuwa yeye ni Mbunge wa Tanzania nzima na anapenda awe wa
kwanza kukatwa kodi stahiki kwenye mafao yake ya kustaafu!
·
Hivyo,
napenda kufafanua kwamba marekebisho niliyowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu
tarehe 8 Juni 2016 katika hotuba yangu ya Mapendekezo ya Serikali Kuhusu
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2016/17 maana yake ni kuwa
kiinua mgongo cha viongozi wote wa kisiasa waliotajwa kusamehewa kodi chini ya
Sheria ya Mafao ya Viongozi wa kisiasa (The Political Service Retirement
Benefits Act 1995) sasa kitakatwa kodi! Hivyo, kiinua mgongo cha Mhe. Samia
Suluhu Hassan Makamu wa Rais, kitakatwa kodi! Mhe. Kassim M. Majaliwa, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ruangwa naye atakatwa
kodi! Vivyo hivyo, Mhe. Spika na Naibu Spika watakatwa kodi! Aidha, Mawaziri
(wakianza na Waziri wa Fedha) na Naibu Mawaziri wote sisi ni wabunge, hivyo
kiinua mgongo chetu kitakatwa kodi! Wakuu wa Mikoa na Wilaya kadhalika kiinua
mgongo chao kitakatwa kodi!! Mabadiliko haya ni kwa mujibu wa kifungu 10(3) cha
Sheria ya Kodi ya Mapato ambacho kimeweka sharti la kutotambua misamaha mingine
yoyote ya kodi ya mapato ambayo haijatolewa kwa mujibu wa sheria hii.
Hoja Na.3: Ofisi ya Taifa
ya Ukaguzi (NAO) ametengewa fedha kidogo sana kuweza kutekeleza majukumu yake
ipasavyo. Hivyo, bajeti ya ofisi hiyo
iongezwe.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Ukomo
wa bajeti ya matumizi mengineyo (OC) uliotengwa kwa mafungu mbalimbali
umezingatia maamuzi na mkakati wa Serikali wa kupunguza matumizi ya kawaida na
kuelekeza fedha nyingi katika bajeti ya miradi ya maendeleo;
·
Katika
kufikia ukomo wa matumizi mengineyo kwa Serikali nzima (Wizara, Idara, Taasisi
za Kiserikali, Mikoa na Halmashauri) uchambuzi wa kina ulifanyika kubaini
mahitaji ya fedha ambayo siyo ya lazima kwa wakati huu na hivyo hayawezi
kuathiri utendaji wa taasisi husika. Miongoni mwa mahitaji yaliyopunguzwa ni:
gharama za kumbi za mikutano, mafunzo na safari nje zisizo za lazima,
maadhimisho na sherehe, posho na kudhibiti matumizi ya magari kwa mafungu yote.
Aidha Serikali iliangalia miradi ambayo inaweza kutekelezwa kwa awamu;
Hata
hivyo, Serikali inatambua umuhimu na majukumu ya msingi ya Ofisi ya Taifa ya
Ukaguzi, kama ilivyo kwa taasisi nyingine nyeti, ikiwemo vyombo vya ulinzi na
usalama, mihimili mingine ya Dola na uwezo wa kukabiliana na dharura. Hivyo,
endapo kutajitokeza mahitaji ya lazima ambayo yatakwama kutekelezwa na ofisi ya
CAG kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali itahakikisha mahitaji hayo
yanazingatiwa wakati wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu
mwaka.
Hoja Na.4: Ushuru wa
bidhaa kutozwa kwenye ada ya miamala ya uhawilishaji wa fedha utaathiri
mtumiaji wa mwisho na si makampuni ya simu
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa katika
miamala ya fedha (Excise Duty on Money Transfer) hautakatwa kwenye fedha
zinazotumwa au kupokelewa, bali katika ada inayotozwa na benki au kampuni ya
simu;
·
Kwa sasa Sheria inatamka kwamba ada hii
itatozwa katika kutuma fedha tu. Hata
hivyo, baadhi ya kampuni za simu na benki zimekuwa zikitumia mwanya wa Sheria
hiyo kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea tu;
·
Kwa
mapendekezo haya, ushuru wa bidhaa utatozwa kwenye ada ya miamala ya
uhawilishaji fedha ama wakati wa kutuma au kupokea fedha au vyote viwili kadri
itakavyotozwa; na
·
Mantiki
yake ni kuwa, ushuru huu utalipwa na benki au kampuni ya simu na siyo mtumaji
au mpokeaji. Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), itawajibika kuhakikisha kwamba tozo hiyo inaendana na
uhalisia wa huduma itolewayo na kufanya ukaguzi (cyber forensic audit) wa
miamala ya makampuni ya simu kabla na baada ya tozo ili yasihamishie mzigo kwa
mtumiaji wa mwisho.
Hoja Na. 5 Tathmini ya hali ya umasikini kimkoa
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Viashiria
vya kupima hali ya umaskini nchini
hupatikana kwa kutumia Utafiti wa Mapato na Matumizi katika kaya ambao
hufanyika kila baada ya miaka mitano hapa Nchini. Utafiti wa mwisho ulifanyika
mwaka 2011/12.
·
Mheshimiwa Spika,
i.
Hali
ya umaskini katika kaya hupimwa kwa kuangalia mahitaji ya msingi (basic needs)
kwa kila mwanakaya ukijumuisha mahitaji ya chakula yenye kiwango cha kilo
kalori 2,200 kwa mlo kwa siku na hii ni kutokana na Kipimo cha Shirika la Afya
Duniani - WHO. Mbinu hii inaonesha kiwango cha chini kabisa cha kipato
anachohitaji mtu kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbali mbali ya msingi.
ii.
Kiwango
cha umaskini wa chakula hupimwa kwa gharama ya kiwango cha chini cha aina mbali
mbali ya vyakula vyenye kufikia kiwango cha kilo kalori 2,200 kinachohitajika
kwa mlo wa mtu maskini kwa siku katika mwezi. Kwa utafiti huu gharama ya
kununulia chakula cha mtu mmoja kwa siku bila kujali eneo alilotoka ni
Shillingi 858. Kiwango cha umaskini wa chakula ni gharama ya matumizi yote ya kaya
ambayo yapo chini ya gharama wanayohitaji ili kukidhi mahitaji ya chakula yaani
(Food Poverty Line). Na kwa umaskini wa mahitaji ya msingi ambao huhusisha
chakula ni Tshs. 1,216 (Basis Needs poverty line) kwa siku kwa kila mtu mmoja
tu.
Mheshimiwa Spika, utafiti
wa kukusanya taarifa za kupima hali ya umasikini nchini hukusanya matumizi na
mapato ya kaya. Taarifa zinazokusanywa
ni umri, hali ya ndoa, elimu na afya, manunuzi na matumizi ya kaya, umiliki wa
bidhaa za matumizi na mali, makazi na vifaa vya ujenzi, upatikanaji wa huduma
na vifaa, shughuli za ajira na kiuchumi, utalii na shughuli za kilimo. Uchambuzi wa kina wa hali ya umaskini katika ngazi ya mkoa
na wilaya yaani (Poverty Mapping) uliongozwa na wataalam wa REPOA na
ulibainisha kuwa:
Region
|
Watu Wanaoishi Chini Mstari wa
Umaskin 2000/01 (%)
|
Watu Wanaoishi Chini Mstari wa
Umaskini 2011/12 (%)
|
Mwanza
|
43
|
35
|
Kagera
|
29
|
39
|
Kigoma
|
38
|
49
|
Singida
|
49
|
38
|
Geita
|
Included in Mwanza
|
44
|
·
Mheshimiwa Spika, sababu zinazoeleza
kwanini kiwango cha umasikini katika Mikoa kama Mwanza, Kigoma, Singida, Geita,
na Kagera ni kikubwa zaidi ukilinganisha na mikoa ya Lindi na Mtwara ni nyingi.
·
Umasikini wa kipato ni mkubwa zaidi pale
ambapo wananchi wengi zaidi wanaishi vijijini (33.3%) ikilinganishwa na mijini
(21.7%). Mfano: Mwaka 2000/01 umaskini wa Kipato mkoa wa Mwanza ulikuwa 48%.
Baada ya kugawanywa na kutolewa Wilaya ya Geita ambayo ilikuwa inaongoza kwa
Umaskini wa Kipato 62.3% na kuwa Mkoa mpya wa Geita kiwango cha umasikini Mkoa
wa Mwanza kinaonekana kupungua kutoka 43% (2000/01) hadi 35% (2011/12). Aidha, kwa
mkoa wa Geita, sababu mojawapo ya umasikini wa kipato (44%) ni kiwango kikubwa
cha uzazi (wastani wa watoto 7 kwa kila mwanamke mwenye umri wa kuzaa). Hivyo,
shughuli za kiuchumi zinaelemewa na ongezeko kubwa la idadi ya watu (population
explosion).
Aidha,
wilaya za Kwimba na Sengerema umaskini wa kipato ni 39% na Misungwi 50% mwaka
2011/12. Wilaya za Mijini ambazo ni Nyamagana na Ilemela umaskini wa kipato ni 17%
na 15%. Hivyo wananchi wengi vijijini
kutegemea kilimo, ufugaji na uvuvi usio na tija, havitoshi kupunguza umaskini
wa kipato kwa kasi inayotakiwa. Hivyo, zitahitajika jitihada za makusudi
kuongeza tija katika shughuli za msingi za kiuchumi vijijini.
Mheshimiwa Spika,
umasikini katika mkoa wa Kigoma unachangiwa na miundombinu hafifu ya
usafirishaji ambao unapunguza fursa za masoko. Pia Kigoma inabeba mzigo mkubwa
wa wakimbizi na hivyo kusababisha ziada inayozalishwa kutumika zaidi kulisha
wakimbizi na kupunguza ustawi wa Kaya katika mkoa husika.
·
Kwa mikoa ya Lindi na Mtwara umaskini huenda
umepungua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za biashara na uchumi kufuatia ugunduzi
wa gesi asilia na ujenzi wa Kiwanda cha Saruji.
Aidha, ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka kwa mikoa hii ni chini ya wastani
wa Taifa wa 2.7%. maana yake ni kuwa kinachozalishwa kinatumika katika
kustawisha uchumi katika kaya zao.
·
Mheshimiwa Spika, kwa
mkoa wa Pwani, Wakazi wake wengi wanafanyia shughuli zao za kuongezea kipato
katika Jiji la Dar es Salaam ambalo lina fursa nyingi Kiuchumi. Kadhalika,
Pwani imepata fursa nyingi za Wakazi wake kujiongezea kipato chake kutokana na
kuimarika kwa miundombinu ya barabara, maji na umeme ambazo ni vichecheo vya
kuinua kipato cha Mwananchi mmoja mmoja.
Hoja Na. 6 Wizara ya Fedha na Mipango iangalie upya kuondoa misamaha
ya kodi kwenye taasisi za dini kwa kuwa zinatoa huduma za kijamii kama shule,
hospitali, n.k.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Baada
ya kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali pamoja na waheshimiwa wabunge, utaratibu
niliopendekeza kwa taasisi za kidini kulazimika
kulipa kodi kwanza kwa bidhaa watakazonunua au kuagiza nje na kodi hiyo kurejeshwa baada ya ukaguzi kufanyika
na kujiridhisha kuwa bidhaa hizo zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa umeonekana
unaweza kukwamisha au kuchelewesha utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na taasisi za kidini na
kusababisha athari katika upatikanaji
wa
huduma muhimu kwa jamii. Kwa kutambua mchango mkubwa wa taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za
elimu na afya, napendekeza kufuta utaratibu niliotangaza
katika hotuba ya bajeti na badala yake Serikali itaimarisha zaidi hatua mbalimbali
za udhibiti wa misamaha ya kodi kama ifuatavyo:
i.
Taasisi
za kidini kuwasilisha vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila
mwanzo wa mwaka wa kalenda, na kuthibitisha kama vifaa vilivyopewa msamaha
mwaka uliopita vilitumika kama sheria inavyotaka;
ii.
Kuwasilisha
majina ya watu walioidhinishwa na Shirika au Taasisi kuandika barua za kuomba
msamaha wa kodi, wakiainisha cheo, saini, picha, anwani na namba zao za simu.
Taarifa hizo ni muhimu katika kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia
bidhaa zilizoombewa na kupewa msamaha kama zimepata kibali cha taasisi hizo na
zimetumika kutekeleza miradi iliyotarajiwa.
Pia wanapaswa kuandika barua ya kumuidhinisha wakala wa forodha
waliomteua kutoa mizigo itakayokuwa ikiagizwa kutoka nje;
iii.
Kila
wanapoomba msamaha wanapaswa kupata barua kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Serikali
ya Mtaa na Mkuu wa Wilaya mahali Taasisi au Mradi unaotekelezwa ulipo ili
kuthibitisha kuwepo kwa Taasisi au mradi na mahitaji ya vifaa vinavyoombewa
msamaha;
iv.
Magari
yanayoagizwa kwa msamaha yawe na namba na rangi maalum za utambuzi mfano: TEV
222 AXZ kama njia ya kudhibiti matumizi yake; na
v.
Taasisi
ya dini itakayothibitika kutumia vibaya msamaha wa kodi itafutiwa usajili na
Serikali.
·
Mheshimiwa Spika, utaratibu
na hatua mbalimbali za udhibiti wa misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara,
watumishi wa umma na taasisi zisizo za kiserikali utatangazwa katika gazeti la
Serikali na kupitia vyombo vya habari.
Hoja Na.7: Uwezo wa TRA kukusanya Kodi ya Majengo
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika,
·
TRA ni
mamlaka ambayo ina uzoefu wa kutosha katika ukusanyaji kodi za Serikali na ina
vituo vya ukusanyaji kodi katika Wilaya na Mikoa yote Tanzania;
·
TRA
inatekeleza majukumu yake kupitia sheria mbalimbali ambazo zinarahisisha ukusanyaji
wa kodi kwa kupitia utaratibu wa kisasa wa Benki pamoja na njia za
kielektroniki. Aidha, Kamishna Mkuu anaruhusiwa kama ataona inafaa, kuazima
baadhi ya watumishi wenye uzoefu wa utozaji kodi ya majengo toka maeneo mengine
ya serikali ikiwemo serikali za mitaa kwa lengo la kujenga ushirikiano na
kuongeza ufanisi; na
·
Kwa
kutumia uzoefu na mifumo iliyopo ya TRA, ni wazi kuwa kodi ya majengo
itakusanywa kwa ufanisi mkubwa na kwa uwazi zaidi, tofauti na sasa ambapo
wananchi wengi hawalipi kodi hiyo.
Kuhusu Viwango vya Kodi ya Majengo
·
Waziri wa Fedha na Mipango ataweka viwango
vya kodi ya majengo baada ya kushauriana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI ili kuweka uwazi na kujumuisha maoni ya wadau wote muhimu zikiwemo
Halmashauri husika; na
·
Kodi ya majengo itatozwa kwa kuzingatia
mazingira ya maeneo husika ambapo TRA itakuwa na jukumu la kutoza, kukusanya na
kuwasilisha makusanyo hayo kwenye akaunti maalumu kwa manufaa ya serikali za
mitaa.
·
Mapato kutokana na kodi ya majengo
yataingizwa katika mfuko mkuu. Mawaziri wenye dhamana ya Fedha na TAMISEMI
watashauriana kuhusu mgawanyo wa fedha hizo kwa kuzingatia bajeti za
Halmashauri husika.
Hoja Na.8: Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika Huduma za
Utalii
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Kabla ya hotuba ya bajeti ya 2016/17 nchi zote wanachama wa Jumuiya Afrika
Mashariki zilikuwa zinatoza VAT kwenye huduma ya utalii isipokuwa
Tanzania ambayo imependekeza kutoza katika bajeti yake ya mwaka 2016/17;
·
Mwaka 2014 Serikali kupitia Bunge ilitunga
sheria ya VAT. Sheria hii ilitungwa ili kutatua upungufu
uliokuwepo katika sheria ya VAT ya mwaka 1997;
·
Msamaha wa VAT kwenye huduma za utalii
ulifutwa mwaka 2014 baada ya kukubaliana na wadau ambao waliiomba Serikali
mwaka moja toka Novemba 2014 ili kulinda mikataba iliyoingiwa kabla ya
kutunga sheria ya VAT ya mwaka 2014;
·
Idadi ya watalii waliotembelea mbuga za
wanyama kwa kipindi 2011 hadi 2014 katika nchi za Tanzania, Kenya na Afrika
Kusini zinaonyesha kwamba Tanzania licha ya kutotoza VAT kwenye huduma hii bado
imetembelewa na watalii wachache kuliko nchi hizo kama ifuatavyo:
Mwaka
|
Idadi
ya Watalii
|
||
Tanzania
Hakuna
VAT
|
Kenya
Kuna
VAT
|
Afrika
Kusini
Kuna
VAT
|
|
2011
|
867,994
|
1,750,000
|
8,339,000
|
2012
|
1,077,058
|
1,619,000
|
9,188,000
|
2013
|
1,095,884
|
1,434,000
|
9,537,000
|
2014
|
1,140,156
|
1,261,000
|
9,549,000
|
Serikali inapendekeza kutoza VAT kwenye
huduma za utalii kwa sababu VAT sio kigezo kikubwa kinachoangaliwa na Mtalii
wakati anafanya maamuzi kufanya utalii. Baadhi ya vigezo muhimu vinavyoangaliwa
ni vivutio, usalama, huduma kwa watalii na hali ya usafiri.
Hoja Na.9: Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na tatizo la
watoa huduma kutoza bei kwa kutumia fedha za kigeni kama Dola ambalo
linapelekea kushuka kwa thamani ya shilingi?
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Dollarization ni
matumizi ya sarafu ya kigeni katika nchi moja sambamba na sarafu ya nchi hiyo;
·
Matumizi makubwa ya fedha za kigeni katika
uchumi husababishwa na mambo kadhaa yakiwemo vita vya muda mrefu katika nchi,
kuongezeka kwa mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya nchi
husika ikilinganishwa na sarafu ya kigeni. Kama nilivyoeleza katika hotuba
yangu, kushuka kwa thamani ya shilingi yetu kulitokana na kuimarika kwa Dola ya
Kimarekani, kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha za kigeni kwa ajili ya bajeti ya
serikali pamoja na mapato madogo ya fedha za kigeni yasiyokidhi mahitaji ya
uagizaji wa bidhaa na huduma nje;
·
Kwa ujumla, mahitaji ya fedha za kigeni kwa
ajili ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi hayawiani na uuzaji wa bidhaa
na huduma nje. Kwa mfano katika mwaka 2015, thamani ya mauzo ya bidhaa na
huduma nje ilikuwa Dola za Kimarekani milioni 9,450.0 ikilinganishwa na Dola
milioni 12,528.2 zilizotumika kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje. Hali hii
inasababisha kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa na huduma;
Mwenendo wa thamani ya Shilingi umekuwa ni
chanzo kikuu kwa wafanya biashara nchini kupanga bei za bidhaa na huduma zao
kwa fedha za kigeni. Hivyo basi, namna nzuri na endelevu ya kupunguza au
kuondoa matumizi ya fedha za kigeni katika matangazo ya bei au malipo ya bidhaa
na huduma mbalimbali kwenye soko la ndani ni kuimarisha thamani ya Shilingi
yetu na kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei. Hali hii itawezekana kwa kuendelea
kutekeleza sera madhubuti ya fedha na kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la
uzalishaji wa chakula pamoja na kuboresha usambazaji wa chakula nchini. Hii
inajumuisha pia kuboresha miundombinu itakayowezesha kilimo cha umwagiliaji na
kusafirisha chakula kirahisi kutoka sehemu zenye ziada kwenda sehemu zenye
upungufu;
·
Aidha, kuongeza uzalishaji wa bidhaa za
mauzo nchi za nje kutapunguza nakisi katika urari wa biashara ya bidhaa na
huduma nchi za nje na hivyo kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa thamani ya
Shilingi. Hivyo basi, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni (dollarization) ni suala la muda wa kati
linalohitaji kuimarisha sera madhubuti za uchumi jumla ikiwa ni pamoja na
kuendelea kuweka mifumo thabiti itakayoleta ongezeko la haraka la uzalishaji
wenye tija na hivyo kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje;
·
Si nia ya Serikali kurejesha sera ya
udhibiti wa umiliki wa fedha za kigeni (administrative
de-dollarisation) kwani madhara yake ni makubwa na baadhi ya nchi
zilishajaribu zikashindwa na hivyo kurudisha sera ya soko huria. Udhibiti wa
umiliki wa fedha za kigeni utaleta
ushawishi kwa watanzania
kutunza fedha za kigeni katika mabenki ya nje kinyume na sheria (capital flight). Hii itasababisha
upungufu mkubwa wa fedha za kigeni na hivyo kufanya nchi
kushindwa kulipia mahitaji yake kutoka nje. Pia, hali hii itasababisha kushamiri kwa soko lisilo rasmi (parallel market) la fedha za kigeni cf. IMF (2015) Dollarization in
SSA: Experience and Lessons;
·
Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu
kuhakikisha kwamba matumizi ya fedha za kigeni katika uchumi wetu yanafanyika
kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria. Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006,
sehemu ya tatu, kipengele cha 26, inatamka wazi kuwa shilingi ya Tanzania
itakubalika na kutumika kama fedha halali kwa malipo (legal tender) ndani ya
nchi yetu. Hii inamaanisha kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo
haiwezi kukataliwa na mtu yeyote kwa malipo halali ndani ya nchi yetu. Hivyo, ni kosa kukataa kupokea shilingi ya
Tanzania kwa malipo halali nchini; na
·
Vile vile, Sheria ya Usimamizi wa Fedha za
Kigeni ya mwaka 1992 (The Foreign
Exchange Act, 1992) inaruhusu mtu yeyote kupokea, kumiliki na kutumia fedha
za kigeni kwa shughuli zake za kiuchumi. Vile vile, Sheria hiyo inatamka kwamba
mtu yeyote anaruhusiwa kuwa na akaunti ya fedha za kigeni katika benki
iliyoruhusiwa na Benki Kuu kwa ajili hiyo.
Hoja Na.10: Serikali
ipunguze kukopa katika mabenki ya ndani ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kupata
mikopo.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Nakisi
ya bajeti kwa mwaka 2016/17 ni asilimia 4.5 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na
asimilia 3.7 mwaka 2013/14, asilimia 3.6 mwaka 2014/15 na asilimia 4.2 mwaka
2015/16. Kiwango cha nakisi ya bajeti kimeongezeka kwa asilimia 0.3 ya Pato la
Taifa ikilinganishwa na mwaka 2015/16. Ongezeko hilo limetokana na nia nzuri ya
Serikali ya kutekeleza kwa dhati Mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano;
·
Kigezo
kimojawapo cha uchumi mpana katika kuanzishwa kwa Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, ni kuwa na kiwango cha nakisi ya bajeti kwa Pato la Taifa cha
asilimia 3 pindi ifikapo 2021/22. Katika kutekeleza hili, Serikali imepanga
kupunguza kiwango cha nakisi hatua kwa hatua bila kuathiri utekelezaji wa bajeti;
·
Katika
mwaka 2016/17, Serikali imepanga kuziba nakisi ya bajeti ya asilimia 4.5 ya
Pato la Taifa kwa kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi
hicho, asilimia 3.0 ya Pato la Taifa itakopwa kutoka vyanzo vya nje na asilimia
1.5 ya Pato la Taifa itakopwa kutoka katika vyanzo vya ndani. Ukopaji huo
hufanyika kwa kuuza hatifungani kwenye soko la ndani la fedha badala ya kukopa
moja kwa moja kwenye benki za biashara; na
·
Kwa
maana hiyo, kiasi kitakachokopwa kutoka soko la ndani kinazingatia ukomo wa
ukopaji ambao hauathiri utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi ambapo mikopo kwa
sekta binafsi imekuwa ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 kwa mwaka. Ongezeko
hili linawiana na lengo la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kama
ilivyoainishwa katika Tamko la Sera ya Fedha. Aidha, kiwango cha mikopo ambayo
imekuwa inayotolewa na benki za biashara kwa sekta binafsi ni zaidi ya asilimia
80 ya mikopo yote, wakati mikopo inayotolewa na benki za biashara kwa Serikali
ni chini ya 2%
Hoja Na. 11: Kuondolewa kwa misamaha
ya kodi katika maduka na migahawa ya vyombo vya ulinzi na usalama kunaondoa
motisha katika taasisi hizo. Ikiwa msamaha wa kodi utafutwa, bidhaa na vifaa
vilivyopo katika bohari za majeshi yetu zitapelekwa wapi? Na zipo kiasi gani?
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Uamuzi wa Serikali wa kuwapa motisha
watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama bado upo palepale. Mapendekezo ya
kuondoa msamaha wa kodi katika maduka na migahawa ya vyombo vya ulinzi na
usalama ni kutokana na misamaha hiyo kutumika vibaya. Ili kuondoa kasoro hiyo,
Serikali imeamua kuweka utaratibu wa kuwalipa posho watumishi wa vyombo vya
ulinzi na usalama ili wanufaike moja kwa moja kama walengwa. Kiasi cha posho
atakayolipwa askari kitakokotolewa baada ya mashauriano na vyombo husika.
·
Serikali inakamilisha utaratibu wa bidhaa
ambazo zimesamehewa kodi katika maduka yote ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Utaratibu huo utakapokamilika wahusika watajulishwa.
Hoja Na.12: Kodi kwenye “transit goods” ni kinyume na taratibu kwa
kuwa kodi hiyo hulipwa na mlaji. Hii itasababisha waagizaji wa mizigo kuhamia
bandari nyingine za Beira na Mombasa.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Sheria ya VAT ya Mwaka 2014 imeweka viwango
viwili vya kutoza kodi ambavyo ni asilimia 18 kwa bidhaa na huduma zinazotumika
hapa nchini na asilimia 0 pale bidhaa na huduma inaposafirishwa nje ya nchi
(Exported);
·
Huduma zinazotolewa kwenye mizigo
inayosafirishwa kwenda nchi za jirani kupitia Tanzania siyo “exports” bali
zinatolewa na kutumiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana kodi
ya ongezeko la thamani (VAT) haitozwi kwenye transit goods bali hutozwa kwenye
huduma ambapo mtumiaji na mtoaji wako Tanzania.
Huduma hizi zinaweza kutolewa mahali popote ndani ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na siyo bandarini tu, na hivyo ni sahihi kabisa huduma hizi kutozwa
asilimia 18;
·
Utafiti uliofanywa kubaini kama kutoza kodi
ya VAT huduma hizi kunaathiri biashara kwenye bandari umeonesha kwamba katika
kipindi cha Julai, 2015 hadi April, 2016 mizigo iliyopita kwenye bandari ya Dar
es Salaam imepungua kwa asilimia 15 ukilinganisha na mizigo iliyopita katika
Mwaka wa Fedha 2014/15 katika kipindi kama hicho. Katika Bandari ya Mombasa ambapo huduma hizi
zimesamehewa kodi ya VAT mizigo imepungua kwa asilimia 25 katika kipindi hicho. Kwa ujumla biashara ulimwenguni kote imeshuka
katika kipindi hiki, na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi jumla; na
·
Kwa misingi hiyo si sahihi kusema kwamba
kutoza kodi ya VAT kwenye huduma zinazotolewa kwenye mizigo inayosafirishwa
kwenda nchi jirani ndicho chanzo cha kushuka kwa biashara katika bandari zetu.
Hoja Na.13: Serikali iangalie upya mfumo wa “Single Customs
Territory” unaodaiwa kusababisha kupungua kwa mapato ya bandari kutokana na
baadhi ya nchi jirani kuepuka kutumia bandari ya Dar es Salaam.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Mfumo wa “Single Customs Territory (SCT)”
ulianza kutumiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mfumo huu
ulionesha manufaa makubwa katika kuwezesha biashara na kudhibiti uvujaji wa
mapato baina ya nchi husika. Mfumo huu huruhusu wafanyabiashara wanaotumia
bandari zetu kupitisha mizigo kwenda nchi jirani kulipa kodi kwenye nchi zao
kwanza na pindi mzigo huo unapowasili bandarini na kujiridhisha kuwa kodi
husika zimelipwa, mzigo huo huruhusiwa na hivyo kuepusha uwezekano wa kuingizwa
nchini bila kulipiwa kodi. Utaratibu huu pia hurahisisha uondoshaji wa kadhia forodhani.
Mfano mzuri wa mafanikio ya mfumo huu ni mizigo inayokwenda Rwanda kwani
imeongezeka kwa asilimia 16 kwa kipindi cha kuanzia Julai 2015 hadi Aprili 2016
ukilinganisha na kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia muda
wakusafirisha mzigo kutoka muda wa kuingia na kutoka (from entry to exit) umepungua;
·
Mfumo huu wa SCT kwa mizigo inayokwenda
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeanza kutumika kufuatia makubaliano
kati ya serikali za nchi hizi mbili.
Lengo lake ni kuharakisha biashara kwa kupunguza muda wa kutoa na
kusafirisha mizigo kwenda DRC na kudhibiti mapato kwa nchi zote mbili. Hivyo
kushuka kwa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani hakujasababishwa na SCT;
·
Kwa upande mwingine, dunia imeshuhudia
kupungua kwa biashara ya kimataifa katika kipindi hiki ambako kumesababishwa na
kudorora kwa uchumi wa China, kushuka kwa bei ya bidhaa (commodities) na mafuta
ikiwa pamoja na madini mbalimbali. Hivyo, kupungua kwa mizigo inayokwenda nchi
jirani na ile inayotumika hapa nchini, hakujaiathiri Tanzania peke yake bali
hata bandari ya Mombasa mizigo ya nchi jirani yaani transit ilipungua kwa asilimia 25 kwa kipindi cha kati ya Julai
2015 hadi Machi 2016 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2014/15.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na TRA/Serikali umebainisha sababu za muda
mfupi na muda mrefu zilizosababisha kupungua kwa mizigo kwenye bandari ya Dar
es Salaam ikiwa ni pamoja na mizigo inayokwenda nchi jirani na ile kwa ajili ya
matumizi ya ndani ya nchi (imports);
·
Sababu za muda mfupi ni pamoja na:-
Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu kwenye Nchi za kanda yetu kama vile Tanzania,
Uganda, Burundi, machafuko nchini Burundi na Sudan Kusini, kushuka kwa bei ya shaba katika soko la dunia
kuliathiri uchumi wa Zambia na hivyo kushuhudia kupungua kwa mizigo ya kwenda
na kutoka Zambia, na maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na nchi ya Msumbiji
na Afrika kusini kwa mfano Msumbiji imejenga reli ya standard gauge na kuboresha bandari na hivyo kuifanya bandari kuwa
na miundombinu bora ukilinganisha na bandari yetu. Hali hii imeifanya bandari ya Beira kupendelewa zaidi
na nchi jirani;
·
Sababu za muda mrefu ni pamoja na:- Ufanisi
mdogo wa bandari ya Dar es Salaam ukilinganisha na bandari zingine, miundombinu
hafifu ya kusafirisha mizigo hususan kwa njia ya reli na hivyo kufanya njia
pekee ya uhakika kusafirisha mizigo kuwa ni barabara ambayo ni ghali zaidi
ukilinganisha na reli; na
·
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria
kikamilifu kuondokana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za
bandari na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na kujenga
reli ya kati kwa kiwango cha standard
gauge.
Hoja Na.14: Tamko la kufuta retention kwenye Taasisi za kimkakati
kama TPDC, Serikali ikishindwa kupeleka fedha kwa wakati, itapoteza mapato
mengi kwa sababu watashindwa kusimamia kwa ufanisi mapato kutoka kwa
wawekezaji.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
Utaratibu
wa kubakiza sehemu ya mapato (Retention) ulikuwa na lengo la kuongeza ufanisi
katika utekelezaji wa shughuli kwa baadhi ya Wizara na Taasisi. Katika baadhi ya Wizara na Taasisi hizo
ufanisi wa ukusanyaji maduhuli umeongezeka;
·
Hata hivyo, kumejitokeza dosari katika
utekelezaji wa utaratibu huo, ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa yasiyowiana
na majukumu ya msingi na kutochangia inavyostahili katika mfuko mkuu wa
Serikali; na Ili kurekebisha dosari na kuhakikisha kuwa
Taasisi husika zinapata fedha kwa wakati, Serikali imeelekeza Taasisi hizo
kuwasilisha mpango kazi na mtiririko wa mahitaji ya fedha (action plan and cash
flow), vigezo ambavyo vitazingatiwa katika utoaji wa fedha
Hoja Na. 15 Ushuru wa Forodha kwenye Sukari ya Viwandani
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Katika
ukurasa wa 71
kwenye kitabu cha Hotuba ya Bajeti 2016/17 niliyoisoma hapa Bungeni nilieleza
kuwa, waagizaji wa sukari ya viwandani watatakiwa kulipa ushuru wa asilimia 15
kwenye sukari wanayoagiza badala ya asilimia 10 wanayolipa sasa katika mwaka wa
fedha 2015/16. Hilo lililenga kutekeleza
maamuzi ya Baraza la Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya fedha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki ya kupunguza msamaha kwenye sukari ya viwanda hatua kwa hatua
hadi kufikia asilimia 25 kama ifuatavyo: mwaka 2016/17 kiwango kitakuwa
asilimia 15, 2017/18 kiwango kitakuwa cha asilimia 20 na 2018/19 kiwango
kitakuwa asilimia 25.
·
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa
maamuzi ya kuanza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 15 kwenye sukari
inayoingizwa nchini kwa matumizi ya viwanda ulikuwa ni uamuzi wa pamoja wa
mawaziri wenye dhamana ya masuala ya
fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ni Tanzania
pekee ndiyo ingetekeleza maamuzi haya katika mwaka wa fedha 2016/17. Nchi za Burundi, Kenya na Uganda zimeomba
muda wa kujiandaa ili waweze kuanza kutekeleza hatua hii katika mwaka wa fedha
2017/18. Rwanda wanatumia mfumo tofauti ambapo sukari yote hutozwa asilimia 25
badala ya kutumia ushuru wa forodha wa asilimia 100 au Dola za Marekeni 460 kwa
tani moja kwa kutegemea kiwango kipi ni kikubwa zaidi. Sababu ya nchi hizi
kutotumia kiwango hicho cha ushuru wa forodha ni ukweli kuwa bidhaa hizi
hazizalishwi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha,
ili kujiandaa kwa utekelezaji wa hatua hii, Kenya imepewa unafuu wa
ushuru wa forodha kwa kuruhusiwa kuingiza sukari ghafi kwa kutumia kiwango
cha asilimia 0 badala ya asilimia 100 au
Dola za Marekani 460 kwa tani kwa kipindi cha mwaka mmoja. Baada ya kupokea maoni ya watengenezaji wa
vinywaji pamoja na kutafakari juu ya umuhimu wa bidhaa hiyo ambayo hutumika
kama malighafi ya viwanda vyetu, Serikali imeamua kusitisha utekelezaji wa
hatua hii hadi mwaka wa fedha 2017/18 kama ilivyo kwa nchi nyingine za Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Hata hivyo,
Serikali itaendelea kuwataka watumiaji wa sukari hii kuendelea kulipia kodi ya
asilimia 25 kwanza na kurejeshewa asilimia 15 baada ya kuthibitisha uhalali wa
matumizi.
Hoja Na.16: Wizara ya Fedha
na Mipango ijihadhari na madalali wa mikopo (transaction agents) maana
wataongeza gharama za mikopo.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Ukopaji wa fedha unafanywa kwa mujibu wa
Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura
134. Sheria hiyo imetoa Mamlaka kwa Waziri wa Fedha na Mipango kukopa
mikopo ya ndani na nje kwa niaba ya Serikali. Kwa mujibu wa taratibu
zilizoainishwa katika sheria hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango hujadiliana moja
kwa moja na wakopeshaji ambao wanaweza kuwa ni Nchi (Bilateral Creditor), Benki
moja moja au kundi la mabenki;
·
Hata hivyo, kutokana na muundo (structure)
wa soko la fedha la ndani au la kimataifa, wakati mwingine Waziri wa Fedha
anaweza akateua taasisi nyingine kumsaidia ili kurahisisha upatikanaji wa fedha
kutoka soko la fedha husika. Mathalan, kwa sasa Benki Kuu ya Tanzania inatumika
kama wakala (Agent) wa Serikali katika kuuza Hati Fungani na Dhamana za
Serikali na kuiwezesha Serikali kupata Fedha kutoka Soko la Ndani;
·
Kwa upande wa soko la fedha la kimataifa,
mikopo mikubwa huchangiwa na taasisi nyingi za fedha yakiwemo mabenki na
wakopeshaji wengine. Taasisi hizo huteua benki au taasisi moja miongoni mwao
kuwa Wakala yaani Agent/lead arranger au
lead manager kuwasikilisha mabenki hayo katika majadiliano na mkopaji. Huu
ni utaratibu wa kawaida kwenye masoko ya fedha ya kimataifa na hufanya hivyo
ili kurahisisha majadiliano na upatikanaji wa fedha kwa wakati;
·
Sifa za Wakala huyo anayechaguliwa na
mabenki au wawekezaji kwenye soko la fedha la kimataifa lazima ni pamoja na
kuwa uwezo wa kuitangaza nchi kikamilifu katika soko la fedha la kimataifa
hivyo kuifanya nchiyo kupata fedha na kwa gharama nafuu ya soko, kwa upande
mwingine, Wakala huyo anatakiwa awe na taarifa za kutosha za mkopaji ikiwemo
hali ya uchumi, siasa na masuala ya kijamii ya nchi husika na uwezo wa nchi hiyo
kurejesha mikopo. Aidha, mkopaji lazima ajiridhishe na kukubali kutumia Wakala
huyo; na
·
Utaratibu huu hutoa uhakika kwa Serikali
kupata mikopo kwa masharti yanayokubalika baina ya pande mbili zinazo husika.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Sheria hii imeweka
utaratibu maalum wa kuufuata wakati wa kukopa. Kwa mujibu wa Sheria hii kuna
Kamati Maalum ambazo huchambua masharti ya kila mkopo na kujadiliana na
wakopeshaji na baada ya majadiliano kukamilika, Kamati hizi ndizo zinamshauri
Waziri wa Fedha na Mipango kukopa mkopo husika.
Hoja Na.17: Serikali ishirikishe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti
katika maandalizi ya bajeti.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·
Serikali imekuwa ikiishirikisha Kamati ya
Bunge ya Bajeti na Waheshimiwa Wabunge katika hatua mbalimbali za maandalizi ya
bajeti. Ushirikishwaji huo hufanyika katika hatua zifuatazo:
·
Maandalizi ya Mwongozo wa Mpango na Bajeti
Kamati za Kudumu za Bunge za Kisekta; na
·
Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambayo
hushirikishwa kikamilifu katika kuchambua makadirio ya bajeti ya Serikali;
kupitia rasimu ya mfumo wa bajeti; kupitia hoja za kibajeti zinazoibuka kwenye
sekta mbalimbali; kushauriana na Serikali kuhusu vyanzo vipya vya mapato.
·
Hata hivyo, ili kulinda kazi ya Bunge ya
kuishauri na kuisimamia Serikali ni muhimu kwamba Bunge lisijiingize katika
kazi za kiutendaji katika maandalizi ya bajeti na badala yake Bunge lichambue
na kushauri kuhusu mapendekezo ambayo tayari yanakuwa yameridhiwa na Serikali.
F: HITIMISHO
8.
Mheshimiwa
Spika, tuna dhamana ya
kuleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa shughuli zote za umma na
matumizi ya rasilimali za Taifa ili kuwezesha kupiga hatua kubwa ya kuiondoa
nchi yetu katika umaskini. Katika hili, kila mwananchi atambue wajibu wake wa kufanya kazi kwa bidii, kuwa
na nidhamu ya hali ya juu katika nyanja zote na uzalendo kwa Taifa letu.
9.
Mheshimiwa Spika, nirudie tena kuzielekeza Wizara, Idara zinazojitegemea,
Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa kuzingatia hatua za kuimarisha ukusanyaji wa mapato; usimamizi wa
matumizi ya Serikali na hatua za kupunguza gharama; na kulipa na kuzuia
ongezeko la madeni ya Serikali. Serikali ina dhamira ya dhati kabisa ya kuchukua hatua hizo na ninaomba Watanzania
wote watambue kwamba ni lazima kujinyima, kujituma na kuvuja jasho ili kupata
maendeleo na kupunguza utegemezi. Wajibu wa kwanza wa kuiendeleza Tanzania ni
wa Watanzania wenyewe. Tuna akili za kutosha, rasilimali nyingi na fursa tele
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na Uchumi wa Kipato cha Kati ifikapo
2025.
10.
Mheshimiwa
Spika, ninawaomba tena
Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hatua zinazoongozwa na Serikali ya Awamu ya
Tano kuhakikisha kuwa tunaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya kodi na
yasiyo ya kodi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo yenye tija kwa manufaa ya
watanzania wote.
11.
Mheshimiwa
Spika,
naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment